Makala

MAWAIDHA YA KIISLAMU: Tujitahidi kuboresha ibada zetu kumi la mwisho likifika ukingoni

May 31st, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na HAWA ALI

SIFA zote njema anastahiki Mwenyezi Mungu Azzawajalla, Mwenye kuneemesha neema kubwakubwa na nyingine ndogondogo. Swala na salamu zimwendee Mtume Muhammad Swaalla Allahu ‘alayhi Wasallam.

Enyi Waislamu, Siku za mwezi mtukufu wa Ramadhani zinaendelea kuisha. Na hivi sasa tuko katika kumi la mwisho.

Je ndugu yangu Muislamu umejiuliza suala moja; Je, nimefaidika kiasi gani na siku zilizopita? Kuwa mkweli na nafsi yako na ujifanyie hisabu ya vitendo vyako kabla hujafika siku ya kufanyiwa hisabu.

Ndugu Mwislamu, bado wakati upo, na fursa ya kufanya mambo ya kheri bado inaendelea.

Kumi la mwisho ni muhimu katika umri wa mwanadamu, ndani yake kuna usiku mtukufu. Mwenye kuafikiwa usiku huo basi amepata kheri ya dunia na akhera.

Na mwenye kukosa usiku huo basi amekosa kheri ya dunia na akhera.

Ni hasara iliyoje mtu kuishi duniani miaka mingi kisha aondoke duniani patupu bila ya kupata kheri ya dunia wala kheri ya akhera.

Tafakari na uzingatie, hujui kama utafika mwakani ili uweze kufunga Mwezi wa Ramadhan.

Watu wema walikuwa wakimuomba Allah mwaka mzima awaafikie kuweza kuzifikia siku hizi za kheri.

Na wakifikiwa nazo huwa na furaha nyingi, kwa kupata bahati ya kuishi mpaka kuweza kufunga Mwezi wa Ramadhani.

Ndugu Muislamu Mtume Muhammad Swalla Llahu ‘alayhi wasallam Ametufundisha mambo mengi na ibada nyingi ambazo Muislamu anaweza kuzifanya kwa ajili ya kujikurubisha kwa Allah Subuhaanahu wa Taala.

Katika Ibada hizo ni kama ifuatavyo; Kufanya bidii kusali swala ya usiku, na kuwahimiza watu wako nyumbani kuamka kusali pamoja na wewe.

Kusamehewa madhambi yaliyotangulia

Amesema Mtume Swalla Llahu ‘alayhi wasallam): Mwenye kusimama usiku katika mwezi wa Ramadhan kwa Ikhlasi na kutarajia malipo kwa Allah, atasamehewa madhambi yake yaliyotangulia.

Usiku wa ibada

Ilikuwa likifikia kumi la mwisho Mtume alikuwa akigura matandiko yake na akijitahidi kusimama usiku na kuamsha wake zake na familia yake.

Kuzidisha juhudi kutafuta Usiku wa cheo. Usiku huu ni bora kuliko miezi elfu moja, bali ni bora kushinda vitu vyote vilivyomo duniani.

Mwenye kuafikiwa kupata usiku huu basi kwa hakika amefaulu na kupata kheri ya dunia na akhera. Katiak mafundisho ya Mtume Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) kuhusu usiku mtukufu; Ni sunna kuzidisha kusoma Qur’an kwa wingi, kumsifu Allah na kumtukuza na kumsalia Mtume, kutoa sadaka.

Na ni sunna kuomba dua kwa wingi. Bibi Aisha Alimuuliza Mtume: Je niombe dua gani katika usiku huu? Akamuambia sema:

Ewe Mola hakika yako wewe ni mwenye kusamehe waja wako na unapenda kusamehe. Nakuomba unisamehe.