MAWAIDHA YA KIISLAMU: Athari za dhambi ya usengenyaji katika jamiii na jinsi ya kuiepuka
SIFA zote njema anastahiki Mungu Subuhaanahu Wata’ala, Mwenye kuneemesha neema kubwa kubwa na nyingine ndogo.
Swala na salamu zimwendee Mtume wetu Muhamad Swallallahu Alayhi Wasallam, Maswahaba wake watukufu na watangu wema hadi siku ya Kiyaamah.
Baadhi ya madhambi wapenzi wasomaji yana athari kubwa sana katika maisha ya kijamii na ya mtu binafsi na katika kumporomosha mtu kiroho na katika kufikia ukamilifu wa kiutu, kama ambavyo baadhi ya amali njema zina taathira kubwa mno pia katika kumjenga na kumuinua mtu kiroho na kimaanawi.
Kusengenya, ni moja ya madhambi ambayo huwa ni utangulizi wa kufanywa madhambi mengine na kuenea maovu katika jamii.
Na hilo huthibiti kwa sura hii, kwamba wakati mtu anapotangaza aibu na mabaya ya watu husababisha kuenea maovu na kuyafanya maovu hayo yazoeleke na kutohisika tena kuwa ni kitu kibaya katika jamii.
Katika Uislamu kulinda na kuhifadhi roho, mali, heshima za watu na fikra zao ni jambo la lazima.
Imekuja katika hadithi iliyopokewa kutoka kwa Imam Ja’afar Swadiq AS kwamba: Heshima ya Muumini ni zaidi ya heshima ya al-Kaaba. Hii ni kutokana na kuwa, heshima ya mtu ni matokeo ya umri wa maisha, hima, idili na juhudi za mtu, hivyo hailaiki na haifai heshima hiyo ambayo mtu kajikusanyia kwa miaka mingi aje mtu na kuiharibu kwa lahadha moja kutokana tu na ujahili wa mtu au malengo maalumu aliyo nayo.
Masengenyo hucheza shere hadhi na heshima
Kusengenya ni miongoni mwa madhambi ambayo hucheza shere hadhi na heshima za watu.
Imenukuliwa kutoka kwa Mtume SAW amesema ya kwamba: Katika usiku wa Miraji nilipita katika kaumu moja na kuwaona watu wa eneo hilo wakijikwangua kwa kucha zao. Nikamuuliza Malaika Jibrili: Hawa ni watu gani na kwa nini wanajikwangua namna hii?
Jibril akasema: Hawa ni watu ambao kazi yao ilikuwa ni kusengenya watu wengine na kuharibu heshima za watu kwa kuwasema kwa ubaya.
Kwa hakika wengi wetu kutokana na kughafilika au kutoshikamana kikamilifu na mafundisho ya Uislamu, tumetumbukia na kunasa katika dhambi ya kusengenya na kuwaramba visogo watu wengine.
Tunapaswa kutambua kwamba, kila ambaye anafanya juhudi za kufichua aibu za watu wengine zilizojificha, Mwenyezi Mungu atamuumbua na kumfedhehesha.
Mafundisho matukufu ya dini ya Kiislamu yanatoa miongozo yenye faida kubwa kwa ajili ya kuacha dhambi ya usengenyaji.
Miongoni mwa miongozo hiyo ni kwamba: Mtu aliyeamua kutafuta tiba ya ugonjwa wa kusengenya anatakiwa azingatie nukta hii kwamba, badala ya kuhesabu aibu na kasoro za watu wengine, jambo bora kwake yeye ni kufikiria zaidi aibu na kasoro zake mwenyewe.
Bwana Mtume Muhammad Alayhi Salaam amesema: “Hongera kwa mtu anayeshughulishwa na aibu zake badala ya aibu za watu”.
Aidha Imam Sajjad (AS) amesema: “Mtu anayeuzuia ulimi wake usiwafedheheshe na kuwaharibia watu heshima zao, Mwenyezi Mungu atayafumbia macho madhambi yake Siku ya Kiyama”.
Njia nyingine inayomsaidia mtu kuacha dhambi ya kusengenya, ni kuwa na hadhari zaidi katika kuchagua marafiki na watu wa kusuhubiana nao na wa kuchanganyika nao.
Hii ikiwa na maana kwamba, achague kufanya urafiki na usuhuba na watu wasio na tabia ya kusengenya, na asikae kwenye vikao na mkusanyiko wa watu wenye tabia hiyo, kwa sababu kukaa kwenye vikao vya usengenyaji huathiri roho na moyo wa mtu atake asitake, na kwa kuzingatia kwamba kusikiliza usengenyaji pia ni haramu, inapasa mtu awe makini zaidi katika suala la kuchagua rafiki na hata katika kutembeleana kifamilia.
Katika hadithi iliyopokewa kutoka kwa Bwana Mtume Muhammad Swallahu Alayhi Wasallam imeusiwa kwamba, waumini wanatakiwa wakatae kuchanganyika na kukaa na watu wasengenyaji mpaka watu hao waache tabia yao hiyo.
Kwa sababu kujiondoa kwenye kikao au mkusanyiko wowote kwa msingi wa kukataa kujumuika na watu wasengenyaji kunaweza kuwa kinga nzuri sana na yenye taathira kubwa ya kujizuia na dhambi ya usengenyaji, na ni aina mojawapo ya mapambano hasi ya kukabili mambo yanayochochea dhambi hiyo nzito.
Kumkataza
Njia nyingine ya kukabiliana na usengenyaji ni kukumbusha na kutanabahisha kwa kutumia ulimi; yaani mara tu mtu anaposikia mtu fulani amesengenywa, achukue hatua papo hapo ya kumkataza msengenyaji kwa kumueleza bayana kuwa ‘usisengenye’!
Njia nyingine ambayo ni ya upole ya kumfanya mtu aache kusengenya, na ambayo inategemea uwezo na werevu wa msikiaji ni kwamba, kama mtu hawezi kuondoka katika hadhara hiyo au kumweleza kinagaubaga msengenyaji kwamba aache kusengenya, basi anaweza angalau kwa uchache kutumia ujanja wa kubadilisha maudhui ya mazungumzo ili kuondoa anga ya hali ya usengenyaji.
Njia nyengine ni mtu kujaribu kujizuia kabisa na mazingira ya kusengenya; yaani ikiwa kuna mtu anataka kuzungumziwa habari zake, mtu anayetaka kuanzisha gumzo kuhusu mtu huyo atafakari kwanza kama uzungumziaji huo utaishia kwenye usengenyaji au la.
Ikiwa atahisi kuna uwezekano wa kufanya usengenyaji basi aache kabisa kuanzisha mjadala huo, na kwa njia hiyo ataweza kuondoa kikamilifu viashiria vya kufanyika usengenyaji.
Kuomba auni na msaada kwa Mwenyezi Mungu kwa njia ya dua na munajati pia kunamsaidia mtu kuacha madhambi ikiwemo ya kusengenya.
Kila wakati tuwe tunamwomba msaada Mwenyezi Mungu atuwafikishe kuepukana na maradhi angamizi ya kiakhlaqi yakiwemo ya kusengenya.