Makala

MAWAIDHA YA KIISLAMU: Mwislamu anavyopaswa kujiandaa na msimu wa mvua iliyopitiliza kama hii

October 25th, 2019 Kusoma ni dakika: 3

Na ALI HASSAN

KWA jina la Mwenyezi Mungu mwenye kuneemesha neema kubwa kubwa na neema ndogo ndogo. Ama kwa hakika ni siku nyingine ambayo Mola wetu ametujaalia kukutana ili kukumbushana neno lake Maulana; Mola wetu.

Kabla ya kujitoma katika mada ya leo, ni vema na aula kumshukuru mno Muumba wetu aliyetukuka ambaye ndiye Muumba wa ardhi na mbingu na vyote vilivyomo.

Hapana mwingine anayestahili kuabudiwa, kuenziwa ila ni yuyo huyo mmoja pekee: Allah (SWT).

Katika uzi uo huo wa ufunguzi na kumshukuru Manani wetu, pia tuchukue uzito wa nafasi hii tukizi sisi waumini wa dini hii tukufu ya Kiislamu kumtakia kheri na kumtilia dua na kumfanyia maombi Mtume wetu (SAW).

Mada yetu leo hii ndugu yangu inaendana na hali ya hewa ilivyo sasa kote nchini, barani mwetu na hata nje ya bara. Hali ya hewa ambayo baadhi ya watabiri wa hali ya hewa, kwa uwezo wake Maulana, walikuwa wametabiri kuwa itakuwa hivyo na ikatukia hivyo. Ajabu ni kuwa baadhi yetu tulipinga utabiri huo na pia kupuuza hatua za tahadhari ambazo tulipewa na wabashiri hao wa hali ya hewa.

Ole wake binadamu!

Ya Rabi tujaalie hali nzuri ya hewa.

Aidha, baadhi yetu hushindwa tutasema nini hali ya hewa inapobadilika pakubwa. Hatujui tuseme maombi gani wakati wa kiangazi; hatujui tutie dua gani wakati wa mvua kama hizi ambazo zimetujia kwa sasa.

Mvua kubwa sio kwamba tu huacha madhara makubwa ya kusombwa kwa madaraja, majumba, madarasa, miundo msingi, mimea na uharibifu mwingineo, lakini pia hutuacha na majonzi makubwa ya kuwapoteza wapendwa wetu na rasilamali nyinginezo kama mifugo.Ni picha za kuatua moyo kuona kuwa waja wanasombwa na kuuawa na maji ya mvua! Inasikitisha kuziona picha kwenye vyombo vya habari ambapo mifugo iliyokuwa hai dakika tano zilizopita, sasa imegeuzwa mizoga!

Ewe Mola wetu twakulilia.

Wanafunzi wetu, hasa wale ambao wanakabiliwa na mitihani ya kuufunga muhula, kuuga mwaka – ikiwemo mitihani ya kidato cha nne (KCSE) na mitihani ya darasa la nane (KCPE) – wanakabiliwa na wakati mgumu. Njia hazipitiki. Baadhi madarasa yamesombwa. Wengine wanakabiliwa na kipindi kigumu sana mno kufuatia shule zao kufungwa kwa kutoafikia viwango vinavyohitajiwa na wizara ya elimu.

Hili nalo likichangiwa zaidi na janga la shule ya Precious Talent iliyoporomoka mtaani Dagoreti.

Majuzi huko Japani pia tumeshuhudia kimbunga kikali cha Hagibis. Hicho nacho pia kikaondoka na nyoyo za waja.

Je, sisi waumini wa dini hii tukufu ya Kiislamu twaambiwa tuseme nini kuomba mvua inye. Na inapokuwa ikinya, tuseme nini au tutie dua gani? Ama sisi waja leo hii tumejisahau kiasi kwamba tumeishia tu kulaani na kulalama?

Dua ya mvua huwa ni maneno machache na mepesi:

“Ewe Mwenyezi Mungu, ijaaliye yenye kumiminika yenye kunufaisha.”

Ama pia namna tulivyofunzwa:

“Ewe Mwenyezi Mungu tunyeshelezee mvua yenye kuokoa, nyingi, yenye kustawisha, yenye manufaa isiyodhuru, ya harakaisiyochelewa.”

Pia twaweza kusema:

“Ewe Mwenyezi Mungu, tuokoe kwa kututeremshia mvua, Ewe Mwenyezi Mungu, tuokoe kwa kututeremshia mvua”

“Ewe Mwenyezi Mungu, tuokoe kwa kututeremshia mvua. Ewe Mwenyezi Mungu wanyeshelezee waja wako, na wanyama wako, na eneza rehema zako, na fufua nchi yako iliyokufa.

Kutoka kwa Bibi Aisha R.A.A.H. kasema, “Mtume S.A.W. anapoona mvua (inanyesha) alikuwa akisema:

Allahumma ij`alhu sayyiban hanian.

Maana yake, “Ewe Mwenyezi Mungu ijaalie iwe mvua kubwa nzuri (yenye kheri)”.

Kutoka kwa Bibi Aisha R.A.A.H. kasema, “Mtume S.A.W. anapoona mvua (inanyesha) alikuwa akisema, [2]”

Allahumma sayyiban naafian.

Maana yake, “Ewe Mwenyezi Mungu ijalie iwe mvua kubwa yenye mafanikio.”

Kama tu ambavyo sisi waja hukutamnika katika maabadi makiwanda na kutia dua ije na kunya mvua ya kheri, pia ni muhimu kuzidisha ibada ikinya inye mvua ya kheri isiyokuwa na hasara.

Si jambo zuri kuwasikia waja sisi tukilalama mara sijui nini usumbufu wa mvua na mafuriko na matope. Tuwe wengi wa dua na maombi.

 

Ijumaa Kareem!

[email protected]