• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 3:25 PM
MAWAIDHA YA KIISLAMU: Tuwachague viongozi waadilifu, wenye kuyapa maslahi ya umma kipaumbele

MAWAIDHA YA KIISLAMU: Tuwachague viongozi waadilifu, wenye kuyapa maslahi ya umma kipaumbele

Na ALI HASSAN

KWA jina la Mwenyezi Mungu mwenye kunemeesha neema kubwa kubwa na neema ndogo ndogo.

Tumejaaliwa leo hii, siku hii kubwa na tukufi, kama ilivyo adana desturi kuangazia utukufu wa dini yetu na kuzipata nasaha za kuimarisha, kuisambaza na kuitangaza dini yetu.

Awali ya yote kama ilivyo kawaida yetu sisi waumini wa dini hii tukufu ya Kiislamu ni kutanguliza kila jambo la kheri kwa kumshukuru, kumtukuza na kumpwekesha Muumba wetu, Allah (SWT), Muumba wa ardhi na mbingu na vyote (viumbe) vilivyomo.

Ama baada ya kumshukuru na kumpwekesha Mola wetu, twachukua uzito wa nafasi hii sawia kumtakia kila la kheri na kumtilia dua na maombi Mtume wetu (SAW) na aila yake na ahali zake.

Leo hii ndugu yangu muumin wa dini hii tukufu ya Kiislamu twajikita kwenye mada ambayo inahusiana na maisha yetu ya kila leo. Leo hii tukiangazia swala la siasa. Swala hili limechangiwa mno na uchaguzi mdogo wa eneo-bunge la Kibra uliomalizika majuzi ambapo Ibrahim Okoth maarufu kama Imran alichaguliwa kuwa mbunge na kuchukua mwahali pa nduguye marehemu Ken Okoth.

Labda ndugu yangu unajiuliza ni kwa nini kuangazia uchaguzi huu, na ni kwa vipi uchaguzi huo unaingiliana na dini yetu au mawaidha ya leo.

Kwanza kabisa, majuzi nikiwa kwenye msikiti wa Jamia, nililipata gumzo na hata nikashiriki kiasi. Gumzo kubwa lilikuwa ni kwa vipi Waislamu ambao wamejisajili kuwa wapiga kura katika eneo la Kibra wangeshirikiana na kuweka kando tofauti zao ili kumpigia kura ‘ndugu yetu’ Mwislamu kwa maana ya Imran.

Miye na wewe ndugu yangu twajua kuwa baadhi ya vigezo vikuu vya kuwachagua viongozi wetu ni kwa kutumia kabila, pesa na ikibidi kwa mbali labda rangi! Subhannallah! Hatuagalii sana maadili, akhlaq, dini, utu na sababu nyinginezo kubwa, hasa hasa DINI!

Kwa kudura zake Maulana Imran alichaguliwa. Swali ambalo yafaa sisi waumini wa dini hii kujiuliza endapo tutaipata sajili rasmi ya Tume Huru ya Uchaguzi Nchini, IEBC, ni kuipiga darubini sajili hiyo na kuona ni Waislamu wangapi walimpigia ndugu Imran kura na kwa sababu gani? Vile vile, kujua ni Waislamu wangapi hawakumchagua ndugu yao huyo na kwa sababu gani.

Ikumbukwe hapa kuwa mbali na Imrani, walikuwepo pia wagombeaji wengine wa kiti hicho ambao pia ni Waislamu na hawakupata kura nyingi vile za kupigiwa mfano. Kwa nini iwe hivyo ilhali eneo hilo la Kibra lina idadi kubwa tu ya Waislamu.

Ndio maana yafaa miye na wewe kujiuliza hapa: “Ni kwa nini sisi wenyewe kwa wenyewe waumini wa dini hii hatuchaguani? Kwa nini tuko radhi kuwachagua watu wa makabila yetu au wenye pesa lakini si ndugu zetu Waislamu? Na je, hao ndugu zetu Waislamu tuliowachagua, wamefanya nini kuutetea umma na dini hii tukufu?

Hebu sasa tuidadavue mada yetu In Shaa Allah.

Uchaguzi huo mdogo yafaa uyafumbue macho yetu sisi waumini wa dini hii.

Tuanze kwa kuulizana – tafadhali nakusishi leo hii tuvumiliane maana maswali yatakuwa mengi (japo asilimia kubwa si ya kukufikirisha ila ni balagha – ni Waislamu wangapi wamechaguliwa katika nyadhfa mbali mbali za siasa tangu hapo. Na ni kwa vipi wameiudumia jamii? Ama wao pia wamo wamo tu katika makundi ya kuwakandamiza wanyonge na kuua Uislamu?

Kukitokea hoja ya umma wa Kiislamu kudunishwa na kukandamizwa, viongozi Waislamu wako kupi? Umma unalishwa sumu kwenye unga, mahindi, mboga, maji, wako kupi viongozi wa kuutetea umma wa Mwenyezi Mungu? Ama wao wamewekwa mifukoni kilichosalia ni kutunisha tu matumbo? Twala moto maskini! Ya Allah (SWT) tusamehe!

Angalia kwenye vyombo vya habari namna viongozi wa Kiislamu, hususa wanawake (maskini) wanavyoropoka na kudensi kwenye majukwaa! Waislamu hasa wanawake tena viongozi. Ya Rabi!

Majuzi nimemsikia Shekhe wetu Ibrahim Lithome akisema kuwa tuwachuje na kuwachagua viongozi waadilifu washika dini. Tutaweza?

In Shaa Allah iwe kheri.

Ijumaa Kareem!

[email protected]

You can share this post!

MAWAIDHA YA KIISLAMU: Baadhi ya njia anazoweza kufanya...

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Nafasi ya hisia katika...

adminleo