Makala

Maulidi, jabali wa mipigo ya ngoma za taarabu aliyetelekezwa na jamii!

August 9th, 2019 Kusoma ni dakika: 4

Na HASSAN MUCHAI

Wakati wa ujana wake, Maulidi Juma alijawa na siha, mwenye sauti nzito, mwepesi jukwaani na aliyejaa fahamu ya matukio ya nyuma.

Alikuwa na nguvu na pumzi za kutosha kumwezesha kuimba kwa saa nne mfululizo! Gwiji huyu wa muziki wa taarabu alikuwa mwenye tabasamu huku akikariri maneno matamu ya kuongoa ambayo yalimfanya kivutio kikuu cha wale wanaosisimka kutokana na mipigo ya ngoma za taarabu.

Nyimbo zake za mahaba, makanyo na siasa zilitawala vyombo vya habari, hasa kile kipindi cha taarab kilichosimamiwa na mtangazaji Khadijah Ali wa Voice of Kenya (sasa KBC).

Alikuwa pia mweledi wa kutunga nyimbo na angefanya hivyo moja kwa moja bila kuchelea.

Na mwanaume huyo jamala sasa ni mnyonge ajabu. Mishipa ya mwili imedhoofika na nyama kukauka. Uso umechanika na ngozi kuparara. Uzee umemsonga na maradhi kumkeketa. Bingwa huyo wa muziki sasa ametamauka maishani.

Tulipomtembelea nyumbani kwake hivi majuzi, alitulaki kwa maneno ambayo yamejikita akilini kwa wiki moja iliyopita:

“Jamani tuague maradhi, uzee hauna dawa. Muathiriwa na waja, husitiriwa na Mungu’’

Mzee huyu hutumia muda mwingi katika makazi yake eneo la Snake Valley mtaani Soko Mjinga, Kisauni eneo bunge la Kisauni. Aghalabu, kutembea hata mita chache ni shida.

Anaongea kwa matao na wakati mwingine pumzi kumwishia. Hana uwezo kuona mbali. Hawezi kujibu maswali na anahitaji mwanawe Abdulrahman kuwa mfasiri wake. Hata tulipoomuuliza majina ya wanakikundi wenzake kwenye Maulidi & Party, hangeweza kumtaja hata mmoja.

Licha ya haya yote, tabasamu lake alilokuwa akibwaga jukwaani wakati wa ujana wake lingalipo.

Mara kwa mara mara atavuta fikra anapoulizwa swali. Akishindwa kujibu, atatabasamu mdomo wazi na kuchora taswira ya mwimbaji jukwaani.

Ingawa kuna ishara zote kwamba Maulidi anaishi maisha ya uchochole, bado anajipa moyo kwa kufaharia sifa na matuzo aliyopata kutokana na usogora wake wa kutunga na kuimba nyimbo za taarabu.

Licha ya mapungufu haya yote, Maulidi bado azikumbuka nyingi ya nyimbo alizoimba. Japo kwa tabu atakariri ubeti mmoja, wa pili hata akamilishe!

Enzi zake, mji wa Mombasa na maeneo ya karibu kama vile Likoni, Diani, Msambweni, Mtwapa, Kilifi, Malindi, Voi hata Majengo ya Nairobi yalimtambua Maulidi. Bendi yake ya Maulidi and Party ilitamba kwenye sherehe za harusi.

Alipopanda jukwaani na kufumua mikwaju yenye mahadhi ya kihindi, mashabaki wake waliduwaa. Mdundo wa nyimbo zake, maneno yenye ushawishi kimahaba na sauti nyororo iliiwaacha wengi na hamu ya kudai zaidi kutoka kwake.

Maulidi aliwahi kutunga na kuwatumbuiza marais Kenyatta, Nyerere, Moi, Kibaki na viongozi wengine mashuhuri miaka ya awali. Wengi bado wazikumbuka nyimbo zake za kusifu KANU na uongozi wa Rais Moi miaka ya ‘80 na ’90.

Kutokana na ustadi na umaarufu wake kuvutia halaiki ya watu, wanasiasa hasa marehemu Sharriff Nassir walipenda sana kuandamana naye katika mikutano ya hadhara na wakati mwingine kumtumbuiza Rais mstaafu Moi Ikulu ya Mombasa, Nairobi, Nakuru au hata nyumbani kwake Kabarak.

Wakati Kanu ilikumbatia mfumo wenye utata wa kupiga kura maarufu kama “mlolongo,” Maulidi aliimba wimbo wenye utata uliotetea mfumo huo.

“Kwa nini kupinga ukweli, na kura za mlolongo ndio kura za halali?’’ Isitoshe, wimbo wake “Moi kiongozi wetu, unayezifuata amri za Mungu na kuzihubiri hadharani, ni wewe hatutaki mwingine Kenya’’ ulimsawiri kama mfuasi sugu wa Kanu.

Maulidi Juma alizaliwa 1941 kijijini Mida kaunti ya Kilifi. Lakini hakubahatika kujiunga na shule au chuo chochote. Badala yake alijihusisha na shughuli ndogo ndogo nyumbani kwao.

