Makala

MAWAIDHA YA KIISLAMU: Salamu ni zawadi ya Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa waja wake

July 12th, 2019 Kusoma ni dakika: 3

Na HAWA ALI

SIFA zote njema anastahiki Mwenyezi Mungu Subuhaanahu Wata’ala, Mwenye kuneemesha neema kubwakubwa na nyingine ndogondogo.

Swala na salamu zimwendee Mtume wetu Muhammad, rahmatan lil ‘alamiyn, maswahaba wake kiram na watangu wema hadi siku ya Kiyaamah.

Leo inshaa Allah tutatupia jicho suala la umuhimu wa salamu ambazo kwa kawaida huzikurubisha pamoja nyoyo zetu.

Wakati watu wawili wanapokutana, kitu cha kwanza wanachokifanya kwa ajili ya kudhihirisha mapenzi yao, ni kusalimiana na kisha kufuatia hatua zingine kama kupeana mikono na kadhalika. Kwa hakika moja ya mipango ya kujenga ubinaadamu na kuimarisha mapenzi ya Kiislamu ambayo pia ni suala linaloweza kuondoa nyongo na badala yake kustawisha mahaba kati ya wanaadamu ni kutoleana salamu. Aidha kupeana mikono sambamba na salamu, ni moja ya mambo yanayowakurubisha pamoja zaidi wanadamu. Tunapomtolea salamu mtu wa upande wa pili, ni wazi kwamba, huwa tunataka kujua hali yake ya kiafya ba kadhalika. Kupeana mikono na kuitikisa katika hali ya kusalimiana, ni ishara nyingine ya mapenzi na kutakiana heri kati ya pande mbili. Kuamkuana kwa kupeana mikono, huziweka nyoyo pamoja. Inatupasa tujiulize swali moja nalo ni hili kwamba, ni nini siri ya jambo hilo?

Kwa mujibu wa aya ya 23 ya sura ya Hashr, salamu imetajwa kuwa moja ya majina yake Mwenyezi Mungu. “Yeye ndiye Mwenyezi Mungu ambaye hapana aabudiwaye kwa haki isipokuwa Yeye tu, Mfalme, Mtakatifu, Mwenye salama….” Kwa ajili hiyo kila mwanzo wa salamu, usafi na uzima ni vyake yeye Mwenyezi Mungu Mtukufu. Mwenyezi Mungu Muumba wa kila kitu ambaye ni mpole, huwasalimu waja wake kwa salamu ambazo zimejaa baraka na Amani.

Kadhalika salamu iliyotajwa katika sura ya Taha aya ya 47 isemayo: “….Na amani iwe juu ya anayefuata muongozo.” Bila shaka salamu haihusu duaniani peke yake, bali pia wakati wa kufarijika na rehema za Mwenyezi Mungu katika siku ya Kiyama pia kutatolewa salamu ambayo ndiyo zawadi na maamkizi maalumu kwa ajili ya waja wake wema. Malaika nao pia watawakaribisha watu wa peponi kwa salamu kwenye meza pana ya neema za Mwenyezi Mungu, kama wanavyowatolea salamu na maamkizi ya Mwenyezi Mungu wakati wa kutolewa roho zao.

Ukweli ni kwamba, waumini wa kweli hupewa salamu kutoka kwa kila mtu mwenye imani kama vile wapewavyo salamu hizo kutoka kwa malaika, marafiki na watu wanaosafiri nao kwenda peponi. Aidha masikio ya watu hao, yaani waumini hayatasikia kitu kingine ghairi ya salamu na hujitenga na kila aina ya upuuzi, mambo yasiyo na faida na dhambi. Katika aya ya 127 ya sura ya al-An’aam, Qur’ani Tukufu inaeleza ukweli kuhusiana na suala hilo na kuitaja pepo kuwa ni nyumba ya amani na salama kwa kusema: “Watu wema watapata nyumba ya salama kwa Mola wao, naye ni Kiongozi wao kwa sababu ya yale waliyokuwa wakiyatenda.”

Hakuna shaka kuwa, jina ‘Daru Salaam’ lililotumika katika aya hii lina maana ya nyumba ya Mwenyezi Mungu, kwa sababu neno Salaam ni moja ya majina yake mazuri, ambapo amelitumia jina hilo kwa ajili ya kuisifu na kuitukuza pepo. Hali hiyo inabainika wazi pia kuhusiana na Al- Ka’abah ambapo ameitaja kuwa ni nyumba yake. Nyumba ya ‘Salama’ pia ni nyumba ambayo imejaa ndani yake usalama na wala wakazi wake hawana jambo lingine ghairi ya usalama na amani, kwa sababu watu hao hawatapatwa na umasikini, shida, maradhi, kutengana na wapendwa wao, vifo wala uzee.”

Sambamba na salamu kuleta mapenzi na ukunjufu wa nyoyo kati ya watu, pia huleta hali ya unyenyekevu na kuepukana na jeuri.

Watu wanyenyekevu si tu kwamba huwa hawapati hasara na madhara, bali pia hupata izza na mapenzi kutoka kwa wenzao.

Ni kutokana na umuhimu wa suala hilo ndipo mtukufu Mtume Muhammad Swallallahu Alayhi Wasallam daima akawa anawatangulia watu wengine kutoa salamu na katu hakuna mtu yeyote aliyemtangulia kutoa salamu.

Aidha mtukufu Mtume Alayhi Salaam alieneza tabia hiyo njema kwa watoto na alikuwa akisema: “Maadamu nipo hai sitoacha kuwasalimia watoto hadi hapo amali hii itakapofanywa kuwa sunna baada yangu.”

Chimbuko la sifa hii nzuri ya Mtume ni tabia njema, roho safi na unyenyekevu. Katika kuishawishi zaidi jamii ya Waislamu itekeleze amali hiyo njema Mtume Swallallahu Alayhi Wasallam alisema, “Kuna thawabu 70 kwa kila salamu moja na jibu lake, ambapo kati ya hizo 69 ni za mtoaji salamu na moja ni ya yule mwenye kujibu.” Aidha mtukufu huyo amesema: “Mtu bakhili na mchoyo ni yule ambaye anafanya ubakhili katika utoaji salamu.”

Salamu ni aina ya maamkizi ya Kiislamu na asili ya neno “Tahiyyat-Maamkizi” linatokana na neno “Hayy-hai” ikimaanisha kumtakia uhai na maisha yule anayesalimiwa. Qur’ani Tukufu inasema hivi katika aya ya 61 ya sura ya an-Nur: “….Na mnapoingia katika majumba basi mtoleane salamu, ni maamkio yanayotoka kwa Mwenyezi Mungu yenye baraka njema. Hivyo ndivyo Mwenyezi Mungu anavyokubainishieni Aya ili mpate kufahamu.”

Aya hii inataja salamu kuwa, maamkizi ya Mwenyezi Mungu ambayo mbali na kuwa ni maamkizi, lakini pia ni yenye baraka nzuri. Aidha kwa mujibu wa aya hii itafahamika hapa kuwa maana halisi ya neno, “Salamu Alaykum-amani iwe juu yenu” inatokana na asili ya neno “Salamullahi Alaykum” ikimaanisha, “amani ya Mwenyezi Mungu iwe juu yenu, Mwenyezi Mungu anakutoleeni salamu na dumuni katika amani.”

Kwa ajili hiyo kusalimiana ni moja ya njia za kutangaza urafiki na udugu. Amri hii ya Kiislamu imejengeka juu ya msingi mkuu wa kuimarisha uhusiano wa kijamii kati ya watu wote.

Allah atujalie kheri na Baraka za salamu tunazotoa.

Amin.