Mazingira tulivu ya Kefri Lamu yafananishwa na bustani ya Edeni
NA KALUME KAZUNGU
MANDHARI tulivu na yenye uasilia, ikiwemo miti ya kale na nyasi safi kwenye ofisi za Taasisi ya Utafiti wa Misitu Nchini (KEFRI), tawi la Lamu yamekuwa kivutio cha wengi ambao kila kuchao huzuru eneo hilo kujivinjari.
Ofisi za KEFRI Lamu hupatikana pembezoni mwa mji wa Mokowe.
Unapowasili kwenye taasisi hiyo, kwanza utakaribishwa na lango kuu lililopakwa rangi za aina yake, ikiwemo nyeupe na maandishi ya rangi nyeusi.
Kuta za lango hilo zimejengwa kwa madoido, ikiwemo kutundikwa mawe ya aina yake ilhali sehemu nyingine zikipakwa rangi za kijani, kijani kibivu na kijivu.
Hatua hiyo imeliacha lango hilo kuwa murua na muonekano wake kuiridhisha nafsi si haba kwa yeyote anayeingia kwenye taasisi hiyo.
Punde unapofika ndani, mandhari ya KEFRI huzidi kunogeshwa na kuwa maridadi hata zaidi, hasa kutokana na mazingira sufufu ya rangi ya kijani kibichi iliyokolezwa utadhani uko kwenye Bustani ya Edeni.
Edeni ni bustani inayotajwa au taswira yake kuchorwa katika Kitabu cha Mwanzo cha Biblia.
Yaani wengi wamekuwa wakiulinganisha umaridadi wa KEFRI na ule wa Bustani ya Edeni ambayo imefasiriwa kuwa nzuri, iliyopambwa na Mungu mwenyewe na kisha kuwaweka binadamu wa kwanza, yaani Adamu na Hawa kuilinda baada ya uumbaji.
Majengo ya ndani ya taasisi ya KEFRI mjini Mokowe pia yamepangwa katika hali nzuri, kushabihiana na kuingiliana vyema na muonekano wa jumla wa eneo hilo, hivyo kupendeza kabisa kwa macho.
Ni kutokana na hali hiyo ambapo watu wa tabaka zote, ikiwemo viongozi, maafisa wa utawala, mashirika makubwamakubwa ya mazingira na kijamii, yamekuwa yakiandaa mikutano na makongamano mbalimbali kwenye ukumbi wa taasisi hiyo.
Ili kulinganisha au kuoanisha hali asili au mazingira ya kimsitumsitu ya KEFRI, ukumbi wa mikutano pale umebandikwa jina la miti asilia ya Lamu mlangoni ambapo unaitwa ‘Mkoko Hall.’
Baadhi ya vyumba vipatikanavyo kwenye majengo ya KEFRI pia yamebandikwa majina ya miti, ikiwemo Mbambakofi, Mwangati, Mkelekele, Msaji.
Miti hiyo hufanya vyema katika kukua kwake kwenye mazingira ya Lamu na inafahamika kwa kuwa na mbao ngumu.
Vyumba vingine vilivyobandikwa majina ya miti ni Mvinje, Mchikichi, Mbuyu na Mkoma.
Miongoni mwa watu mashuhuri ambao tayari wamekuwa wakinaswa na hadhi na fahari ya ofisi za KEFRI, hivyo kuchagua kuandaa mikutano kwenye ukumbi wake ni Gavana wa Lamu, Issa Timamy, Wabunge, Maseneta, Mawaziri wa serikali kuu, na madiwani.
Maafisa wa Utawala wanaowakilisha serikali kuu, ikiwemo Kamishna wa Kaunti ya Lamu, Manaibu wao, machifu na wazee wa mitaa pia wamekuwa wakiandaa mikutano yao kwenye ukumbi wa KEFRI ilmradi wafurahie mandhari hayo ya kuvutia na kuuburudisha moyo.
Isitoshe, maafisa wa mashirika ya kijamii na yale ya kushughulikia uhifadhi wa mazingira pia hayajaachwa nyuma kwani kila mara wamekuwa wakikimbilia kuchagua kuandaa mikutano yao kwenye eneo hilo la KEFRI.
Katika mahojiano na na Taifa Jumapili ofisini mwake Jumatano, Afisa Msimamizi wa KEFRI tawi la Lamu ambaye pia ni Mwanasayansi Mtafiti wa kituo hicho, Bw Henry Komu alisema kama taasisi, wao wako na vile wanajitahidi kudhibiti mwonekano wa afisi au vituo vyao vya utafiti si Lamu tu bali Kenya yote.
“Ikumbukwe KEFRI jukumu lake kuu ni kutafiti misitu au miti na kuhakikisha elimu hiyo inasambazwa kwa jamii ili kuendelea kuboresha mazingira. Na hii ndiyo sababu tukaafikia kwamba ofisi zetu zilingane kabisa na majukumu tunayotekeleza kama KEFRI. Ofisi zetu zote nchini ziko na mfumo mmoja,” akasema Bw Komu.
Bw Komu alifafanua kuwa miti mingi waliyopanda kwenye taasisi yao ni ya asili na iliyofanyiwa utafiti na kugundulika kuwa inafanya vyema kwenye mazingira ya Lamu.
“Ukifika hapa kama mteja wetu huondoki bure. Miti tuliyopanda tumeiwekea maelezo kuihusu na pia jinsi anayetaka kupanda atatekeleza jukumu hilo na kwa wakati gani. Yaani unahudhuria mikutano yako au unakodi chumba cha kulala hapa na punde unapoondoka unakuwa kabisa na ukwasi wa elimu kuihusu miti na misitu,” akasema Bw Komu.
Bw Komu aliwakaribisha wote wanaotaka kuzuru KEFRI kufanya hivyo akiwahakikishia kwamba ziara zao hazitakuwa kazi bure.
Anasema ofisi yake imekuwa ikitoa hamasa kwa wanaofika hapo na kuulizia masuala ya upanzi na uhifadhi wa miti.
“Ukifika hapa tutakuelimisha kuhusu ni lipi la kufanya. Tutakupendekezea miche mwafaka ya kupanda Lamu au kwenye makazi yako. Pia tutakupa miche uende ukajipandie na kukuza,” akasema Bw Komu.
Karisa Luwali, ambaye ni mwanamazingira wa Shirika lavuguvugu la uhifadhi la Lamu Green Movement, alisifu mandhari ya KEFRI, akisema yamejaa kwasi mwingi wa elimu kuhusu uhifadhi.
“Tunapohudhuria makongamano, hasa yale yanayohusu mazingira hapa, watu huwa wanapata msukumo wa kutunza mazingira yao na kuyafanya kuwa ya hadhi hasa kutokana na kile wanachojionea hapa. Miti na nyasi zimepamba muonekano wa hapa na kuleta hewa safi,” akasema Bw Luwali.
Kwa upande wake, Mkuu Msimamizi wa Uhifadhi kwenye Shirika la Huduma za Misitu Nchini (KFS), kaunti ya Lamu, Bw Samuel Lodiro, anawahimiza watu kuiga taswira ya mandhari yaliyoko kwenye taasisi ya KEFRI, akishikilia kuwa endapo watafaulu kufanya hivyo, Lamu itakuwa eneo bora la kuishi.