Makala

MAWAIDHA YA KIISLAMU: Mazingatio kuhusu kisa cha mtu mwenye ukoma, kipara na kipofu

January 17th, 2020 Kusoma ni dakika: 3

Na HAWA ALI

KILA sifa njema zinamstahikia Allah Mola wa walimwengu wote na mlezi na mshughulikiaji wa mahitaji ya viumbe vyote. Swala na Salamu zimfikie kipenzi chetu na Mtume wetu, Mtume Muhammad Swallallahu Alayhi Wasallam.

Ndugu wa Kiislamu, hakika neema za Allaah Azzawajalla ni nyingi mno hazihesabiki kama Anavyotaja Mwenyewe katika Qur’an. Yeye Ndiye mtoaji rizki zote na Mwenye kudabiri (kuendesha) mambo yote. Lakini wengi miongoni mwa waja Wake hawashukuru, sababu; kuna baadhi ya watu hujaaliwa neema lakini hawatafakari wala kutambua kwamba inatoka kwa Allaah Pekee. Ikiwa ni neema ya mali, watoto, chakula, uhai, siha, hata kubakika katika usalama, amani na furaha ya nafsi nayo pia ni neema. Wengine hujaaliwa neema kadhaa na kadhaa lakini humshukuru mwengine. Wengine wanakanusha kabisa kwamba neema waliyojaaliwa ni kutoka kwa Mola wetu. Bali wengine hujaaliwa neema Zake lakini wanamshirikisha Allaah

Anasema hivyo katika kauli Yake:

“Na neema yoyote mliyonayo basi imetoka kwa Allaah [na nyinyi hamumshukuru]. Kisha inapokuguseni dhara mara Yeye mnamlilia [mnamlalamikia]. Kisha Anapokuondeleeni hiyo dhara, mara kundi moja miongoni mwenu linamshirikisha [tena] Mola wao. Wanazikanusha zile neema Tulizowapa, basi stareheni kidogo, karibuni mtajua [malipo yenu ya ubaya wenu].” [An-Nahl 16: 53-55]

Kisa kifuatacho cha watu watatu waliojaaliwa neema za Allaah Azzawajalla kinatupa mfano na mafunzo kuhusu kukanusha au kushukuru neema Zake Ta’ala. Nacho ni kisa katika Hadiyth ya Mtume (Swallallahu Alayhi Wasallam):

Imepokelewa kutoka kwa Abu Hurayrah RA kwamba kamsikia Mtume wa Allaah akisema: “Allaah alitaka kuwajaribu watu watatu katika wana wa Israaiyl; mkoma, kipofu na mnyonyoka nywele (kipara). Akawatumia Malaika.

Akamwendea aliye na ukoma akamuuliza: Kitu gani ukipendacho mno? Akajibu: Rangi na ngozi nzuri [ya mwili], na uniondokee [ukoma] niliokuwa nao unaowakirihisha watu kwangu. Akasema: [Malaika] Akamgusa ukamuondokea ugonjwa akapewa rangi na ngozi nzuri. Akamuuliza: Mali ipi upendayo zaidi? Akajibu: Ngamia au ng’ombe.

Basi mwenye ukoma akapewa ngamia jike mjamzito. [Malaika] Akasema [kumuombea]: Allaah Akubarikie navyo.

Kisha Malaika akaenda kwa kipara akamuuliza: Kitu gani ukipendacho mno? Akajibu: Nywele nzuri na kiniondokee [kipara] kinachowakirihisha watu kwangu. Akamgusa, kikamuondoka [kipara] akapewa nywele nzuri. Akamuuliza: Mali ipi upendayo zaidi? Akajibu: Ng’ombe au ngamia. Akapewa ng’ombe jike mja mzito. Akasema [kumuombea]: Allaah Akubarikie navyo.

