MAZINGIRA NA SAYANSI: Taa za mitaani ni hatari kwa wadudu, utafiti waonyesha
Na LEONARD ONYANGO
HUKU serikali za Kaunti na Kitaifa zikiwa mbioni kuweka taa mitaani kuwezesha Wakenya kufanya biashara zao usiku na mchana na hata kupunguza visa vya uhalifu ambavyo hutekelezwa kwa wingi gizani, wanasayansi sasa wanasema kuwa hazifai.
Wanasayansi wanasema taa hizo za mitaani zinasababisha kufa kwa wadudu na huenda wakatoweka duniani mwishoni mwa karne hii.
Wanasema idadi kubwa ya wadudu hufa karibu na taa hizo na huenda wakaisha duniani mwishoni mwa karne ya 21.
“Tunaamini kwamba taa zinazowaka nje usiku, unyunyiziaji wa kemikali na mabadiliko ya tabianchi yatasababisha kutoweka kwa wadudu duniani,” wakasema watafiti hao wa Chuo Kikuu cha Washington, Amerika.
Wanasayansi hao sasa wanashauri watu kuzima taa zisizo za lazima usiku kwa lengo la kunusuru wadudu ambao wanasema wanatoweka kwa kasi ya kushtua.
Kulingana na Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UN Environment), asilimia 40 ya wadudu wako katika hatari ya kutoweka duniani katika miaka michache ijayo.
“Kasi ya wadudu kutoweka ni mara nane zaidi ya wanyama, samaki na ndege. Takwimu zinaonyesha kuwa wadudu huenda wakatoweka duniani kufikia mwishoni mwa Karne ya 21,” linasema shirika la UN Environment.
Uhaba wa wadudu tayari umeripotiwa katika mataifa ya Ujerumani na Puerto Rico.
“Utafiti wetu umethibitisha kuwa wadudu wanatoweka kwa kasi duniani. Iwapo wadudu wataisha duniani huenda kukawa na shida kubwa,” akasema Brett Seymoure, mtafiti katika Chuo Kikuu cha Washington.
Mnamo Februari 2019 watafiti wa nchini Ujerumani walisema kuwa idadi ya wadudu warukao au watambaao imepungua kwa asilimia 80 katika mataifa ya Ulaya.
Kupungua kwa wadudu hao kumesababisha ndege 400 milioni ambao hula wadudu kufariki katika kipindi cha miaka 30 iliyopita.
Watafiti hao wa Ujerumani walihesabu wadudu katika maeneo mbalimbali nchini humo kati ya 2008 na 2017. Wanasayansi hao pia walihesabu idadi ya viumbe ambao hutegemea wadudu kwa chakula.
Walibaini kwamba wadudu pamoja na viumbe wanaotegemea wadudu kwa chakula walipungua kwa kwa asilimia 40.
Baadhi ya viumbe kama vile vyura, popo, ndege, samaki, nakadhalika, hutegemea pakubwa wadudu kwa chakula.
Kuna mamilioni ya aina za wadudu duniani na wengi wao hawajagunduliwa na wanasayansi.
Watafiti hao wa Chuo Kikuu cha Washington, kupitia ripoti yao iliyochapishwa katika jarida la Biological Conservation, wanasema kuwa baadhi ya wakulima wanatumia taa kuua wadudu katika mashamba yao na huo ni ushahidi tosha kwamba taa ni hatari kwa wadudu.
Baadhi ya wadudu hujikusanya karibu na taa wakidhani kwamba ni mwangaza wa mwezi.
Wavuvi, katika Ziwa Victoria kwa mfano, hutumia taa kuvutia wadudu ambao huleta dagaa (omena). Dagaa wanapokuja kula wadudu hao hunaswa kwa nyavu.
Uchovu na kuliwa
Watafiti wa Chuo Kikuu cha Washington, wanasema asilimia 40 ya wadudu ambao hukusanyika kando ya chanzo cha mwangaza hufariki kabla ya asubuhi kutokana na uchovu au kuliwa.
Watafiti kutoka Uingereza, mwaka jana, walisema kuwa mwangaza wa magari husababisha vifo vya wadudu 100 bilioni kwa mwaka nchini Ujerumani.
Watafiti wanasema kuwa mwangaza wa taa husababisha aina fulani ya wadudu kushindwa kuzaana.
“Baadhi ya wadudu hutumia mwangaza wa jua au mwezi kujua mahali kuna maji kwa ajili ya kutaga mayai, lakini mwangaza wa taa huwafanya kupoteza mwelekeo,” wanasema watafiti hao.
Wanasayansi hao pia walibaini kuwa mwangaza wa taa husababisha baadhi ya wadudu kushindwa kupata chakula hivyo kufaa kwa njaa.
“Kuna ushahidi tele wa kuonyesha kwamba mwangaza wa taa unasababisha kupungua kwa wadudu. Watu sasa wanafaa kuchukua hatua mwafaka ili kuhifadhi wadudu hao ambao wengi wao wana manufaa kwa uzalishaji wa chakula na ukuaji wa mimea,” wanasema watafiti hao.
Utafiti huo wa Chuo cha Washington ni wa kwanza kuhusisha mwangaza wa taa na kuangamia kwa wadudu. Mbali na mwangaza, kemikali zinazonyunyiziwa mashambani zimelaumiwa kwa kusababisha maafa ya mabilioni ya wadudu.