Mashujaa Dei 2024: Mudavadi alivyomkaribisha Ruto kuhutubu badala ya Kindiki
KINYUME na ilivyotarajiwa katika maadhimisho ya Mashujaa Dei 2024, Naibu Rais mteule, Kithure Kindiki kumkaribisha Rais William Ruto kutoa hotuba, Mkuu wa Mawaziri, Musalia Mudavadi ndiye alitekeleza wajibu huo.
Prof Kindiki ndiye alimlaki Dkt Ruto pindi alipotua kwa helikopta ya kijeshi katika Kaunti ya Kwale, ambapo maadhimisho hayo yamefanyika.
Kwa mujibu wa itifaki za afisi ya urais, hafla za kitaifa rais hukaribishwa na naibu wake kuhutubia taifa.
Katika maadhimisho ya Mashujaa Dei mwaka huu, 2024, yaliyofanyika Kwale Stadium, Mkuu wa Mawaziri, Bw Mudavadi ndiye alitekeleza jukumu hilo.
Bw Mudavadi, hata hivyo, alitambua uwepo wa Prof Kindiki kama naibu rais mteule.
Licha ya kuwa Prof Kindiki ni Naibu Rais Mteule, bado hajaapishwa rasmi kwa wadhifa huo kwa sababu mahakama imepiga breki mchakato huo hadi kesi iliyowasilishwa na mawakili wa Naibu Rais aliyebanduliwa Rigathi Gachagua isikizwe.
Mahakama imeshatoa ilani kwamba kesi hiyo itasikizwa Jumanne, Oktoba 22, 2024 na kuna uwezekano kwamba maamuzi mapya yatatolewa.
Bw Mudavadi alionekana kukwepa masuala ya kisiasa, mazungumzo yake yakiegemea hatua ambazo Kenya imepiga baada ya kupata uhuru wa kujitawala 1963.
“Asasi za kiserikali, kuanzia bunge hadi idara ya mahakama zinaheshimu Katiba na sheria. Hiyo ni ishara ya demokrasia kukua,” Bw Mudavadi alisema.
Gachagua aling’atuliwa mamlakani kufuatia mswada uliowasilishwa na mbunge wa Kibwezi, Mwengi Mutuse ambapo Seneti ilimvua mamlaka kwa mashtaka matano kwa jumla ya kumi na moja aliyotuhumiwa.
Yanajumuisha ufisadi, kueneza siasa za kikabila na chuki, matumizi mabaya ya ofisi na mamlaka, kati ya mengine.
Bw Gachagua, hata hivyo, kupitia mawakili wake alipata amri ya kusimamisha Prof Kindiki kuapishwa kupitia Mahakama Kuu.
Naibu rais huyo anayeondoka ameapa kumenyana na maamuzi ya Seneti kortini, akisema ana imani na idara ya mahakama.
Kisiki kilichoko mbele ya Prof Kindiki kikiondolewa, ataapishwa rasmi kuchapa kazi kama naibu wa rais wa Jamhuri ya Kenya na majina yake kuchapishwa kwenye Gazeti Rasmi la Kiserikali.