Makala

MAWAIDHA YA KIISLAMU: Tawhid ni msingi muhimu wa dini wa kumuamini Mwenyezi Mungu pekee

July 19th, 2019 Kusoma ni dakika: 3

Na HAWA ALI

SIFA zote njema anastahiki Mwenyezi Mungu, Muumba wa mbingu na ardhi na vilivyomo.

Swala na salamu zimwendee Mtume Muhammad, Swallallahu Alayhi Wasallam, Maswahaba wake kiram na watangu wema hadi siku.

Katika dini Kiislamu, msingi muhimu zaidi ni Tawhid (Kuamini Mwenyezi Mungu mmoja pekee).

Kwa ufafanuzi zaidi, Tawhid inajumuisha kumuamini Mwenyezi Mungu mmoja pekee, muumba wa viumbe vyote, asiyekuwa na mfano wala mshirika na mwenye sifa zisizokuwa na mapungufu. Imani hii hubainishwa kwa kutamka kauli ifuatayo;La ilaha illallah.

Quran takatifu imeelezea imani ya Tawhid kuwa ni upekee wa Mwenyezi Mungu pamoja na sifa zake zote kwenye aya zinazosema; Mwenyezi Mungu ni mmoja pekee, hawezi kuhitaji chochote wala kumtegemea yeyote kwa msaada, hakuzaa wala hakuzaliwa na wala hana mfano wake.

Hawezi pia kushirikishwa na kiumbe chochote. Laiti kungekuwa na Mwenyezi Mungu zaidi ya mmoja, basi bila shaka utaratibu wa ulimwengu ungevurugwa.

Yeyote anayemshirikisha Mwenyezi Mungu anahesabika kuwa amefanya kufuru. Mwenyezi Mungu hachagui wala habagui. Viumbe wote ni wake na wanapaswa kumuabudu yeye pekee.

Tawhid ni utekelezaji wa ibada za Mwenyezi Mungu ili kuonyesha mapenzi kwake na kumtukuza kikamilifu kama Muumba wa pekee asiyekuwa na mshirika.

Ni kuamini kwamba Mwenyezi Mungu pekee ndiye anastahili kuabudiwa na kuombwa msaada kwa kila jambo.

Yeye ndiye anayetoa na anayejaalia katika maisha ya wanadamu.

Hivyo basi, kanuni na masharti yote aliyoyaweka Mwenyezi Mungu yanapaswa kuzingatiwa na kufuatwa pasi na kukengeuka.

Kwa kuzingatia haya, mwanadamu hana budi kuweka imani kamili kwa Mwenyezi Mungu ili kuweza kupata mwongozo bora wa kimaisha.

Uislamu umebainisha utofauti uliopo katika mfumo wa ulimwengu mzima kwa ujumla.

Dini ya Kiislamu imefikia watu wa jamii mbalimbali wanaoishi katika maeneo tofauti ulimwenguni.

Licha ya utofauti huo kuwepo, manabii na mitume wote waliwasilisha ujumbe mmoja kwa njia ya wayhi kutoka kwa Mwenyezi Mungu kuhusiana na dini ya Kiislamu ili kuleta mwongozo kwa wanadamu.

Mfumo wa ulimwengu

Kwa kifupi, tunaweza kusema kwamba Uislamu umebeba mfumo mzima wa ulimwengu.

Uislamu haubagui mwanadamu kulingana na jamii au uhalisia wa kijinsia. Uislamu ni mwongozo unaosaidia wanadamu wote kuishi vyema kwa misingi ya kanuni bora za kimaisha zilizowekwa na Mwenyezi Mungu.

Kila kitu kilichopo katika ulimwengu huu kimeumbwa na kuwekwa na Mwenyezi Mungu kwa taratibu zake maalum za kimaisha. Uislamu unahakikisha ukweli, haki, usawa, usalama, ukarimu, hisani, upole, utulivu, uwajibikaji, na kanuni nyingine zote zinazoendana na ubora wa maisha ya wanadamu.

Kitu kingine muhimu kinachobainisha thamani ya mwanadamu ni akili aliyojaaliwa na Mwenyezi Mungu.

Kulingana na dini ya Kiislamu, akili ni uwezo mkubwa aliojaaliwa mwanadamu na Mwenyezi Mungu.

Kutokana na uwezo huo, mwanadamu anaweza kutambua na kutenganisha kati ya jambo zuri na baya, au lenye faida na lisilokuwa na faida.

Kuwa na akili ni mojawapo ya sifa zinazowatofautisha wanadamu na viumbe wengine. Sifa hii imeweza kuwafanya wanadamu kuwa na wadhifa mkubwa zaidi kuliko viumbe wengine. Kuna aya katika Quran na hadithi pia zinazosisitiza wanadamu kutumia akili kabla ya kuchukuwa maamuzi ya kutenda jambo lolote.

Uislamu unahimiza wanadamu kutumia akili zao walizojaaliwa na kufuata kanuni, masharti na maamrisho ya Mwenyezi Mungu. Imani ya Kiislamu ya Kiislamu hujengwa kwa kuzingatia mafunzo ya dini na kutumia akili tulizojaaliwa.

Kwa namna hii, daima Waislamu wanatarajiwa kutumia akili zao kwa ajili ya kuchukuwa maamuzi bora yanayostahili katika suala la imani ya kidini.

Watu wasiotumia akili zao hupotea njia na kuchukuwa maamuzi ya kufanya mambo yaliyoharamishwa kama vile ulevi, utumiaji wa madawa ya kulevya na utumiaji wa vitu vingine visivyokuwa halali.

Wanadamu ni viumbe walioumbwa kwa ubora zaidi kuliko viumbe vingine vyote kama inavyoelezewa katika aya ya Quran tukufu inayosema: “Hakika tumemuumba mwanadamu kwa maumbile yaliyo bora zaidi; Kutokana na sababu hii, wanadamu wanapaswa kutambua thamani yao mbele ya Mwenyezi Mungu aliyewaumba na kuzingatia maamrisho yake kwa kutekeleza ibada.

Imani ya mwanadamu haitegemei na jinsia yake, chimbuko, tabaka wala hadhi ya jamii. Ni jukumu la kila mwanadamu kuwa na imani kamilifu ya dini ya Kiislamu.