MAWAIDHA YA KIISLAMU: Husuda huletwa na kutotosheka na neema zake Mwenyezi Mungu
Na HAWA ALI
SIFA zote njema anastahiki Mwenyezi Mungu, swala na salamu zimwendee Mtume Muhammad (SAW), maswahaba wake watukufu na wa tangu wema hadi siku ya Kiyaamah.
Husuda ni miongoni mwa magonjwa makubwa ya moyo.
Mtu mwenye husuda ana donda la chuki moyoni mwake juu ya neema alizoneemeshwa mwingine na Allah (subhnahu wataala).
Kwa maana nyingine anachukia utaratibu wa Allah (Subhanahu Wataala) aliouweka katika kugawanya neema zake kwa waja wake.
Hasidi kutokana na chuki yake dhidi ya mja aliyeneemeshwa na Allah (subhanahu wataala), huwa tayari kwa hali na mali kumdhuru mja huyo asiye na hatia yoyote.
Ni kwa msingi huu Allah (subhanahu wataala) anatufundisha kujikinga kwake na shari za viumbe vyake, akiwemo hasidi kama tunavyosoma katika Suratul-Falaq: Sema: “Ninajikinga na Mola wa Ulimwengu wote. Na shari ya alivyoviumba. Na shari ya giza la usiku liingiapo na shari ya wale wanaopulizia mafundoni na shari ya hasidi anapohusudu”(113:1-5).
Husuda husababishwa na kutotosheka na kutoridhika na neema za Allah (subhanahu wataala). Hasidi anataka kila neema aliyotunukiwa mwingine awe nayo yeye au mwingine abakie bila neema hiyo.
Anataka awe juu ya mwingine na aonekane wa maana pekee katika jamii. Akihisi kuwa kuna yeyote aliyemzidi kwa cheo, utajiri, elimu, watoto,umaarufu, hupandwa na moto wa chuki moyoni mwake ambao humsukuma kufanya visa mbali mbali dhidi ya huyo anayemhisi kuwa amemzidi au yuko sawa naye.
Muislamu anatakiwa ajitakase na uovu huu wa husuda kwa kutosheka na kile alichonacho akijua kuwa kila neema aliyopewa mwanaadamu imekadiriwa na Allah (subhanahu wataala). Na hapana yeyote mwenye uwezo wa kupunguza neema ya mtu aliyokadiriwa na Mola wake hata kwa kiasi cha chembe ndogo iliyoje na hakuna yeyote awezaye kumuongezea mtu neema kuliko vile alivyokadiriwa na Allah.
Pia Muislamu wa kweli anajitahidi kujiepusha na husuda ili asije akaziunguza amali zake njema alizozitanguliza na akawa miongoni mwa watakaokhasirika katika maisha ya akhera.Abu Hurairah (radhi za Allah ziwe juu yake) amesimulia kuwa Mtume(swalla Allahu alayhi wasallam) amesema: “Kuweni waangalifu juu ya husuda, kwani husuda inaunguza amali njema za mtu kama moto unavyounguza kuni. (Abu Daud)
Kushindana katika kufanya mema
Husuda au wivu unaoruhusiwa ni ule unaofanywa kwa ajili ya kushindana katika kufanya mema.
Wivu wa namna hii sio ule wa kuchukia kuwa kwa nini fulani ameneemeshwa bali ni ule unaomfanya mja ajitahidi zaidi kufanya mema kama anavyofanya au kumzidi mwingine.
Mtume (swalla Allahu alayhi wasallam ametufahamisha ni husuda ya namna gani inayoruhusiwa kwa Muislamu katika Hadithi ifuatayo: Ibn Mas’ud (radhi za Allah ziwe juu yake) amehadithia kuwa Mtume wa Allah amesema: “Hapana husuda (inayoruhusiwa katika Uislamu) ila kwa watu wawili: “Mtu ambaye Mwenyezi Mungu (subhanahu wataala) amempa mali na akampa uwezo wa kuitumia katika njia ya Allah na mtu ambaye Allah amempa elimu na hekima akawa anafundisha wengine pamoja na yeye mwenyewe kuingiza elimu hiyo katika vitendo”. (Bukhari na Muslim).
Makusudio ya hadithi hii sio mtu amuonee husuda mwenzake kwa nini amepewa neema hizo yeye hajapewa. Anachotakiwa ni amuombee dua zile neema alizopewa azidi kuzitumia kwa ajili ya Allah (subhanahu wataala) na yeye ambae hakupewa basi amuombe Allah ampe ili azitumie kwenye njia ya Allah na si kutamani kwa ajili ya kujifakhirisha na kuwadharau wanaadamu wengine au kuwaletea madhara wanaadamu wengine. Muislamu unapomuona mwanadamu mwenzako yoyote yule ameneemeshwa neema na Allah iwe uzuri wa ufahamu,mali,watoto basi ni wajibu wako kumuombea kheri na barka kwa Allah na si kutamani vile vitu mwenzako vimuondokee.Na katika kumuombea kheri basi sema maneno yafuatayo kila unapomuona mwenzako ameneemeshwa neema yoyote ile.
“Masha Allah laa quwwata illa billah” maana yake ni (Haya ndiyo Allah aliyoyataka hakuna nguvu ila za Allah). Pia maneno mengine ni “Allahumma Baarik Alayhi “ maana yake ni (Ewe mola mbaarik kwa hicho”
Tunamuomba Allah atujaalie katika wale watakaokuwa wenye kutosheka na vile walivyopewa na Allah na tunamuomba Allah atuweke mbali kuwa katika watu wenye husuda.
Azitakase nyoyo zetu na atujaalie zenye kuambiwa mazur na kuyafata na kukatazwa mabaya na kuyaacha. Aaamin