MAZINGIRA NA SAYANSI: Ufugaji wa vipepeo una faida tele
Na MAGDALENE WANJA
LICHA ya kushuhudiwa uharabifu mkubwa wa misitu katika sehemu nyingi nchini, jamii zinazoishi katika eneo la Arabuko-Sokoke katika eneobunge la Malindi zinajikimu kimaisha kutokana uhifadhi wa mazingira.
Katika juhudi za kuhifadhi mazingira na mojawapo ya misitu mikubwa zaidi katika eneo la Pwani, wakazi hao wamefunzwa jinsi ya kuwafuga vipepeo ambao wanauza katika nchi za kigeni.
Mtafiti katika Makavazi ya Kitaifa, Bw Hussein Aden alisema kwamba msitu huo ni makazi ya asilimia 30 ya vipepeo na asilimia 20 ya ndege nchini.
“Kupitia mradi huu ambao husambaza vipepeo katika sehemu mbalimbali ulimwenguni,mradi huu unaleta mapato ya Sh 18 milioni kila mwaka,” alisema Bw Aden.
Mradi huo kwa jina la Kipepeo ulianza mnamo mwaka 1993 ili kuwavuna vipepeo kutoka kwenye msitu na kuwaweka katika mandhari mazuri kuhakikisha wanaongezeka.
Mradi huo wa Kipepeo pia unawawezesha wakazi kuuza asali na nguo zilizotengenezwa kutokana na silk.
Bw Msanzu Karisa ambaye alipoteza mguu wake kutokana na ugonjwa wa matende (Elephantiasis) miaka 10 iliyopita, alisemakuwa amekuwa akipata pato lake kutoka kwa mradi huo.
Bw Karisa alianza kwa kima cha Sh10,000 ambazo alizipangia kwa mradi huo wa kufuga vipepeo.
“Hitaji la vipepeo liliendelea kuongezeka na kufikia sasa, ninajihakikishia angalau pato la Sh100,000 kwa mwezi,” akasema Bw Karisa.
Kipepeo hutaga kati ya mayai 1,000 na 2,000 katika maisha yake na huchukua muda wa kati ya siku tatu na tano mayai hayo kuanguliwa.
Mabuu au pupa huwekwa kwenye miti michanga ambacho ni chakula chao na baada ya majuma mawili, huwekwa kwenye miti mikubwa.
Baada ya wiki nne, wakulima hao hupeleka kwenye kituo cha kuuzia.
Viwavi – watoto wa kipepeo – kwenye kituo hicho husimamiwa na watu waliochaguliwa ambao pia huwatunza kabla ya kutayarishwa ili kuuzwa kwa soko la nje.