MARY MUSYOKA: Lupita Ny'ong'o hunitia moyo
Na JOHN KIMWERE
ANAAMINI anacho kipaji cha kufanya vizuri katika tasnia ya maigizo na kutwaa tuzo za kimataifa kama Oscars na Grammys kati ya zingine.
Anasema amepania kujituma mithili ya mchwa ili kutimiza ndoto zake ikiwamo kukuza talanta za wasanii wanaoibukia.
Anadokeza kuwa analenga kufuata nyayo za waigizaji mahiri duniani kama Taraji Penda Henson maarufu Cookie mzawa wa Marekani. Msanii huyo alijizolea sifa tele kutokana na filamu zake maarufu kama ‘Empire,’ ‘What men want,’ ‘Baby boy,’ na ‘Hidden figures’ kati ya zinginezo.
Mary Kamanthe Musyoka ni kati ya waigizaji wanaokuja wanaopania kutinga hadhi ya kuigiza katika filamu za Hollywood ndani ya miaka michache ijayo. Kando na uigizaji, chipukizi huyu ni msomi wa mwaka wa tatu kwenye Chuo Kikuu cha Kenyatta (KU) anakosomea shahada ya digrii katika masuala ya elimu.Tayari anajivunia kuanzisha kampuni ya kuzalisha filamu kwa jina Making Things Happen.
Kadhalika anasema ana imani brandi hiyo itaibuka maarufu ndani ya miaka mitano ijayo. ”Bila kupaka mafuta kwenye mgongo wa chupa binafsi nilianza kuvutiwa na uigizaji tangia nikiwa mdogo,” anasema na kuongeza kuwa licha ya hayo alidhamiria kuwa mwimbaji.
Katika mpango mzima chipukizi huyu alianza kujituma katika masuala ya filamu mwaka wa 2017 chini ya kundi la Mwangaza Production. Pia anasema Lupita Ny’ong’o alimtia motisha zaidi kuendeleza talanta yake katika tasnia ya maigizo.
Anasema uigizaji ulimvutia alipomtazama msanii huyo kwenye kipindi cha Shuga ambapo alijaa imani kuwa anacho kipaji cha kushinda tuzo ya Oscars miaka ijayo. Hata hivyo anasema alitambua talanta yake akiwa mdogo maana alizoea kukariri mashairi nyumbani ambapo alikuwa anafurahi baada ya kuona jamii yake ikitabasamu.
Tangu mwaka 2017 chipukizi huyu anajivunia kushiriki filamu kadhaa ambazo zimepata mpenyo kupeperushwa kupitia runinga tofauti hapa nchini.
”Kiukweli ninashukuru maana nimebahatika kushiriki filamu kadhaa ikiwamo ‘Njoro wa Uba,’ ‘Selina,’ ‘Hullabaloo Estate,’ ambazo zimeonyeshwa kupitia Maisha Magic East,” alisema. Kadhalika ameshiriki filamu iitwayo ‘Aunitie boss’ ambayo hupeperushwa kupitia NTV inayomilikiwa na Kampuni ya Nation Media Group. Kadhalika ameshiriki filamu kama ‘Silence,’ ‘The Untold,’ na Sprinkles of Blood,’ kati ya zingine.
Kwa wasanii wa Afrika angependa kufanya kazi na waigizaji kama Liya Kebede (Ethiopia) na Benu Mabhena (Zimbabwe) walioshiriki filamu kama ‘The Good Shepherd’ na ‘Blood Diamond,’ mtawalia.
Anaponda maprodusa wa humu nchini kwa kutokuwa wabunifu pia kuongozwa na kasumba ya kutokuamini wapo wasanii waliotuzwa talanta ya uigizaji. ”Ingawa sijakomaa katika uigizaji sina budi kutaja kuwa taifa hili limefurika wasanii wengi tu wavulana na wasichana lakini wamekosa mwongozo ili kukuza talanta zao,” akasema.
Chipukizi huyu anatoa mwito kwa wasanii wenzake kuwa wanastahili kuwa wabunifu, wajifunze kujituma mzigoni pia wajiamini wanatosha mboga katika kazi zao. Pia anawashauri kuwa wanapaswa kufuata mwelekeo unaofaa wala wasikubali kushushwa hadhi na maprodusa mafisi.