Makala

MAZINGIRA NA SAYANSI: Moshi wa mafuta ya dizeli unasababisha nimonia – Utafiti

January 28th, 2020 Kusoma ni dakika: 3

Na LEONARD ONYANGO

WAKENYA zaidi ya 15,000 walihusika katika ajali za barabarani mwaka 2019.

Kati yao 3,400 walifariki huku wengine zaidi ya 6,600 wakipata majeraha mabaya.

Lakini imebainika kuwa huenda magari yaliua watu wengi zaidi mwaka 2019 kuliko idadi hiyo iliyotolewa na Mamlaka ya Usalama wa Barabarani (NTSA).

Wanasayansi sasa wanasema kuwa moshi unaotolewa na magari yanayotumia mafuta ya dizeli huenda unachangia katika ongezeko la vifo vinavyosababishwa na homa ya mapafu (nimonia).

Watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Liverpool walibaini kwamba hewa iliyochafuliwa na moshi wa mafuta ya dizeli inaweka watu katika hatari ya kupatwa na maradhi ya Nimonia.

Utafiti huo uliochapishwa katika jarida la Journal of Allergy and Clinical Immunology, unasema kuwa watu wanaopumua hewa iliyo na moshi wa mafuta ya dizeli wanakuwa na uwezekano mkubwa wa kupatwa na nimonia ambayo husababishwa na bakteria wanaojulikana kama Streptococcus pneumonia.

Bakteria hao ndio husababisha maradhi ya nimonia na homa ya uti wa mgongo (meningitis). Magonjwa haya huchangia kwa kiasi kikubwa vifo vya watoto wachanga walio chini ya miaka mitano. Kadhalika, husababisha vifo vya maelfu ya watu wazima kote duniani.

Tangu 2015, maradhi ya nimonia yamekuwa yakiongoza kwa kusababisha idadi kubwa ya vifo humu nchini.

Kulingana na ripoti kuhusu hali ya kiuchumi ya 2018 iliyotolewa na Shirika la Takwimu Nchini (KNBS), maradhi ya nimonia yaliangamiza watu 21,584 mnamo 2017. Idadi ya watu waliofariki kutokana na nimonia ni karibu mara nne kuliko waliofariki kutokana na Ukimwi.

Ugonjwa wa nimonia uliua watu 21,295 na 22,473 katika mwaka wa 2016 na 2015 mtawalia.

Magonjwa mengine yaliyoangamiza idadi kubwa ya watu 2017 ni Malaria ulioua watu 17,553 na kansa ambao uliangamiza watu 16,953.

Mnamo 2018 watu milioni 1.8 walienda hospitalini kutibiwa nimonia na mwaka uliotangulia wa 2017, watu milioni 1.2 walitafuta matibabu ya nimonia.

Takwimu za wizara ya Afya zinaonyesha kuwa watoto 700,000 hutibiwa maradhi ya nimonia kila mwaka.

Lakini jambo la kusikitisha ni kwamba karibu asilimia 25 hufariki kwa sababu huchelewa kupelekwa hospitalini wanapougua maradhi hayo.

Ripoti iliyotolewa na shirika lisilo la serikali la Save the Children mnamo 2017, ilionyesha kuwa vipimo visivyotoa matokeo sahihi na uhaba wa dawa za kukabiliana na bakteria ni miongoni mwa sababu zinazochangia katika ongezeko la vifo vinavyotokana na nimonia.

Ugonjwa huo ukigunduliwa mapema unatibika kwa dawa inayouzwa kwa Sh200.

Chanjo ya kukabiliana na maradhi ya nimonia ilianza kutumika humu nchini mnamo 2011 kwa watoto wa kati ya umri wa wiki sita na 14.

Lakini takwimu za Save the Children zilionyesha kuwa zaidi ya watoto 418,000 wa umri wa miezi 12-23 hawakupewa chanjo hiyo mnamo 2017.

Maafa yanayotokana na nimonia huenda yakaendelea kushuhudiwa humu nchini kwani takwimu za KNBS zinaonyesha kuwa kiwango cha mafuta ya dizeli yanayotumiwa humu nchini kinaongezeka kila mwaka.

Kwa mfano, ripoti ya KNBS ya 2019 inaonyesha kuwa kiwango kilichotumiwa humu nchini kiliongezeka kwa asilimia 4.2 mnamo 2018 ikilinganishwa na 2017.

Kwa mujibu wa KNBS, sekta ya usafiri wa barabarani ndio inaongoza kwa kutumia kiasi kikubwa cha mafuta ya dizeli. Sekta zingine zinazotumia kiasi kikubwa cha mafuta ya dizeli ni ujenzi, usafiri wa reli, uchimbaji wa madini, usafiri wa hewani, kilimo na viwanda.

Kulingana na watafiti wa Chuo Kikuu cha Liverpool, bakteria hao wa Streptococcus pneumonia wanaishi mwilini, haswa kooni na puani, bila kusababisha maradhi.

Lakini bakteria hao hugeuka kuwa hatari iwapo watafika katika sehemu nyinginezo za mwili kama vile kwenye damu na mapafu.Bakteria hao wanapofika kwenye sehemu hizo za mwili huwa hatari na waweza kusababisha kifo.

Maradhi ya nimonia na homa ya uti wa mgongo (meningitis) yasipotibiwa kwa haraka yanaweza kusababisha madhara makubwa mwilini na hata kuua mwathiriwa.

Wanasayansi hao walikuwa wakitafiti ili kujua namna bakteria hao wasiokuwa na madhara husafiri na kuingia kwenye damu na mapafuni.

Watafiti hao walitumia panya kujaribu kubaini jinsi hewa chafu inayotokana na moshi wa dizeli inavyosababisha maradhi ya nimonia.

Wanasayansi hao waligundua kuwa chembechembe zilizomo kwenye moshi wa dizeli hulemea kinga za mwili zinazojulikana kama ‘macrophages’. Kinga hizo huhusika na uuaji wa bakteria na kuondoa uchafu mwilini.

Lakini chembechembe za moshi wa dizeli hufanya kinga hizo za mwili kushindwa kufanya kazi. Hali hiyo hutoa mwanya kwa bakteria hao kuingia kwenye mfumo wa damu na kusafiri hadi kwenye mapafu.

Bakteria hao wanapofika kwenye ubongo, mwathiriwa huwa kwenye hatari ya kuugua homa ya uti wa mgongo.

“Sote tunajua kuwa uchafuzi wa hewa ni hatari kwa afya na hata husababisha vifo kote duniani. Lakini kile ambacho hatukukijua ni kwamba uchafuzi wa hewa kwa moshi wa mafuta ya dizeli kunachangia katika kuenea kwa maradhi ya nimonia,” akasema Profesa Aras Kadioglu wa Chuo Kikuu cha Liverpool.

“Utafiti huu umedhihirisha kuwa kuna haja ya kukabiliana uchafuzi wa hewa ili kuzuia maradhi hatari kama vile nimonia,” akaongezea.

Utafiti huo pia ulisaidia kutegua kitendawili kuhusu idadi kubwa ya watu wanaofariki kutokana na nimonia katika mataifa yaliyo na hewa chafu zaidi ulimwenguni kama vile China.

“Utafiti wetu umebaini kuwa moshi wa dizeli unachangia kusafiri kwa bakteria kutoka kwenye pua na koo hadi kwenye mapafu na kusababisha maradhi ya nimonia,” akasema Rebecca Shears, ambaye pia alihusika katika utafiti huo.