Akili MaliMakala

Mazoea ya serikali kukopa yanavyolemaza ukuaji wa sekta ya kibinafsi

Na BENSON MATHEKA April 9th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

BIASHARA za Kenya zinakabiliwa na changamoto kubwa kupata mikopo kutokana na viwango vya juu vya riba, hali ambayo inaweza kuzidi kuwa mbaya zaidi kutokana na utashi wa serikali kuendelea kukopa ndani ya nchi.

Haya yanajiri wakati ambao Hazina ya Kitaifa inapanga kuongeza kiwango cha mikopo kutoka kwa benki za humu nchini katika miaka ijayo, jambo ambalo litazidi kusukuma sekta ya kibinafsi nje ya soko la mikopo.

Waziri wa Hazina ya Kitaifa, John Mbadi, alisema serikali imepanga kuongeza upatikanaji wa mikopo huku ikijitahidi kupunguza viwango vya riba.

Hatua hii inajiri wakati ambao ukuaji wa mikopo kwa sekta ya kibinafsi unapungua.

Wanauchumi wanasema hatua hii ya serikali ina hatari ya kusukuma sekta ya kibinafsi nje ya soko la mikopo.

“Benki zitapendelea kukopesha serikali kwa sababu inaonekana kuwa salama, jambo ambalo litapelekea viwango vya riba kupanda na kufanya biashara za kibinafsi kupata ugumu wa kupata mikopo,” alisema mchumi Francis Wahito.

Anasema upatikanaji wa mikopo umekuwa mgumu kwa sekta ya kibinafsi kutokana na viwango vya juu vya riba.

Serikali inaendelea kukopa na hivyo kuisukuma nje sekta ya kibinafsi hatua ambayo inadumaza ukuaji wa uchumi.

Shirika la kimataifa la kukadiria viwango vya mikopo, Moody’s, lilibadilisha matarajio ya Kenya kutoka “hasi” hadi “chanya” kutokana na uwezekano wa kupungua kwa hatari katika kulipa madeni na kuimarika kwa uwezo wa kumudu deni.

Ripoti ya Moody’s imeonyesha kuwa iwapo serikali itasimamia vizuri mpango wake wa kudhibiti matumizi, gharama ya mikopo ya ndani itapungua na hatimaye kufungua njia za ufadhili kutoka nje.

“Kile kilichobadilika ni matarajio. Matarajio yanahusu kile kinachotarajiwa kutokea siku zijazo,” uchambuzi kutoka Taasisi ya Fedha za Umma ulionyesha.

“Alama yetu ya mkopo kama nchi haijaimarika sana, na bado tuko kwenye hatari ya kukopa kwa gharama kubwa.”

Kwa mujibu wa mkakati wa usimamizi wa deni wa muda wa kati 2025–2028, Hazina ya Kitaifa inapanga kuongeza kiwango cha mikopo ya ndani hadi asilimia 75 na kupunguza mikopo kutoka nje hadi asilimia 25.

Kwa sasa, wakopeshaji wa ndani na nje wanagawana deni la umma, ambalo lilikuwa Sh10.93 trilioni kufikia Desemba 2024, ambapo Sh5.87 trilioni zilikopwa ndani ya nchi na Sh5.06 trilioni ni deni la nje.