Matumaini wizara ya afya ikiingilia kusaidia walioathiria na mafuta
MWANGA wa matumaini umewaangazia wahasiriwa wa janga la mafuta yaliyomwagika kwenye Mto Thange, Kaunti ya Makueni, baada ya Wizara ya Afya kuingilia kati rasmi kwa mara ya kwanza tangu tukio hilo lilipofanyika 2015.
Wizara ya Afya ambayo awali haikuhusishwa wakati janga hilo la kimazingira lilipofanyika zaidi ya mwongo mmoja uliopita, iliingilia kati kutoa msaada wa afya na vipimo kwa umma ikijibu ombi la Gavana Mutula Kilonzo.
Kamati ya Seneti kuhusu Nishati inayoongozwa na Seneta Oburu Oginga ilielezwa kwamba familia zisizopungua 10,000 Wadi ya Thange ziliathiriwa zinapambana na matatizo sugu ya kiafya ikiwemo maradhi ya ngozi na kupumua kutokana na visima vya maji viliyobaki na kemikali ya sumu ambavyo sasa vimefungwa.
Waziri wa Afya Aden Duale alihakikishia Seneti kwamba Kampuni ya Mafuta Nchini (KPC) itashurutishwa kisheria kuwajibia athari zilizotokana na mkasa huo akisema wamechelewesha sana kufanya hivyo.
Waziri wa Afya alifika mbele ya Kamati ya Seneti kupokea mawasilisho kuhusu athari kwa afya na umma zilizotokana na tukio la mafuta ya KPC yaliyomwagika Mto Thange na kuhatarisha maisha ya wakazi 10,000.
Kulingana na Waziri, udadisi ulifichua baaadhi ya visima vya maji umbali wa kilomita 40 kwenye nyanda za chini vinasheheni chembechembe za mafuta ikiwemo ripoti kuhusu mazao ya kilimo kudorora, matatizo ya uzazi kwa mifugo na watoto kuzaliwa wakiwa na matatizo yasiyo ya kawaida.
Aidha, alisema katika kikao cha baraza kilichohudhuriwa na wanajamii na uongozi, walielezea wasiwasi kuhusu ongezeko la maradhi ya saratan na figo, gharama ya matibabu na mazingira kuzidi kuzorota.
“Wizara ya afya imependekeza wanajamii kusambaziwa maji yaliyo salama kupitia kuchimba visima katika maeneo ambayo hayajaadhiriwa, kutoa msaada kisaikolojia, ushauri nasaha na vipimo vya matibabu kila mwaka kwa wanajamii,” alisema Bw Duale.
Seneta wa Makueni, Daniel Maanzo alisema Mahakama Kuu iliagiza KPC kuwalipa fidia wakazi wa Thange, akihoji ina uwezo wa kufanya hivyo maadamu inaandikisha faida ya Sh12 bilioni kila mwaka.
“KPC inapaswa kushurutishwa kuwalipa fidia wakazi wa Thange ambao wameteseka sana kwa zaidi ya miaka 10 iliyopita. Inasikitisha kwamba asasi hii ya serikali haijatilia maanani swala hili ipasavyo,” alisema Seneta Maanzo.
Seneta Oburu alisema wakazi wa Thange wamehangaika miaka mingi kutokana na madhara ya mafuta yaliyomwagika bila suluhisho lolote thabiti akisema udadisi unaonyesha maji na udongo eneo hilo unasheheni kemikali sumu.
Familia zaidi ya 242 katika Wadi ya Thange zinapambana na vifo na maradhi yasiyoeleweka yanayohusishwa na janga la mazingira huku Seneti ikitoa wito kwa wadau husika kuhakikisha suala hilo linatatuliwa kikamilifu.
“Seneti inahimiza KPC, Mamlaka inayosimamia Mazingira (NEMA) na serikali ya kaunti ya Makueni kushirikiana ili tusuluhishe kero hili ambalo limekithiri kwa miaka mingi na kuwaacha wakazi wakiteseka,” alisema Bw Oburu.