Talanta yake ya uimbaji wa nyimbo za taarab ilianza kuchomoza akiwa mdogo kwani mazingira aliyokulia yalikuwa yamezungukwa na utamaduni wa uswahili. Nyimbo alizokuwa akiimba zilikuwa na mahadhi kamili ya taarabu.

Akiwa Mida, Maulidi aliyaandama makundi ya waimbaji wa ngoma za kiasili za Kigiriama. Alikuwa akizunguka mitaa ya Kibaoni, Gede, Takaungu na maeneo mengine ya karibu alikojifunza kuimba na kupiga ngoma za kiasili.

Akiwa Mida alianzisha kikundi cha Young Sport Band 1956. Alikuwa akiimba bila kutumia kipaza sauti hali iliyonawirisha sauti yake. Aidha, vyombo walivyotumia havikuwa vya kisasa.

Maulidi aliingia mjini Mombasa 1971 na kupiga kambi mtaa wa Kisauni ambako anaishi hadi sasa. Akiwa Mombasa alikutana na mwimbaji mkongwe wa taarab, marehemu Mohammed Khamis Juma Bhalloh.

Pia, kulikuwa na vikundi vingine mashuhuri vya waimbaji kama vile Johari Orchestra na Morning Star. Aliamua kujiunga na kikundi cha Zein Musical Party kama mwimbaji na mcharaza kibodi.

Baada ya kujihisi kukomaa kisanaa, mnamo 1972, Mzee aliunda kundi la Maulidi & Party ambalo liliwahusisha Maulidi Juma (mwimbaji na mtunzi), Mohammed Mbwana (kibodi), Rajabu Pilau ( mtunzi na mcharaza bongo), marehemu Ali Mwadhamu (tabla), marehemu Bhadi Mfaume ( Tabla na Accordion), marehemu Bakari Aziz (Bongo), Juma Bakari (gita) na Shembwana Anas (msimamizi wa sasa wa kundi).

Kubuniwa kwa kundi la Maulidi & Party kulizua ushindani mkali wa malumbano ambao haujawahi kushuhudiwa Mombasa kati ya Mohammed Khamis Juma Bhalo na pia Zuhura Swaleh.

Ushindani huu ulileta msisimko mkubwa Pwani nzima ya Kenya. Maulidi & Party iliendelea kufumua kuvuma kwa vibao kama vile “Vishindo vya mashua, zapita siku zapita, nayaogopa mapenzi, waja mtachoka, yasokuwa hayanenwi’’ na kadhalika. Mtunzi wa kundi alikuwa Rajab Pilau.

Ili kufanikisha zaidi kikundi chake, Maulidi aliwaalika waimbaji wa kike Asha Abdow (maarufu Malika), marehemu Stara Bhute na Malikia Rukia na kufumua vibao vilivyovuma enzi hizo. Kutokana na sifa zao, kundi lilialikwa kutumbuiza Ujerumani, Ufaransa, Uholanzi na Uswizi.

Kati ya 1998 na 2000, kundi la Maulidi & Party lilianza kuyumba yumba kutokana na mizozo ya ndani kwa ndani na kustaafu kwa baadhi ya wanachama wake mathalan Rajab Pilau ambaye alikuwa nguzo ya kundi.

Hata hivyo, mabadiliko ya kiteknolojia, hisia za vizazi vipya, msingi hafifu na ukosefu wa mwelekeo wa maono ya siku za usoni ni sehemu tu ya chanzo cha kufifia kwa kundi. Kikundi hicho, kwa mfano, hakikurekodi hata video moja.

Umasikini pia ulichangia pakubwa. Uliwadia wakati mzee hangeweza kusafiri mbali kwenda kucheza kutokana na ukosefu wa pesa. Maisha yalianza kuwa magumu na wengi wetu wakaamua kuachana na uimbaji. Tulikuwa tukipokea Sh300 kucheza usiku kuccha. Pili, wanasiasa walikuwa radhi kututumia na siasa zinapoisha wanatutenga’’ alisema Rajabu Pilau ‘Taifa Leo’ ilipomtembelea nyumbani wake Takaungu.

Kwa mujibu wa Juma Salim Makayamba, mwandani wa Maulidi, chanzo halisi cha kuvunjika kwa kundi hilo ni ukosefu wa mwelekeo na mikataba duni kuhusu haki miliki. Asema Maulidi & Party ilifumua zaidi ya albamu 45 na cha kushangaza ni kwamba, kundi halina mkataba wa umiliki wa hata santuri moja!

“Jamani tumzike Mzee akiwa hai. Kuna haja mtu akifa kumlimbikizia sifa na wakati alikuwa hai tulimpuuza. Tunaomba Maulidi ashughulikiwe sasa akiwa hai. Ana maradhi na anahitaji msaada kupata matibabu’’ asema Makayamba.

Aidha, huenda Maulidi Juma akawa mwakilishi wa kizazi cha mwisho cha waimbaji wa nyimbo asilia za taarab ambazo mipigo yake inafanana sana na nyimbo za mahadhi ya kihindi au kiarabu. Endapo hili litafanyika, taifa litapata hasara kubwa na Maulidi atabaki tu kuwa kumbukumbu kwenye jedwali la waliovuma’.