MAPISHI: Namna ya kupika makaroni
Na MARGARET MAINA
Muda wa kuandaa: Dakika 5
Muda wa mapishi: Dakika 20
Walaji : 3
Vinavyohitajika
- makaroni pakiti moja
- chumvi
- siagi
- vitunguu saumu (utaviponda)
- tangawizi (utaiponda)
- pilipili
- tui la nazi
Maelekezo
Tayarisha sufuria safi, weka maji ya kutosha. Ongeza chumvi kiasi na pilipili manga iliyosagwa.
Bandika mekoni na acha mpaka maji yachemke.
Weka makaroni kwenye maji yaliyochemka. Japokuwa maelekezo kwenye pakiti nyingi yanasema kuwa muda wa kupika ni dakika 10, hakikisha uivaji kwa kuyaonja. Baada ya kuiva, epua sufuria.
Tayarisha chujio na mimina makaroni ndani ya chujio ili kuchuja maji uliyochemshia makaroni.
Chukua maji yasiyo moto wala baridi miminia juu ya makaroni yakiwa bado ndani ya chujio.
Rejesha sufuria uliyochemshia makaroni mekoni huku ukiwa umepunguza sana moto.
Weka siagi ndani ya sufuria yako na iacha iyeyuke vyema. Rejesha makaroni ndani ya sufuria yenye siagi. Waweza ongeza pilipili manga iliyosagwa kama ukipenda.
Koroga vizuri kabisa kwa dakika mbili ili mchanganyiko wa makaroni, pilipili manga na siagi ukolee barabara.
Mackaroni yako yapo tayari kwa kuchanganywa na mboga.
Epua sufuria kisha pakua kwa kuku au chochote ukipendacho.