MATHEKA: Bunge lafaa livunjwe kufuatia dai la hongo
Na BENSON MATHEKA
IKIWA kuna wakati ambao Wakenya wanafaa kutumia nguvu zao za kikatiba dhidi ya bunge basi ni sasa. Kuna kila sababu ya Wakenya wanaojali nchi yao kutumia nguvu za kisheria kuvunja bunge ambalo limeonyesha wazi kwamba haliwakilishi maslahi yao.
Nasema hivi kufuatia madai kwamba wabunge waliohongwa, ndani ya chumba cha mjadala bungeni ili wakatae ripoti ya kamati ya pamoja ya kilimo na biashara kuhusu kuingizwa kwa sukari ya magendo na yenye sumu nchini.
Inasikitisha kwamba hongo hiyo inadaiwa kupeanwa na baadhi ya wabunge kwa niaba ya watu fulani waliotajwa kwenye ripoti hiyo.
Inasemekana kuwa ripoti ilipendekeza baadhi ya mawaziri na maafisa wakuu wa serikali wachunguzwe zaidi kuhusu mchango wao katika uingizaji wa sukari hiyo.
Kinachodhihirika hapa ni kwamba waliotoa hongo hiyo kupitia wabunge ni watu wenye ushawishi mkubwa sana nchini. Kwa kutekeleza jukumu lake la kutetea maslahi ya wapigakura na kutetea watu wachache wenye ushawishi, wabunge walifeli katika majukumu yao ya kikatiba na hawafai kamwe kuwa bungeni.
Njia ya pekee ni Wakenya kuungana na kutumia nguvu zao za kikatiba ili bunge livunjwe.
Kwa maoni yangu, Wabunge ndio kikwazo kikubwa katika vita dhidi ya ufisadi na kwa kuwa chama tawala cha Jubilee ndicho kilicho na wabunge wengi, wakenya wanafaa kuwa na wasiwasi kuhusu aina ya sheria ambazo bunge hili limekuwa likipitisha au litapitisha.
Hali imekuwa mbaya zaidi baada ya Wabunge wa vyama vikuu vya upinzani kuamua kuungana na serikali ambapo kiongozi wa wachache John Mbadi aliungana na kiongozi wa wengi Adan Duale kuongoza Wabunge kukataa ripoti hiyo.
Hii ndio hatari ya kuwepo kwa siasa za ubarakala. Ikumbukwe kuwa sio mara ya kwanza madai ya rushwa kuripotiwa bungeni na hasa katika kamati zinazochunguza sakata mbalimbali.
Kulikuwa na madai kwamba wakuu wa kampuni ya Kenya Power walikutana kisiri na wanachama wa kamati iliyokuwa ikichunguza sakata katika kampuni hiyo. Baadhi ya maafisa wakuu wa Kenya Power wameshtakiwa kwa ufisadi kufuatia juhudi za maafisa wa upelelezi wa jinai na Tume ya Maadili na Ufisadi (EACC).
Kwa maoni yangu wabunge wa sasa wameshindwa kudumisha hadhi na heshima ya bunge, hawana maadili yanayostahili kwa mtu kuitwa mbunge, wamepaka matope asasi tukufu ya serikali, wamesaliti kiapo chao kwa kutokuwa waaminifu kwa Jamhuri ya Kenya na kwa Rais aliyejitolea kuangamiza ufisadi wanaoendeleza ndani na nje ya bunge na hawafai kuruhusiwa kuendelea kuhudumu.
Kuna haja ya bunge hili kuvunjwa kwa sababu kuna dalili kwamba wabunge wataendelea kutumia mamlaka yao vibaya na kinga wanayofurahia kwa kisasi dhidi ya wanaowakosoa.
Walidhihirisha haya walipopunguza bajeti ya Mahakama wakidai majaji wamekuwa wakitoa maagizo wasiyofurahia.
Wakati umefika kwa Wakenya kusahau tofauti zao za kikabila, kusahau tofauti zao za kisiasa na kuwafuta kazi Wabunge wote na kuwachagua wengine wapya wanaojali maslahi yao.