Akamwendea kipofu: Akamuuliza: Kitu gani ukipendacho mno? Akajibu: Allaah Anirudishie macho yangu nipate kuwaona watu. Akamgusa, Allaah Akamrudishia macho yake. Akaumuuliza: Mali ipi uipendayo zaidi? Akajibu: Mbuzi. Akapewa mbuzi mjamzito. Baada ya hapo, wanyama wote watatu wakazaa na kuzaliana hadi kwamba kila mmoja alikuwa na bonde lilojaa ngamia, na mwengine bonde la ng’ombe na mwengine bonde na mbuzi.

Akasema: Kisha [Malaika] akamrudia mkoma akiwa katika hali kama yake ya mtu mwenye ukoma. Akasema: Mimi ni masikini, nimepotelewa na [vitu] mahitajio yangu yote safarini, kwa hiyo sina leo wa kunitimizia isipokuwa Allaah kisha wewe. Nakuomba kwa Ambaye Amekupa rangi na ngozi nzuri, na mali, unigawie ngamia ili anifikishe katika safari yangu. Akajibu: Nina majukumu mengi [kwa hiyo siwezi kukupa kitu!]. [Malaika] Akasema: Kama kwamba nakujua? Si wewe uliyekuwa na ukoma wakikirihika watu, na ulikuwa masikini kisha Allaah ‘Azza wa Jalla [Aliyetukuka na Utukufu] Akakupa mali [yote hii]? Akajibu: [Hapana ni uongo!] Hakika nimerithi yote hayo kwa mababu zangu. [Malaika] akasema: Ikiwa unasema uongo, basi Allaah Akurudishe kama ulivyokuwa awali.

Akamwendea aliyenyonyoka nywele (kipara) akiwa katika hali kama yake ya mtu mwenye kipara. Akamuuliza kama alivyomuuliza huyu [mwenye ukoma], naye akamjibu kama alivyojibiwa naye. Akamwambia: Ikiwa unasema uongo, basi Allaah Akurudishe kama ulivyokuwa awali.

Akasema: Akamwendea kipofu akiwa katika hali kama yake ya mtu kipofu. Akamwambia: Mimi ni masikini na msafiri, nimepotelewa na [vitu] mahitajio yangu yote safarini, kwa hiyo sina leo wa kunitimizia isipokuwa Allaah kisha wewe. Nakuomba kwa Ambaye Amekupa macho yako, unigawie mbuzi ili anifikishe katika safari yangu. Akajibu: Bila shaka! Nilikuwa kipofu na Allaah Akanirudishia macho yangu [na nilikuwa masikini Allaah Akanitajirisha]. Chukua utakacho, na acha utakacho, kwani waLlaahi sitakuzuia chochote [unachohitaji] kuchukua kwa ajili ya Allaah. Akasema [kumuombea]: Weka mali yako, kwani hakika mmejaribiwa, na Allaah Ameridhika nawe na Amewaghadhibikia wenzako.” [Al-Bukhaariy na Muslim]

Basi nasi tujiulize kama tunamshukuru Allaah Azzawajalla kwa neema Zake zote, hata ya neema ya kuvuta pumzi moja ya uhai ambayo ni kubwa mno! Tujitahidi kumshukuru kwa wingi kwani ni wachache mno wanaotafakari neema za Mola wao kama Anavyosema Mwenyewe katika kauli Yake:

“Na ni wachache wanaoshukuru katika waja Wangu”. [Sabaa 34: 13]

Pia tunatakiwa kuzichunga na kuzitumia vizuri neema za Allah Subuhaanahu Wataala kwani tutakwenda kuulizwa mbele ya Hakimu wa mahakimu vipi tulizitumia. Allah Anasema:

“Tena bila ya shaka mtaulizwa siku hiyo juu ya neema.” [At-Takaathur 102: 8]

Tunamuomba Allah atuwafikishe kuzitumia neema alizotupa katika njia anayoiridhia na iwe sababu ya kupata pepo yake. Amin.