Mazishi: Waluo waanza kukumbatia mabadiliko
JAMII ya Waluo imekuwa ikishuhudia mabadiliko makubwa kuhusu utaratibu wa mazishi, huku familia nyingi zikianza kutoka kwa mila za jadi na kuanza kutenga sehemu maalum za makaburi ndani ya boma au kutumia makaburi ya umma.
Mabadiliko haya yamechochewa na sababu mbalimbali, zikiwemo msongamano wa watu, upungufu wa ardhi, maisha ya mijini na mitazamo mipya ya kiimani na kijamii.
Hii ni kinyume na desturi za jadi ambapo wazee wa ukoo waliamua mahali pa kumzika marehemu kulingana na jinsia, hali ya ndoa na umri.
Kwa mfano, wanaume huzikwa upande wa kulia wa boma wakielekea ndani, wanawake upande wa kushoto, huku wasichana ambao hawajaolewa wakizikwa karibu na ua bomani.
Hata hivyo, familia nyingi sasa zinasema mila hizo si lazima kufuatwa, hasa ikiwa marehemu hakuwa akiziamini.
Bw David Omore kutoka Kakrao, Migori, alisema familia yake ilizika baba yao kwenye sehemu ya makaburi ya familia kama alivyoagiza kabla ya kufa, licha ya upinzani kutoka kwa wazee wa ukoo.
“Baba yetu hakuamini mila hizo. Tuliheshimu mapenzi yake,” alisema.
Kwa upande wake, Ker Odungi Randa, Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Jamii ya Waluo, anakiri kuwa hali inabadilika.
“Tunaishi katika dunia ya kisasa. Ardhi inazidi kupungua. Tunahimiza familia kutenga sehemu maalum za kuzika wapendwa wao badala ya kueneza makaburi kila sehemu ya boma,” alisema.
Katika Kaunti ya Kisumu, serikali ya kaunti imepiga marufuku mazishi katika boma zilizopo ndani ya jiji.
Mazishi sasa yanaruhusiwa tu katika makaburi ya umma au vituo rasmi vya kuchomea miili.
“Tunaelewa thamani ya kumbukumbu katika utamaduni wa Waluo, lakini sasa jiji linapanuka na baadhi ya maeneo ya makazi yanageuka ya kibiashara,” alisema Meneja wa Jiji la Kisumu, Bw Abala Wanga.
Wengine kama mwanahistoria Levin Odhiambo Opiyo wanaunga mkono wazo la makaburi rasmi.
“Awali niliona mazishi makaburini kama njia ya kuwasahau marehemu, lakini sasa naona ni njia ya kudumisha kumbukumbu kwa vizazi vijavyo,” aliandika.
“Tofauti na boma, makaburi hudumu na huruhusu vizazi vijavyo kuwaenzi waliotangulia,” aliandika.
Aliongeza kuwa mara nyingi makaburi ya kifamilia hupotea kwa sababu ya mabadiliko ya umiliki wa ardhi au ujenzi wa nyumba mpya.
“Makaburi yaliyopangwa vyema, yenye bustani na mandhari ya utulivu, hutoa nafasi ya faraja na tafakari kwa waliobaki,” alisema.
Hata hivyo, pamoja na mabadiliko haya, baadhi ya familia bado zinasisitiza umuhimu wa mila na kuamini kuwa mazishi nyumbani huendeleza uhusiano wa kiroho kati ya walio hai na waliotangulia.