Makala

MAWAIDHA YA KIISLAMU: Ni masikitiko ikiwa kuna baadhi yetu tunaokosa fadhila za mfungo

May 17th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na HAWA ALI

SIFA zote njema anastahiki Mola Azzawajalla, Mwenye kuneemesha neema kubwakubwa na nyingine ndogondogo. Swala na salamu zimwendee Mtume wetu Muhammad, rahmatan lil ‘alamiyn, maswahaba wake kiram na watangu wema hadi siku ya Kiyaamah.

Hakika mwezi wa Ramadhan ni mwezi miongoni mwa miezi 12 ya mwaka mzima. Ambao Allah (Subuhaanahu wa Ta’ala) Ameuchagua mwezi huu na akaupa hadhi kubwa, na ni mwezi wenye fadhila nyingi. Miongoni mwa fadhila za mwezi huu mtukufu; ni kuwa huu ni mwezi wa kusamehewa madhambi, ni mwezi wa subira, ni mwezi wa Qur-aan, milango ya moto hufungwa na milango ya pepo hufunguliwa na Mashaytwaan hufungwa, ni mwezi ambao una siku iliyo bora kuliko miezi elfu nayo ni siku ya Laylatul Qadr, ni mwezi wa Du’aa; kwani maombi katika mwezi huu ni yenye kujibiwa, ni mwezi wa kutoa na mengi mengine.

Kwa hakika ni mwezi wa ‘Ibaadah na ‘amali zake zina ujira mkubwa katika mwezi huu kuliko miezi mingine.

Lakini basi ni masikitiko makubwa kwa watu walio wengi zinawapita fadhila hizi ima kwa sababu ya ujinga au kwa kufuata matamanio ya nafsi zao.

Alisikika Mtume (Swalla Allahu ‘alayhi wa sallam) alipokuwa Msikitini kwenye Minbar aliitikia Aamiyn, Aamiyn, Aamiyn, Maswahaba wakamuuliza Ya Rasuula Allaah tumekusikia ukiitikia Aamiyn mara tatu;

“Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: Alinijia Jibriyl (‘Alayhis Salaam) akaniambia ni khasara iliyoje ya mtu imemfikia Ramadhaan na isiwe ni sababu ya kusamehewa madhambi yake, sema Aamiyn, kisha akanambia ni khasara iliyoje ya mtu aliyewadiriki wazazi wake wawili na isiwe ni sababu ya kuingia Peponi, sema Aamiyn, kisha akanambia ni khasara iliyoje kwa mtu aliyesikia akitajwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kisha asimswalie, sema Aamiyn.”

Ukweli miongoni mwa watu walio wengi wamekosa msamaha na fadhila za mwezi huu mtukufu, wameacha mafundisho sahihi ya Dini yetu tukufu ya Kiislamu na makosa mengi yanafanywa na wengi wetu.

Nami nakusudia hasa kutaja baadhi ya makosa yanayofanywa na walio wengi katika mwezi huu mtukufu wa Ramadhaan, namuomba Mola Mtukufu aniwezeshe inshaAllaah.

Baadhi Ya Makosa Yafanywayo Mwezi Wa Ramadhaan

Miongoni mwa watu wanahifadhi Swawm zao za Ramadhaan na kisimamo cha Taarawiyh na Swalah za faradhi kila mwaka na ‘Ibaadah nyingine, lakini ‘Ibaadah zao wanazipeleka arijojo kwa kumshirikisha Allah Mtukufu, wanakwenda kwa waganga kupiga ramli, kuangalia bahati kwa kupitia ‘nyota zenu’, na du’aa zao hawazielekezi kwa Allah moja kwa moja bali wanaomba mizimu, makaburi na kuvaa mahirizi wakitaraji zinawakinga na madhara na Shaytwaan, hali Allah Azzawajalla Amelikemea sana jambo hilo, Amesema Allaah (Subuhaanahu wa Ta’ala)

“Kama ukimshirikisha (Allaah) bila shaka ‘amali zako zitaruka patupu, (hutozipatia thawabu japo ni ‘amali njema); na lazima utakuwa miongoni mwa wenye khasara.” Az-Zumar: 65

Hivyo basi mshirikina hatokubaliwa matendo yake mpaka aache ushirikina atubie kwa Mola wake na ampwekeshe katika ‘Ibaadah zake ndio zitapokelewa ‘amali zake.

Na miongoni mwa watu wameufanya mwezi wa Ramadhaan ni mwezi wa kucheza na mambo ya upuuzi, mwezi wa kupoteza wakati na kuifanya

Swawm ni jambo jepesi bila mazingatio yoyote; utawaona watu mchana wa Ramadhaan na usiku wake wanacheza Karata, Keram, Dhumna, Bao na mfano wake.

Wamejikusanya makundi makundi wake kwa waume watoto kwa wazee wamechanganyika wala hawaoni hayaa, na wengine wameufanya ni mwezi wa kupiga ngoma khasa ukiangalia katika nchi zetu za Afrika Mashariki; wanadai kupiga ngoma kuamsha watu kula daku, na wengine hucheza ngoma hizo khasa ikaribiapo siku ya ‘Iyd huanza kupiga ngoma zao mchana wa Ramadhaan wakiomba ‘Idi toa’, yaani wapewe pesa na huku wanaume wakiwa wamejivisha mavazi ya kike na kukata viuno hadharani!! Hawajui kuwa hiyo ni laana!