Makala

Mashujaa Dei 2024: Ruto alibadilisha suti ya Kaunda na kuvalia rasmi kuhutubia taifa

Na SAMMY WAWERU October 20th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

KIONGOZI wa nchi, Dkt William Ruto anafahamika kwa kuvalia suti ya Kaunda ambayo baadhi ya viongozi na wananchi wameonekana kuiga fashioni yake ya mavazi.

Wapo wanaomkejeli kwa kutumia vazi hilo, jinsi anaongoza taifa na sera zake, na pia wapo wanaotaka kuonekana kama Rais.

Katika maadhimisho ya Mashujaa Dei 2024, Dkt Ruto alitua Kaunti ya Kwale ambapo sherehe hiyo ilifanyika akiwa amevalia suti ya Kaunda ya rangi nyeupe.

Akiwa ameandamana na mkewe, Mama wa Taifa Bi Rachael Ruto, kiongozi wa taifa alilakiwa na Naibu Rais mteule, Prof Kithure Kithure.

Porf Kindiki alikuwa ameandamana na Gavana wa Kwale, Bi Fatuma Achani, Waziri wa Biashara, Bw Salim Mvurya, na Katibu wa Usalama wa Ndani, Dkt Raymon Omollo.

Suti ya aina hiyo, upekuzi wa Taifa Dijitali unaonyesha katika duka la mavazi la The Salute Uniforms, Amerika inauzwa Dola 180 (USD).

Thamani hiyo, ikibadilishwa kuwa sarafu za Kenya ni zaidi ya Sh23, 000.

Muda mchache baadaye, alipowasili Uwanja wa Kwale kuongoza taifa katika maadhimisho ya Sikukuu ya Mashujaa, Rais Ruto alionekana amevalia mavazi mengine; suti rasmi, akiwa pia amefunga tai.

Kwenye hotuba yake, Dkt Ruto aliainisha miradi ya maendeleo anayotekeleza, ikiwemo bima tatanishi ya afya ya SHA|SHIF, ujenzi wa nyumba za bei nafuu, kati ya sera zingine chini ya utawala wa muungano wa Kenya Kwanza.