MAWAIDHA YA KIISLAMU: Sifa za kihakika za Waumini halisi wa Mwenyezi Mungu
Na HAWA ALI
SIFA zote njema Anastahiki Mola wa viumbe vyote, Yeye Ndiye Mlinzi wa Waumini wa kweli.
Enyi ndugu zangu Waumini! Hakika Allah Aliyetukuka Ameumba viumbe ili wamtii na wamuabudu, Naye Hataki kutoka kwetu riziki wala Haitaji wamlishe.
Kwani Yeye Allah Ndiye Mwenye kuruzuku, Mwenye nguvu madhubuti kabisa.
Na daraja kubwa ya Imani ni kumuamini Allah, na Malaika Wake, na Vitabu Vyake na Mitume Wake na Siku ya Mwisho. Qur-aan imetubainishia sifa za Waumini wa kweli kama ifuatavyo:
“Hakika Waumini ni wale ambao anapotajwa Allaah nyoyo zao hujaa khofu, na wanaposomewa Aya Zake huwazidisha Imani, na wakamtegemea Mola wao. Hao ambao wanashika Sala na wanatoa katika yale tunayo waruzuku” (8: 2 – 3).
Wenye Imani walijua hakika hii na hivyo kuijaza mioyo yao Imani kwa Allah peke Yake, ambaye mkononi Mwake umo Ufalme wote; na Yeye ni Mwenye uweza juu ya kila kitu. Na kama inavyoeleweka kuwa Muumini mkamilifu ni yule mwenye kutekeleza wajibu wa Allah na mwenye kumtegemea Yeye katika kila jambo na anapotajwa Allah basi nyoyo zao hujawa na hofu na aya Zake zinaposomwa Imani yao huongezeka na pia huwa na yakini juu ya yakini.
Hivyo, huwafanya wawe ni bishara njema kwa ahadi Yake na kuogopa adhabu Yake.
Imani katika nafsi ya Muumini inapanda na kuwa juu ya kila kitu na hivyo na mafungamano ya karibu na Allah, hivyo kutoweza kushughulishwa na kitu chochote ambacho kinaweza kumtoa katika Imani hiyo. Allah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anasema:
“Watu ambao biashara wala kuuza hakuwashughulishi na kumdhukuru Allaah, na kusimamisha Swalaah, na kutoa Zakaah. Wanaikhofu Siku ambayo nyoyo na macho yatageuka” (24: 37).
Hivi ndivyo watu wa Imani walivyoshikia Imani yao na kuwa na uhusiano na Mola wao na kufanya amali katika kumridhisha Allah (Subhaanahu wa Ta’ala) kwa viungo vyao na mioyo yao.
Yalikuwa mafungamano ya watu hawa kwa ndugu zao Waumini ni mafungamano ya ndugu kwa nduguye, anampenda kwa ajili ya Allah na kumchukia kwa ajili ya Allah, anampa kwa ajili ya Allah na kumyima kwa ajili ya Allah (Subhaanahu wa Ta’ala). Hilo ni kuhakikisha kauli ya Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
“Mwenye kupenda kwa ajili ya Allah na kuchukia kwa ajili ya Allah, na kutoa kwa ajili ya Allah na kuzuia kwa ajili ya Allah, hakika yeye atakuwa amekamilisha Imani yake”.
Hivyo, mafungamano baina ya Waumini yalikuwa ni mahusiano baina ya viungo katika mwili mmoja. Na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anapigia mfano kuhusu hilo pale aliposema:
“Mfano wa Waumini katika kupendana na kurehemeana kwao na kuhurumiana kwao ni sawa na mwili mmoja, kikishtakia kiungo kimoja basi mwili mzima utakosa usingizi na kushikwa na homa” [Al-Bukhaariy].
Rehema inajenga mahusiano baina yao, na mapenzi na mahaba yanawajumlisha pamoja na kuzifunga pamoja nyoyo zao. Hivyo wakawa kama ilivyotajaQur-aan:
“Muhammad ni Mtume wa Allaah. Na walio pamoja naye wana nguvu mbele ya makafiri, na wanahurumiana wao kwa wao. Utawaona wakiinama na kusujudu wakitafuta fadhila na radhi za Allaah. Alama zao zi katika nyuso zao, kwa athari ya kusujudu” (48: 29).
