MAZINGIRA NA SAYANSI: Chakula hatari kwa afya ya mwili, adui wa mazingira pia
Na LEONARD ONYANGO
IKIWA wewe ni mpenzi wa nyama au vyakula vinginevyo ambavyo vimethibitishwa kusababisha maradhi mwilini, basi unadhuru afya yako pamoja na kuharibu mazingira, wanasayansi wamebainisha.
Wanasayansi hao walisema kuwa vyakula vinavyodhuru afya ni hatari kwa jamii na vinahusika na uharibifu wa mazingira pia.
Vyakula vyenye manufaa makubwa kwa mwili kama vile mboga, nafaka, matunda na kadhalika vinachangia katika uhifadhi wa mazingira, kulingana na watafiti hao.
Watafiti wa Chuo Kikuu cha Minnesota na Chuo Kikuu cha Oxford, wanasema kuwa vyakula vinavyodhuru afya kama vile nyama vinasababisha kuongezeka kwa gesi angani au kuharibu mazingira.
Hii ni mara ya kwanza kwa watafiti kujaribu kuhusisha vyakula vinavyodhuru afya na uwezo wavyo kuharibu mazingira.
Ripoti ya utafiti huo iliyochapishwa katika jarida la Proceedings of the National Academy of Sciences (PNAS), unasema watu wakila vyakula vyenye umuhimu kwa afya watapunguza uharibifu wa mazingira.
“Vyakula tunavyokula vinachangia katika uhifadhi au uharibifu wa mazingira. Utafiti huu umethibitisha wazi kuwa kula vyakula vyenye manufaa mwilini, kutasaidia katika utunzaji wa mazingira. Ulaji wa vyakula vinavyodhuru mwili pia vinaharibu mazingira,” akasema Prof David Tilman wa Chuo Kikuu cha Minnesota ambaye ni mmoja wa watafiti hao.
Wanasayansi hao walitafiti uzalishaji wa aina 15 ya vyakula kwa lengo la kutathmini umuhimu wavyo mwilini na athari zake kwa mazingira.
Matokeo yalionyesha kuwa uzalishaji wa vyakula vilivyo na manufaa makubwa mwilini kama vile nafaka, matunda, mboga, mbegu na kadhalika kunachangia kwa kiasi kidogo mno katika uharibifu wa mazingira.
Watafiti hao pia walibaini kwamba uzalishaji wa vyakula ambavyo vimekuwa vikihusishwa na magonjwa mwilini kama vile nyama (ya ng’ombe, mbuzi, kondoo na nguruwe) kunasababisha uharibifu mkubwa kwa mazingira.
Aidha waligundua kuwa uzalishaji wa samaki ambao wana manufaa makubwa mwilini una madhara kidogo sana kwa mazingira.
Hata hivyo utafiti huo unasema vinywaji na vyakula vyenye sukari nyingi vinadhuru afya ila madhara yake kwa mazingira ni kidogo.
Kulingana na Shirika la Chakula Duniani (FAO), nyama ni chanzo cha vitamini, protini na madini mwilini.
Shirika hilo hata hivyo linaonya kuwa nyama inachangia katika maradhi ya moyo. Aina fulani ya protini inayotokana na nyama huziba mishipa ya kubeba damu kutoka kwenye moyo.
“Nyama (nyekundu) si lazima kwa mwili kwani kuna vyakula mbadala vya kutoa vitamini na madini. Nyama inaweza kuwa na mabaki ya kemikali ambazo zinaweza kudhuru mwili,” linashauri FAO kupitia tovuti yake ya www.fao.org .
Shirika la Afya Duniani (WHO) limeorodhesha nyama ya mbuzi, ng’ombe, nguruwe na kondoo katika Kundi A la vitu vilivyo na uwezo wa kusababisha kansa.
Nyama iliorodheshwa katika kundi hilo, baada ya tafiti zilizofanywa na wanasayansi mbalimbali kuhusisha ulaji wa nyama na kansa.
Inasadikika kuwa nyama- hasa iliyosagwa, husababisha kansa ya matumbo na nyongo.
WHO linakadiria kuwa watu 34,000 hufariki kila mwaka kote duniani kutokana na ulaji wa nyama.
Shirika hilo, hata hivyo, linakiri kwamba hakuna ushahidi wa kutosha unaohusisha maradhi ya saratani na ulaji wa nyama.
Mwezi uliopita, kikosi cha watafiti 14 wakiongozwa na Bradley Johnston, Profesa wa Afya ya Jamii katika Chuo Kikuu cha Dalhousie cha Canada, walitoa ripoti ya utafiti iliyopuuzilia mbali tafiti za hapo awali zilizoonyesha kwamba nyama ni hatari kwa afya.
Wanasayansi hao walishikilia kwamba hakuna ushahidi unaohusisha ulaji wa nyama na kansa au maradhi mengineyo.
Lakini utafiti huo ulishtumiwa vikali na wanasayansi waliowataka watu kupunguza au kujiepusha na nyama.
Watafiti wa vyuo vikuu vya Minnesota na Oxford, wanaonekana kukubaliana na ripoti ya Umoja wa Mataifa (UN) iliyotolewa Agosti, mwaka huu, ambayo ilihimiza watu kula kwa wingi vyakula vinavyotokana na mimea kama njia mojawapo ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Ripoti ya UN ilisema kuwa mifugo, hasa ng’ombe, nguruwe, na mbuzi, huchangia pakubwa katika uzalishaji wa gesi aina ya methane ambayo huchafua hewa na kusababisha joto jingi duniani.
Wanaharakati wa mazingira wamekuwa wakishinikiza serikali kupiga marufuku ulaji wa nyama au kutoza kodi ya juu bidhaa zinazotokana na nyama kama njia mojawapo ya kulinda mazingira.
“Utafiti huu umeonyesha kuwa kuna haja ya kuachana na vyakula vinavyochangia katika uharibifu wa mazingira na kula vyakula vyenye umuhimu mwilini na uhifadhi wa mazingira,” akasema Prof Jason Hill wa Chuo Kikuu cha Minnesota.
“Kwa ufupi ni muhimu kufahamu kuwa vyakula visivyodhuru mwili pia vinafaa kwa mazingira. Vyakula hatari mwilini pia vinadhuru mazingira,” akaongezea.