MALUMBANO YA USHAIRI: Maisha ni kujaribu
Ikueleme dunia, iwe nanga mgongoni,
Madhila yakufukia, huna hewa mapafuni,
Mawe yakikushukia, yakikuponda mwilini,
Inuka ukajaribu, maisha ni kupambana.
Mawi yakutindikia, uwe mlevi tabani,
Moyoni wariaria, uyumbiwe baharini,
Mawimbi yakubugia, huna tena tumaini,
Inuka ukajaribu, maisha ni kupambana.
Zavuma sana ghasia, zimekushikia kani,
Ghubari likavamia, huna upeo machoni,
kwa kasi wabingiria, huna tena usukani,
Inuka ukajaribu, maisha ni kupambana.
Uchumi wakulemea, na kukutoa makini,
Humudu mafuta taa, kuangaza maishani,
Ubaki wasuasua, kujigotea kizani,
Inuka ukajaribu, maisha ni kupambana.
Mbioni ukijwakwaa, uvingire mtangani,
Matege yakakuvaa, wakakucheka fulani,
Hima inuka jitwaa, usijute aswilani,
Inuka ukajaribu, maisha ni kupambana.
Kinamasi cha kukia, sijisirimbe usoni,
So vema kukiakia, lau wataka sakini,
Kiruke ukikimbia, wenende mbali njiani,
Inuka ukajaribu,maisha ni kupambana.
silie shata kambua, ujilinganisha nani,
Upinde mti; keua, ndo maisha yatakani,
Kaza upate afua, ngoa sio kwa jirani,
Inuka ukajaribu, maisha ni kupambana.
Maisha hayawi waa, lazima kuna tufani,
Jipambanie kung’aa, hiyo ndo yako dhamani,
Usilie wanepua, fanya jambo jiauni,
Inuka ukajaribu, maisha ni kupambana.
E.M.MWANGA MSARIFU
M.D
037, KAKAMEGA
Wanawache
Menibidi kut’ondowa, nduza n’watowe shaka,
Lakutaka kulongowa, asili lalo potoka,
Nyoyo m’taziatuwa, mwalitakalo kutuka,
Mke ana mamlaka, yakumpekesha mume.
N’nenayo si tozuwa, tawajuza ya hakika,
Tarekhe yalivyo kuwa, kale na twalipofika,
Jinsi twalivyo zidiwa, nakuishiya mashaka,
Wake wana mamlaka, kuwapekesha waume.
Babetu aliambiwa, na mkeyo makinika,
Pepo yote mewatiwa, mfanye mnachotaka,
Ila la kukaribiwa, mti adamu komeka,
Hawaa alimsuka, akamlisha mumewe.
Adamu k’aamuriwa, shukani mekhasirika,
Maaduwi mtakuwa, t’endo zitasajiliwa,
Mda m’fupi t’apawa, hatimaye kuondoka,
Hayano yote kutuka, wake husoza waume.
At’ani kujikutuwa, walokotwa kuwateka,
Mitume walizidiwa, kut’ojuwa yalotuka,
Hadi walipo ambiwa, siri ilipo fit’uka,
Vit’invi vyao hakika, nt’ongezi ya waume.
Wenye t’uvu waelewa, la mwendo kwani kumaka,
Hiwa lakwe walijuwa, na yako yafahamika,
Tumwa walimsumbuwa, wakeze wangasifika,
Nonyani msalimika, viti’nvi vya wanawake.
Mume hujamtekuwa, mamiye alomweleka,
Au nduye alozawa, watumbo moja kutoka,
Wawi wakasingiziwa, naye akaafikika,
Adhimu vya aminika, vit’imbi vya wanawake.
Chikomoni n’tatuwa, shikani nalotamka,
Saraha tumezidiwa, ndao yao mamlaka,
Tungataka jizuzuwa, kujitweka madaraka,
N’kilemba chaukoka, metuzidi wanawache.
BASHEIKH AHMAD B
TIMBUKO LA KUZE
TAKAUNGU
Mtaka sicho
Asiyependa hakuna, dhahiri au maficho,
Kuna wanao shibana, wakatoboana macho,
Mahaba nikupendana, kitunze ulicho nacho,
Usiwe mtaka sicho!
Siwe wakudonadona, hukijui utakacho ,
Wa mistari ya vina, wala huna uimbacho,
Waishi kwa kusonona, na hali chako unacho,
Usiwe mtaka sicho!
Una hadhie ubwana, una mambo kochokocho,
Chako usipo kiona, kizuri udumu nacho,
Utapokonywa mchana, ulale hufumbi jicho,
Usiwe mtaka sicho!
Mshukuru Maulana, kwa hicho ulicho nacho,
Ukitunze tena sana, ukilishe ukilacho,
Mahaba nikubebana, usione hicho sicho,
Usiwe mtaka sicho!
Usikuvunge ujana, moyo kautoa kicho,
Dunia ina laana, ina na mambo madhicho,
Imesunduga mabwana, watu walo kuwa nacho,
Usiwe mtaka sicho!
Dengereka wende china, kupata utafutacho,
Kilo kunyima kusona, huli hulali nchicho,
Kiso dosari hakuna, kiwe ndicho ama sicho,
Usiwe mtaka sicho?
Utaharibika jina, wendako chembe unacho,
Kote utajulikana, una gonjwa la kichocho,
Huna mila huna “dina”, n’kipi uzengeacho,
Usiwe mtaka sicho!
Mja sikukakawana, ikiwa chako unacho,
Chombo swafi cha maana, kizuri ujaliwecho,
Chona thamani hakina, wendo wana haja nacho,
Usiwe mtaka sicho!
USTADH MUHAMMAD ABDALLAH (CHETEZO)
“MKINAMLUNDE”
MWANATI WA AFRICA MASHARIKI.
MALINDI, KENYA
Linatuita kaburi
Nakumbusha sihubiri,naomba wenu wasaa,
Simi shekhe si Padiri, simi kamili hataa,
Sote tunatakisiri, kukumbushana twafaa,
Linatuita kaburi, vipi tumejiandaa?
Duniani twasafiri, milele hatutakaa,
Ipo siku itajiri, mauti yatatutwaa,
Roho mbaya na kiburi, kuzimu havitofaa,
Linatuita kaburi, vipi umejiandaa?
Ewe mchukiya kheri, kisalata wa mtaa,
Kidhabu mpenda shari, jema kwako ni kinyaa,
Maovu ukayakiri, ufusuka kukujaa,
Linakuita kaburi, jee.. umejiandaa?
Shetani sikuathiri, ukashikwa na fadhaa,
Mawi ukayakithiri, imani ikachakaa,
Malipo yake ni nari, utageuzwa makaa,
Linatuita kaburi, jee.. tumejiandaa?
Akhera kuna hatari, dunia ukiivaa,
Hakutambuwi tajiri, wala mkata mkaa,
Amali njema ndo siri, ibada ndiyo ridhaa,
Linatuita kaburi, vipi tumejiandaa?
Akrama wakhiyari, ndiyo wenye manufaa,
Wanaozifuata amri, za Mola zinazofaa ,
Kutofanya ya ayari, yake Mungu makataa,
Linatuita kaburi, jee.. tumejiandaa?
Namaliza tafakuri, musinione kinaa,
Kuyafwata ni hiyari, ukiyaafiki twaa,
Ukijipiga kidari, mawaidha kukataa,
Linatuita kaburi, jee.. umejiandaa?
BAMSULEY ABDALLAH BAMSULEY ABDALLAH
SULEIMAN ABDALLAH BAMBAULO
N’NGE MPOLE