MAWAIDHA YA KIISLAMU: Baadhi ya njia anazoweza kufanya Muumin ili kuipa nguvu imani yake
Na HAWA ALI
KILA sifa njema zinamstahikia Allah Mola wa viumbe vyote.
Sala na salamu zimuendee Mtume wetu Muhammad (swalla Allahu alaihi wa sallam) na ahli zake na maswahaba wake.
Imani ya mja huwa inapanda na kushuka. Na hii ni miongoni mwa tabia za Muislamu. Kuna wakati muislamu imani yake humjaa na huwa anajitahidi katika Ibada. Sala tano hazimpiti tena kwa jamaa.
Funga za sunna huwa ndio vazi lake. Adhkaar na sala za usiku ndio mapambo yake. Lakini baada ya muda haya mambo yote huwa hayafanyi tena. Na huanza uvivu wa kutekeleza mambo hayo.
Wengine wao huwa na imani kubwa sana na hamu ya kutenda matendo mema na nia hasa pale wanapokumbushwa. Ila baada ya muda hamu ile ya kufanya ibada inapotea. Lakini hawa wote tujiulize ni kipi kinachowafanya wawe hivyo? Tatizo lao ni udhaifu wa imani au kushuka kwa imani. Imani inapokuwa juu basi ndipo kheri zote huzikimbilia au ndipo hamu ya kufanya ibada humjaa mtu. Lakini imani inaposhuka basi huyu mtu huwa hana tena hamu ya mambo hayo na huwa na uvivu.
Sasa nini afanye ili aipe nguvu imani yake? Leo katika makala hii tutajaribu kuelezea baadhi ya njia ambazo muislamu anaweza kuzifanya ili aweze kuipa nguvu imani yake. Njia zenyewe ni kama zifuatazo :
Kuomba dua kwa Allah akujalie imani thabiti
Hakika kila jambo ikiwa unamuomba Allah (subhanahu wataala) basi Allah atakupatia jambo hilo. Hivyo basi jambo muhimu muombe dua Allah (subhanahu wataala).
Kusoma Quran kwa mazingatio
Endapo muislamu anahisi imani yake imeshuka au inatetereka basi akimbilie kusoma sana Qur’an. Ila aisome Qur’an kwa mazingatio kwa kujua ni kipi ambacho Allah (subhanahu wataala) anakielezea ndani ya Qur’an. Na ikiwa mtu hajui tafsiri ya Qur’an basi asome kwa kutumia msahafu wa tafsiri.
Hakuna yeyote ambaye amesoma Qur’an kwa mazingatio isipokuwa umelainika moyo wake. Na hapo ndipo sifa ya muumini inapopatikana. Na endapo ukaona kuwa unasoma Qur’an na moyo wako hauathiriki na chochote basi jua wewe ni maiti inayotembea duniani.
Allah (subhanahu wataala) anasema “Hakika Waumini ni wale ambao anapo tajwa Mwenyezi Mungu nyoyo zao hujaa khofu, na wanapo somewa Aya zake huwazidisha Imani, na wakamtegemea Mola wao Mlezi.” (8:2). Aya hii inaonyesha wazi kuwa yeyote yule anaesoma Qur’an kwa ufahamu na mazingatio basi kwa hakika imani yake itapanda. Pia Allah (subhanahu wataala) anasema ndani ya Suratu Muhammad aya ya 24 “Je! Hawaizingatii hii Qur’an? Au kwenye nyoyo (zao) zipo kufuli?”
Tujitahidini tulainishe nyoyo zetu ili Qur’an iwe ni ukumbusho kwetu.
Vipi watu wema walikuwa wakiathirika kwa kusoma Qur’an kwa mazingatio?
Tuangalie mifano ifuatayo halafu tujiulize na sisi nafsi zetu zipo sehemu gani?
Siku moja Sayyidina Omar (radhiya Allahu anhu) alikuwa akiisoma aya katika aya za Qur’an. Alipozisoma akaanza kulia na kulia. Mpaka akawa anashindwa kutoka nje ya nyumba yake kwa sababu ya kilio alichokuwa nacho. Je alilia tu bure bure? Hapana alilia kwa sababu aliyafahamu maneno ya Allah kwa upeo wa juu na akawa anajiuliza vipi yeye hali yake itakuwa. Aya yenyewe aliyoisoma ni “Hakika adhabu ya Mola wako Mlezi hapana shaka itatokea.(7) Hapana wa kuizuia.(8). Machozi yake yalishindwa kujizuia akikaa akijiuliza vipi adhabu za Allah (subhanahu wataala) zitakuwa.
