MAPISHI: Pilau ya kuku
Na MARGARET MAINA
MUDA wa kuandaa: Dakika 15
Muda wa kupika: Dakika 30
Walaji: 3
Vinavyohitajika
· Mchele wa biriani nusu kilo
· Kuku 1
· Mafuta ya kupikia
· Vitunguu maji 2
· Karoti 2
· Pilipili mboga
· Tangawizi
· Viungo vya pilau
· ‘Punje’ 5 za kitunguu saumu
· Chumvi
· Nyanya 3
Maelekezo
Kata nyama ya kuku iwe vipande utakavyopenda na uipike ukiwa umeongezea chumvi. Hakikisha supu ya kupikia chakula inatosha.
Menya vitunguu maji ukatekate, vitunguu saumu vimenye kisha utwange pamoja na tangawizi. Zimenye karoti vilevile. Usisahau kuandaa pilipili yako kwa utaratibu uo huo.
Nyanya pia menya kisha ukatekate.
Bandika sufuria mekoni na utie mafuta ya kupikia. Yakichemka tia vitunguu uvikaange. Vikianza kubadilika rangi kuwa ya kahawia, weka vitunguu saumu na tangawizi mbichi. Koroga kisha weka pilipili mboga na karoti.
Kaanga kidogo kisha weka nyanya na uache ziive na vipande vya kuku. Koroga kama dakika tano kabla ya kuongezea viungo vya pilau.
Weka mchele, koroga kisha tia chumvi na umimine supu ile ya kuku kwenye wali.
Koroga kisha funika na uache chakula chako kiive. Baada ya dakika kumi angalia chakula chako kama maji yamekauka.
Kigeuze na baada ya dakika kadhaa angalia tena maana hapo chakula chako kitakuwa tayari kuliwa.
Pakua na ufurahie.