MAWAIDHA YA KIISLAMU: Fadhila sufufu za Siku ya Ijumaa
Na HAWA ALI
SIFA zote njema anastahiki Mwenyezi Mungu, Muumba wa mbingu na ardhi na vilivyomo.
Swala na salamu zimwendee Mtume Muhammad Swallallahu ‘Alayhi Wasallam, Maswahaba wake kiram na watangu wema hadi siku ya Kiyaamah.
Mwenyezi Mungu anasema, “Enyi mlioamini! Kukiadhiniwa kwa ajili ya Sala ya siku ya Ijumaa, nendeni upesi kumtaja Mwenyezi Mungu na acheni biashara. Kufanya hivi ni bora kwenu. Ikiwa mnajua (hivi basi fanyeni). Na itakapokwisha Sala, tawanyikeni katika ardhi mtafute fadhila za Mwenyezi Mungu, na mkumbukeni Mwenyezi Mungu kwa wingi ili mpate kufaulu.” (62:9-10).
Chaguo
Ijumaa ni Siku ya Wiki ambayo Mwenyezi Mungu ameichagua maalum kwa ajili ya Waislamu. Hii ndiyo Siku ambayo Kiama kitasimama. Yasemekana kuwa sababu ya siku hii kuitwa ‘Aljumuah” ni kwamba ndiyo siku ambayo Adam aliumbwa (ju-me-‘a-maana yake, ‘kuunganishwa pamoja); yaani aliumbwa siku ya Ijumaa.
Abu Huraira kasimulia kuwa Mtume, swallallahu alayhi wa sallam, amesema, “Siku bora kuchomozewa na jua ni Ijumaa. Ndiyo Siku ambayo Adam aliingia Peponi, na ndiyo Siku aliyotolewa humo.” (Muslim)
Siku ya Ijumaa ina hadhi kubwa katika Uislamu. Kila Ijumaa, kuna muda ambao Mwenyezi Mungu anazijibu dua. Mwenyezi Mungu ameuweka muda huu katika wakati ambao haukutajwa. Hatujui ni wakati gani jambo hilo hutokea. Hii imeachwa hivyo ili watu wahamasike na kuhangaika kutafuta fadhila za Ijumaa Siku nzima.
Abu Hurairah kasimulia kuwa Mtume, swallallahu alayhi wa sallam, amesema, “hakuna saa katika siku ya Ijumaa ambayo Mja Muislamu wa Allah anayesimama katika Sala na kumuomba kitu ila Mwenyezi Mungu humpa kitu hicho.” (Bukhari na Muslim).
Uislamu umeweka matendo fulani ya kidini na kijamii kwa ajili ya Ijumaa. Hayo ni matendo mahususi kwa mnasaba wa Siku hii. Miongoni mwa matendo hayo ni kufanya josho (ghusl), usafi, kujitia manukato, na kupendeza.
Inapokuwa ni Siku ya Ijumaa, halafu mtu akaoga, akapaka nywele mafuta, akatia manukato mazuri zaidi, akavaa nguo nzuri zaidi, kisha akatoka kwenda kuswali, na akaepuka kuwapangua watu waliokaa pamoja Msikitini, kisha akamsikiliza Khatibu anayekhutubu, basi dhambi zake zitasamehewa baina ya Ijumaa hii na iliyopita, na siku tatu zaidi (yaani jumla ya siku kumi)” (Ibn Khuzaymah).
Mtu anayeyatafakari matendo hayo, ataona kuwa kila moja lina lengo lenye manufaa. Kwa kutumia maji kunawa na kutia udhu, Waislamu hujikinga na maradhi na maambukizi yanayoweza kutokea katika mikusanyiko. Manukato na muonekano mzuri huleta utangamano, ukaribu na urafiki. Haya ndiyo malengo mema ambayo kila jamii njema hutaka kuyafikia.
Mambo mengine
Mambo mengine ya kidini yanayohitajika kufanywa Siku ya Ijumaa ni pamoja na: kwenda Msikitini mapema, kuepuka kuwasumbua watu kwa kuwaruka-ruka au kuwabana-bana, au kuwasogeza-sogeza pale walipokaa, na kutowavurugia mazingatio wakati wanapojielekeza katika ibada. Mkusanyiko wa watu hupendezeshwa na unadhifu na usafi.
Uislamu umetahadharisha juu ya mambo hasi ili kulinda hadhi ya Msikiti. Na hayo humsaidia kudumisha unyenyekevu, tafakuri na taqwa. Wale wanaochelewa Msikitini lakini bado wakatafuta nafasi ya mbele waache tabia hiyo na badala yake wawahi Msikitini kama wanataka kupata fadhila za Ijumaa.
Matendo mengine yanayopendeza Siku ya Ijumaa ni pamoja na kusoma aya za Qur’an, kumswalia Mtume, swallallahu alayhi wa sallam, na kusikiliza khutuba.
Pia anaweza kusoma chochote anachoweza kutoka katika Qur’an kwani kila herufi inayosomwa hupata thawabu kumi. Mtume, swallallahu alayhi wa sallam, amesema, “Siku bora katika Siku zenu ni Ijumaa. Basi kithirisheni kunisalia ndani yake.” (Abu Dawud na An-Nasa’i)
Khatibu
Mtume, swallallahu alayhi wa sallam, alitutahadharisha juu ya wajibu wa kumsikiliza Khatibu anapokhutubu na kuepuka kuvuruga mazingatio wakati wa khutba:
“Ukimwambia mwenzio Siku ya Ijumaa, “Sikiliza!’ ilihali Khatibu anazungumza, basi umefanya kosa.” (Bukhari na Muslim). Kwa maneno mengine, utakuwa umepunguza fadhila zako za Sala ya Ijumaa.
Makala hii imetaja matendo mengi yanayohimizwa Siku ya Ijumaa, na mengi ambayo yanakatazwa. Baadhi ya hayo yamehukumiwa kisheria, na baadhi hayakuhukumiwa.
Lakini yote yakichanganywa pamoja, ni dhahiri kuwa Uislamu ni mfumo wa jamii unaokusanya utamaduni wa kimaadili. Ni mfumo unaofundisha ustaarabu katika mambo yote.