Na kwa sifa hizi zilizotajwa waliweza kuhakikisha katika nafsi zao mafunzo ya Dini yao na muongozo wa Nabii wao, wakawa ni wenye kuamrisha mema na kukataza maovu, na pia kuusiana kwa haki na kuusiana kusubiri na wanasaidiana katika wema na ucha Mungu na wala hawashirikiani katika maovu na uadui.
Muumini anatambua haki ya nduguye Muumini katika kuyalinda mali yake, heshima yake, na cheo chake na kumtetea juu ya Dini yake wala hawakiuki mipaka baadhi yao kwa wengine wala hawaudhiani kwa maneno wala matendo, hivyo kuhakikisha kauli ya Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) pale aliposema:
“Muumini ni yule ambaye watu hupata usalama kwake na Muislamu ni yule ambaye Waislamu wenziwe husalimika na mdomo wake na mkono wake” [At-Tirmidhiy na An-Nasaaiy kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘anhum)].
Na katika riwaya nyengine: “Na Muhaajir ni yule anaye yahama maovu”.
Enyi ndugu zangu watukufu! Hakika katika sifa nyeti na za kipekee za Waumini walio wakweli ni kushindana katika Njia ya Allah na kujitolea mhanga kwa nafsi na mali yake katika kuhakikisha ushindi na kupata shahada kwa ajili ya haki na Dini.
Kwa ajili hiyo, hawahepi katika vita wala hawabaki nyuma katika matukio na kwa hayo hapana tofauti baina ya wakongwe wao wala wadogo kati yao, na wanaume na wanawake wao na mifano ya hiyo katika historia ni mingi iliyo mashuhuri na maarufu. Ni ushujaa wa kipekee na kujitolea mhanga kukubwa.
Enyi Waislamu! Hakika Waumini wa kweli kwa Allah wanakua na starehe na neema ya azima yenye nguvu katika kupambana na matukio tofauti.
Hakika wao wanachukua fursa ya kuigeuza hofu kuwa utulivu na amani na kupigania maisha kwa maslahi ya haki na kheri. Na wanabadilisha kuharibikiwa kwa kuleta ushindi na kufaulu, na kushindwa kwa kufikia kufuzu na ufanisi. Hawa ndio Waumini wa kweli na haki.
Enyi Waislamu! Hakika Imani – Na hii ndio sehemu yake ya kihakika katika Ummah huu – taklifu yake ni kuu na tukufu. Ni wajibu iwe na dhumuni la kimatendo kama methodolojia na tabia ambayo itasimama juu ya nguzo zake na kuwekwa katika vigezo vyake na kusimama kwenye njia bainifu na hivyo kuitafsiri katika yanayojiri hivi sasa. Anasema Allah Aliyetukuka:
“Na anayefanya mema, akiwa mwanamume au mwanamke, naye ni Muumini – basi hao wataingia Peponi wala hawatadhulumiwa hata kadiri ya tundu ya kokwa ya tende” (4: 124).
Waja wa Allah, hizi ni baadhi ya sifa za Waumini katika mahusiano yao na Mola wao , na mafungamano mazuri na ndugu zao, na kushindana katika mambo ya Dini yao.
Hivyo, ni vyema kuzitaja na kuzikumbuka sifa hizo na kupata mazingatio na mawaidha ndani yake na ni juu yetu kushikamana na Dini yetu na kuiga maadili na tabia za Mtume wetu Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na kuifuata Sunnah yake kwa kadri ya uwezo wetu wala tusiipuuze wala kuikejeli na kuifanyia mzaha.
Hivyo mcheni Allah haki ya kumcha wala msife isipokuwa katika Uislamu na turudi kwa Mola wetu na tutubu kwa makosa na madhambi tunayoyafanya mchana na usiku, kwani Yeye ni Mwingi wa kusamehe.
Tunamuomba Allah Atutakabalie ‘amali zetu na Atuepeushie na makosa pamoja na madhambi na Atupatie mema na mazuri hapa ulimwenguni na mema na mazuri Kesho Aakhirah na Atuepushe moto wa Jahanamu.