Makala

MAWAIDHA YA KIISLAMU: Mitandao ya kijamii isiuteke moyo wako hadi ukaingia kiza

October 11th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na HAWA ALI

SIFA zote njema anastahiki Mola Azzawajalla, Mwenye kuneemesha neema kubwakubwa na nyingine ndogondogo.

Swala na salamu zimwendee Mtume wetu Muhammad, rahmatan lil ‘alamiyn, maswahaba wake kiram na watangu wema hadi siku ya Kiyaamah.

Kwanza, Muislamu anapoisikia adhana anatakiwa ainuke na kuhakikisha anaitikia mwito na kutoruhusu jambo lolote limzuie katika kuitika wito wa Allah Subhaanahu Wata’ala.

Anaseme Allah Subhaanahu Wata’ala:” Katika Nyumba ambazo Mwenyezi Mungu ameamrisha zitukuzwe, na humo litajwe jina lake, wanamtakasa humo asubuhi na jioni. Watu ambao biashara wala kuuza hakuwashughulishi na kumdhukuru Mwenyezi Mungu, na kushika Swala, na kutoa Zaka. Wanaikhofu Siku ambayo nyoyo na macho yatageuka”.

Adhana

Hivyo utakaposikia adhana, achana na Mtandao na nenda Msikitini kwa ajili ya kuitikia wito wake Allah Subhaanahu Wata’ala. Kama upo nyumbani (Mwanamke) hakikisha pia unaondoka kwenye Mtandao na kuitika wito.

Pili, mtandao ni njia ya mawasiliano ambayo ni kama msumeno. Inapoleta faida huwa ni zawadi nzuri na inapoleta maovu huwa mbaya na haifai. Kwa Muislamu ni kuhakikisha anautumia Mtandao kwa kuangalia upande wake mzuri tu ambao utamsaidia katika dini yake na maisha yake na si kuutumia katika maovu ambayo yatamuharibia dini yake na maisha yake.

Tatu, ni muhimu kwa watumizi wa Mtandao kuhakikisha wanakinga macho yao kwa kutoangalia yaliyoharamishwa.

Hii ni njia mojawapo ya Shetani kuharibu maadili ya Muislamu kwa kumpandikiza raha za muda mchache kisha kumuachia hisia za majuto na masikitiko ya muda mrefu.

Kuangalia mambo ambayo Allah Subhaanahu Wata’ala ameharamisha huondosha nuru kwenye nyoyo na kuleta kiza na uzito kwenye vifua mpaka Muislamu kuwa mzito katika kutekeleza Ibadah.

Shetani huuchukua moyo wa mja na kuutawala na kuuchezea kama mtoto mdogo anavyocheza na mpira. Na mwishowe ni kupotoka

Nne, Chukua tahadhari na kujiunga na tovuti/vikundi vya mazungumzo na porojo (chatting group sites).

Huu ni mtego kwa waislamu wanaume na waislamu wanawake kuwaingiza katika mahusiano haramu na mwishowe kuwaacha katika maumivu yatakayoweza kuathiri maisha na imani yao.

Isitoshe, ni moja kati ya mawili; ama mtandao uutawale au ukutawale.

Ukiweza kuutawala ndipo utakapoweza kufaidika nao na kujiweka mbali na ubaya wake. Na ukikutawala, macho yako hudanganyika na starehe za raha za muda mchache, pesa zako kuibiwa, muda wako kupotea na kushindwa kutekeleza majukumu yako katika maisha kwa familia na vipenzi vyako. Umetegwa bila ya mwenyewe kujijua.

Ni wajibu wako kujitoa katika mtego kabla hujapotoka au mambo yamesharabika ukawa huwezi tena kuachana nao.

Mwisho kumbuka chochote unapakia au kutolea maoni ikiwa ni kwa siri au dhahiri Malaika wanarekodi.

Ukijifanya mjuaji wataka sifa kwa kuweka uchafu mitandaoniau hodari wa kuweka mafumbo masengenyo au fitna basi utayapata yote ulioandika umewekewa mbele yako siku ya kiyama.

Mume na Mke chungeni sana Mtandao usiwaharibie ndoa yenu, tosheka na mumeo au mkeo usimpe nafasi mwanamume au mwanamke yoyote akuharibie ndoa yako, weka mambo yako wazi kwa mwanandoa mwenzako, kumbuka unaweza kuwa unachat na mwanamke au mwanamume kwa whattsap na mumeo au mkeo hajui lakini kuna siku atakuja kuyaona yote hayo na hapo uaminifu baina yenu utaingia ufa…

Kakangu chunga mtandao usije ukakukosesha kazi kwa kutumia muda mwingi mpaka ukafutwa kazi…

Dadangu mpe mumeo haki yake kwa vile unavyoishika simu yako na kufurahi nayo wakati unachat ndio hivyo umfurahishe mumeo, maliza majukumu yako kwanza what’s up itafuata baaadae..

Kumbuka Allah Subhanahu wataala anaona yote ufanyayo kwa siri na dhahiri…