Matatizo ya ujauzito yaliyozalisha kilimo cha uyoga
ENDAPO kuna mwaka ambao utasalia kwenye kumbukumbu ya Consolata Njeri, ni 2017.
Akiwa anasaka riziki katika Kaunti ya Kakamega, alipata ujauzito uliomfungulia awamu nyingine ya maisha.
Alikuwa ameoleka, na mimba aliyoshika ilimsababishia mahangaiko chungu nzima.
Wakati huo, alikuwa akiendeleza kazi ya sana; kushona vitambaa vya meza, mapazia na virembesho vingine vya nyumba.
“Ilifikia mahali daktari akanishauri sikuwa na budi ila kutulia kwenye nyumba kwa sababu ya ujauzito wangu,” Njeri anasema.
Ushauri huo, ulitokana na hali aliyokuwa akipitia asijue ingebisha hodi awamu ya matatizo zaidi.
Anasimulia kwamba mume wake alimuacha, katika kipindi alichomhitaji zaidi.
Ole wake, isemwavyo katika jamii anayotoka – ya Mlima Kenya, hakuwa na budi ila kujituma kama mtoto wa mvulana.
Kodi za nyumba nazo zilirundikana, akikosa mbele wala nyuma.
Kutia msumari moto kwenye kidonda kinachouguza, Njeri anadokeza kwamba landilodi wa nyumba aliyoishi alimfungia mlango.
Isitoshe, alikuwa na watoto wengine kwenye ndoa majukumu yakimkodolea macho.
Mtoto wa kike akakosa mwelekeo, ila hakufa moyo.
Ni mcha Mungu na anaamini Mola hamwachi mja wake.
Njeri anaelezea kwamba msamaria mwema alijitokeza na kuwa mwokozi wake.
Alimpa nyumba, aliyoigeuza kuwa jukwaa la ukuzaji uyoga.
“Mwanzo, nilitangulia kwa kufanya utafiti kwenye intaneti na chaguo nililopata ni uyoga,” asema.
Vyumba vilivyomsitiri na familia yake, sasa akiwa ‘singo matha’, ndivyo alivitumia kukuza zao hilo.
Uyoga ni sehemu ya kuvu (fungi) inayotokea juu ya ardhi na kukuza vibufu vinavyofanana na mbegu ya mimea.
Aghalabu, huitwa mimea lakini si mimea, ni sehemu ndogo ya kuvu.
Alianzisha kilimo chake kwa mtaji wa Sh1, 800, hela alizopewa na mamake kukithi wanawe mahitaji muhimu ya kimsingi.
“Nilianza na magunia 200, ila mazao yote yakaathirika na ugonjwa (mold),” anaelezea, akikumbuka kukadiria hasara ya kima cha Sh50, 000, pesa ambazo angepata endapo angefanya mauzo.
Njeri anasema hakuwa na budi ila kurejea kwao Gatundu, Kaunti ya Kiambu.
Alianza upya, majukumu ya malezi yakimkaba koo.
Miaka saba baadaye, mama huyu ana kila sababu ya kutabasamu.
Njeri ndiye mwasisi wa Connie farm fresh ‘n’organic mushrooms, kampuni ya ukuzaji uyoga inayokua kwa kasi.
Uyoga, unasifiwa kutokana na virutubisho vyake vya Protini kuchukua mahala pa nyama.
Huku athari za mabadiliko ya tabianchi zikiendelea kukita mizizi, watu wanahimizwa kuwa na njia mbadala kupata kiini cha Protini ufugaji ukiathirika pakubwa hivyo kuhatarisha kiwango cha mifugo.
Njeri anaendeleza kilimo cha uyoga katika Kijiji cha Kairi, Gatundu.
Amefanikiwa kubadilisha dhana kuwa eneo hilo kinachopaswa kulimwa pekee ni mahindi, maharagwe na ufugaji wa ng’ombe wa maziwa na kuku.
Mkulima huyu hutoa mafunzo kwa kina mama na vijana kuhusu kilimo cha uyoga.
“Huhudumu na makundi ya kina wenye ari kukuza zao hili. Vijana wapo, ila wengi wao wametekwa na kero ya pombe. Baadhi ninapowapa ujira, wakipata mshahara siku inayofuata hawarejei kazini kwa sababu ya kutekwa nyara na unywaji mvinyo,” akafafanua wakati wa mahojiano shambani mwake Gatundu.
Njeri, vilevile, ametoa mafunzo kwa zaidi ya watu 60 wenye ulemavu, kupitia ufadhili wa shirika lisilo la kiserikali (NGO) linalojulikana kama Light for the World Organization.
Soko lake ni maduka ya kijumla kama vile matawi ya Naivas na Carrefour Kiambu na Nairobi, na pia City Park na High Range Nairobi.
Hali kadhalika, huuza mazao yake kupitia muungano wa Wakuzaji Uyoga Nchini, ndio Mushrooms Association of Kenya.
Ulaji uyoga unazidi kushabikiwa na wengi, mikahawa sasa ikianza kukumbatia zao hilo badala ya nyama.