Makala

MATHEKA: Mbinu mpya kudhibiti silaha haramu zinafaa

March 11th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na BENSON MATHEKA

Hatua ya waziri wa usalama wa ndani Fred Matiang’i ya kuagiza wanaomiliki silaha wakaguliwe upya na kupatiwa leseni za kidijitali inafaa.

Ni hatua ambayo inafaa kutiliwa mkazo na bodi ya kutoa leseni za kumiliki silaha. Bodi inafaa kuitekeleza kwa umakini bila upendeleo wowote.

Nasema hivi kwa sababu tumeshuhudia watu wakitumia vibaya silaha wanazomiliki kisheria jambo linaloibua maswali kuhusu ufaafu wao wa kumiliki silaha. Ninachozungumzia hapa ni kwamba kuna tofauti ya kuwa na leseni ya kumiliki silaha na ufaafu wa mtu kumiliki silaha.

Kuna watu ambao licha ya kuwa na leseni halali za kumiliki silaha, wamekuwa wakizitumia kuua watu wasio na hatia. Mfano mzuri ni mgonjwa aliyeingia katika hospitali moja jijini Nairobi na kuua tabibu.

Baadhi ya wanaopatiwa silaha huwa na matatizo ya akili. Hii ilifanya mfumo uliokuwa ukitumiwa kutathmini waliopaswa kupatiwa leseni kutiliwa shaka. Ikizingatiwa kwamba baadhi ya watu waliokuwa na leseni za kumiliki silaha walikuwa wakikodisha bastola zao kwa wahalifu, ilifaa kuwe na masharti makali ya kumiliki silaha na ndivyo anavyofanya Dkt Matiang’i.

Hata hivyo, ni jukumu la bodi kuhakikisha kuwa masharti hayo yemezingatiwa kikamilifu ikiwa matumizi mabaya ya silaha yatapungua nchini.

Visa vya watu kuwa na leseni bandia za kumiliki silaha vitakuwa historia kwa sababu ya mfumo mpya wa kielektroniki ambao Bw Matiang’i aliagiza utumiwe. Bodi inafaa kubaini kuwa haitaepuka lawama kwa kudai kwamba mtu akitumia silaha yake vibaya atakuwa na leseni bandia kwa sababu inatakiwa kutoa nambari maalumu kwa kila anayepata leseni.

Haitaweza kuepuka lawama kwa kutoa leseni kwa watu walio na matatizo ya kiakili kwa sababu inapaswa kuhakikisha kila anayemiliki silaha kihalali anafaa kuwa na akili timamu.

Baada ya Bw Matiang’i kulainisha utoaji wa leseni za kumiliki silaha, anafaa kuelekeza juhudi zake kwa wanaomiliki silaha haramu zinazotumiwa na majangili kuiba mifugo. Hili limekuwa tatizo la miaka mingi nchini.

Wakazi wa maeneo yanayokabiliwa na wizi wa mifugo wamekuwa wakihangishwa na majangili wanaomiliki silaha hatari na serikali inapaswa kutafuta njia za kuwapokonya bunduki hizo.

Ninaamini kwamba japo awali imekuwa ni mlima kuwapokonya majangili hawa silaha, kukiwa na mikakati thabiti na nia njema, shughuli hii inaweza kufaulu.

Silaha haramu ni tisho kwa usalama wa taifa na kila hatua zinafaa kuchukuliwa kuhakikisha haziingizwi nchini. Sio siri kwamba silaha hizi huwa zinaingizwa nchini kutoka mataifa jirani yanayokumbwa na misukosuko na kwa sababu hilo linajulikana usalama unafaa kuimarishwa mipakani.

Najua sio Kenya pekee inayokabiliwa na tatizo la silaha haramu, ni tatizo la ulimwengu mzima. Hata hivyo, kujitolea kwa serikali kukabiliana na suala hili kunaweza kuzuia hasara inayosababishwa na silaha haramu. Hii ni kuanzia kwa utendakazi wa bodi ya kutoa leseni za kumiliki silaha na maafisa wa usalama kwa makini katika kazi yao mipakani.