Vipi mimi na wewe tunapozisoma aya kama hizi? Je nyoyo zetu hazipaswi kunyenyekea na kuwa na mazingatio?
Tumuangalie naye Omar Ibn Abdul Aziz. Siku moja Omar Ibn Abdul Aziz alisikilikana analia kwa sauti na kushindwa kujizuia. Jirani yake akaenda kumuuliza “Je ni kipi kimekusibu hadi unalia?”Omar Ibn Abdul Aziz akamwambia ”Hakuna kinachoniliza isipokuwa aya hii ndani ya Quraan, Allah(subhanahu wataala)anasema “…Na uhadharishe na Siku ya Makutano, haina shaka hiyo. Kundi moja litakuwa Peponi, na kundi jengine Motoni”(42:7). Najiuliza ndani ya nafsi yangu je nitakuwa katika kundi lipi kati ya haya mawili?
Hebu tuangalie vipi wenzetu wamekuwa wakiathirika na kusoma Quraan. Vipi mimi na wewe? Je hatuzipiti aya hizi? Je tunaisoma Quraan kwa mazingatio? Hawa ni wachache tu ambao wanaathirika kwa kusoma Quraan. Mifano ipo mingi ndugu zangu wakiislamu. Tujitahidini sana kuisoma Qur’an kwa mazingatio ili tuweze kuzikuza imani zetu.
Kukithirisha kukumbuka mauti
Mauti ni safari ya lazima kwa kila mwanadamu. Nayo ni safari ya kutoka katika dunia katika maisha ya mpito na kuelekea katika maisha ya akhera. Mwanadamu yanapomkuta mauti basi muda wa mtihani wake ndio unakuwa umekwisha na kinachobaki ni kwenda kukutana na hesabu. Je ulishwahi kujiuliza ni vipi roho yako itatolewa? Itatolewa kwa ajili ya kwenda jannah au motoni? Je ulishawahi kujiuliza vipi itakuwa hali yako pale utakapokuwa umebebwa kwenye jeneza?
Je ulishawahi kukaa na kujiuliza vipi utaikuta hesabu yako? Je umeshawahi kujiuliza nini utamjibu Allah pale utakaposimamishwa mbele yake? Mauti ni mazingatio tosha kwa muislamu na kumkumbusha ili aweze kukaa katika njia ya Allah (subhanahu wataala).
Mtihani mkubwa zaidi ni watu kuyachukia mauti. Na wapokuwa wakikumbushwa kuhusu mauti huwa wanachukia na kuona Sheikh hakuwa na mawaidha ila ya kuwatisha. Kumbe wanasahau kukumbushwa mauti ni kumfanya mtu aizidishe imani yake na kujiandaa na siku ya kutoka roho.
Mtume (swalla Allahu alayhi wasallam) anasema katika hadithi “Kithirisheni katika kukumbuka chenye kukata ladha’ Mtume (swalla Allahu alayhi wasallam) ameyaita mauti kama ni kikata ladha. Ndiyo mauti ni yenye kukata ladha ya starehe za uongo za dunia. Mwanadamu anapokumbuka mauti basi awe anajiuliza masuala ya msingi ambayo atakutana nayo. Na endapo muislamu ataona kuwa hata akikukumbuka mauti moyo wake hauthiriki basi pi ana yeye ataingia katika kundi la wale maiti wanaotembea katika dunia hii.
Anasema Allah (subhanahu wataala) “Kila nafsi itaonja mauti. Na bila shaka mtapewa ujira wenu kamili Siku ya kiyama.”(3:185).
Tujiandaeni na mauti na tujitahidini katika kukithirisha kukumbuka mauti kila wakati hili litamsaidia muumini na kumuasi Allah (subhanahu wataala).
Kutembelea makaburi
Makaburi nayo yana siri nzito ndani yake. Tayari tumeshamuhifadhi ndugu yetu katika kuelekea katika maisha yake ya milele. Nini kinachojiri ndani ya mauti? Mwanadamu atakapokaa na kuliwaza kaburi, giza lake na juu yake kufukiwa na michanga. Vipi atakaa ndani ya shimo hilo? Je ulishawahi kujiuliza vipi itakuwa usiku wa kwanza ndani ya kaburi lako? Je, wakati watu watakuwa washamzika, ataweza kujibu maswali ya Munkar na Nakir? Je, kaburi lake litakuwa ni bustani katika bustani ya peponi au mashimo katika mashimo ya motoni?
ITAENDELEA…