MATUNDURA: Buriani ndugu Hugholin Kimaro, Mola akulaze pema penye wema
NA BITUGI MATUNDURA
MNAMO mwezi Novemba 2018, rafiki na mwanahabari Anthony Nyongesa wa Halmashauri ya Uchukuzi na Usalama (NTSA) alinipigia simu kunitaarifu kwamba Mwalimu Hugholin Kimaro alihitaji matibabu ya dharura. Matibabu hayo yalilenga kumuondolea bughudha ya uvimbe kwenye ubongo uliokuwa unamsumbua.
Kadhalika, Bw Nyongesa aliniomba idhini ya kusimamia kundi la WhatsApp la Kimaro Medical Support ili kuchangisha pesa za kumsaidia rafiki yetu, ili apate matibabu dharura kunusuru maisha yake.
Ukumbi huo ulikuwa na marafiki wengi waliowahi kutagusana na Mwalimu Hugholin Kimaro katika vitovu vitatu ambapo maisha yake yalizunguka – ualimu, uanahabari na uandishi wa vitabu.
Siwezi kuwataja marafiki wote hao – ambao walichangamkia sana wito wa Bw Nyongesa wa kuchangisha pesa za kumsaidia Bw Kimaro – kwa sababu ni wengi mno, na wanajijua wenyewe.
Baada ya kufanyiwa upasuaji kwenye kichwa katika Coptic Hospital, Mwalimu Kimaro alilazwa katika Chumba cha Wagonjwa walio katika hali Mahututi (ICU) kwa muda.
Hali yake ilipoonekana kuimarika baada ya majuma machache, alihamishwa hadi Kitengo cha High Dependency Unit (HDU).
Mnamo Januari 4, 2019 – saa moja usiku, nilimpigia Bw Nyongesa simu kutaka kujua hali ya Mwalimu Kimaro hospitalini. Bw Nyongesa, ninayemfahamu kuwa mwepesi wa kuzungumza, alibaki akimung’unyamung’unya maneno.
Jibu lake liliniongezea majonzi zaidi kwa sababu siku hiyo ndiyo niliyomzika shangazi yangu – Mama Maria Moraa Onsakia. Siku chache kabla ya Mwalimu Kimaro kulazwa hospitalini, nilimpigia simu. Ingawa alikuwa anahisi maumivu mno, alijikaza na kuzungumza nami.
Tulitaniana kuhusu ahadi ya ‘mahojiano’ tuliyopanga kufanya miaka mingi sasa imepita. Kwenye mahojiano hayo, Mwalimu Kimaro alitaka ‘kunihoji’ kuhusu machango wangu (iwapo upo) katika maendeleo ya Kiswahili. Aliazimia sana kuchapisha makala kunihusu magazetini.
Hilo halikuwahi kutimia, na halitawahi kamwe. Nilianza kusoma makala ya Mwalimu Kimaro magazetini nilipokuwa mwanafunzi wa shahada ya kwanza katika Chuo Kikuu cha Moi – miaka ya 1990.
Tulikutana naye ana kwa ana mnamo 2007 tuliposhiriki katika Mradi wa Tafsiri wa Microsoft Language Localization (MLL), na baadaye Nation Media Group ambapo nilifanya kazi ya uripota katika gazeti la Taifa Leo.
Mwalimu Kimaro alikuwa mtu mnyenyekevu, mkarimu na muungwana ambaye alitangamana vizuri na watu wengine. Alikuwa pia mwalimu na mwandishi mzuri aliyeshirikiana na wanataaluma wengine katika uandishi wa vitabu.
‘Maalim’ – jinsi tulivyozoea kuitana alikuwa mcheshi vilevile. Baadhi ya vitabu vyake vilivyoselelea ni pamoja na msururu wa Hazina ya Kiswahili (Longman) – alioandika kwa ushirikiano na walimu wengine kama kina Kahura Ndung’u, Njoroge Gichoni na Ruo Kimani Ruo.
Alichangia sana tahakiki za vitabu katika magazeti ya Saturday Nation, Sunday Nation pamoja na ukumbi wa Lugha na Fasihi katika gazeti la Taifa Leo. Ulimwengu wa Kiswahili umempoteza mmoja wa wanajeshi waliokipenda na kukistahi Kiswahili. Kwaheri ya kuonana Mwalimu Kimaro.
Marehemu Mwalimu Kimaro atazikwa kwao Rombo, Tanzania mnamo Januari 18, 2019.
Bitugi Matundura ni mhadhiri wa Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Chuka. [email protected]