Mbinu maalum kuzalisha miche bora ya avokado za Hass
MAPARACHICHI maarufu kama avokado, yanaanza kushabikiwa nchini kutokana na soko lake lenye ushindani mkuu ng’ambo.
Yamegeuka kuwa Dhahabu ya Kijani nchini Kenya, idadi ya wakulima wanaoyazalisha ikiongezeka.
Licha ushindani mkuu masoko ya ndani kwa ndani na ughaibuni, wakulima waliokumbatia matunda haya wanapaswa kuwa na ufahamu jinsi ya kuyazalisha kitaalamu.
Hilo linashikiniza kuhoji; Ni siri ipi mkulima anapaswa kutumia kunogesha mazao?
Katika Kaunti ya Trans Nzoia, KTL Farming Ltd, kampuni inayozalisha miche iliyoimarishwa ya avokado imeibuka na mbinu maalum kuhakikisha mkulima anapata mazao bora.
Ikiwa inaendeleza shughuli hiyo eneo la Kitale, kampuni hiyo inayokuza miche aina ya Hass hutibu mbegu na vipandio (udongo).
“Ufanisi wa mimea yoyote ile, kando na shamba lenye rutuba na chanzo cha maji ya kutosha, mbegu au miche iliyoafikia ubora ndiyo nguzo kuu,” anasema Damaris Omuka, Meneja wa shamba la KTL Farming Ltd.
Mbali na wadudu waharibifu, magonjwa ya mimea kama vile root rot, ni kati ya yanayohangaisha kilimo cha maparachichi.
Damaris anasema siri ni kukabiliana na kero kama hiyo kuanzia kwa udongo unaotumika kukuza miche.
Ndiposa kampuni hiyo imeibuka na mbinu kuhakikisha magonjwa hayasambai.
“Aghalabu, magonjwa ya mimea husambaa kupitia udongo na miche,” Damaris anadokeza.
Root rot, kwa mfano husababishwa na viini hatari vinavyojulikana kama Phytophthora cinnamomi.
Kwenye mahojiano ya kipekee na Akilimali katika shamba la KTL Farming Ltd Kitale, Damaris alifichua kwamba huanza kwa kukagua mbegu kuzalisha miche.
“Mbegu, hutumia za maparachichi asilia na huziosha vizuri kabla ya kuzipanda,” akaelezea.
Aidha, huoshwa kwa majimoto yenye nyuzijoto 49 hadi 50 (°C), kwa karibu dakika 30.
Hata hivyo, mkulima anatahadharishwa dhidi ya kutumia maji yaliyopita nyuzijoto 52 (°C), ili kuepuka kuharibu mbegu.
Damari alisema, mbegu na udongo, pia hutibiwa.
Udongo huchomwa ili kuua viini vya magonjwa na wadudu.
Kemikali kama vile Methyl bromide, gypsum na malighafi asilia kupanda hutumika.
Kampuni hiyo ina eneo maalum la shughuli hiyo.
“Mbegu asilia zinapokua, huzipandikiza (grafting) kwa kutumia matawi (zion) ya maparachichi yaliyoboreshwa,” Damaris akasema.
Wana wakulima wa kipekee wanaowasambazia, na alidokeza kwamba wamefunza baadhi ya wafanyakazi kutekeleza shughuli hiyo.
Udongo unaotumika kukuza miche, huinuliwa kitaluni na eneo hilo lina kanuni kuingia.
“Si kila mtu anayeingia kwenye kiunga cha kuzalisha miche. Langoni, yapo maji yaliyotibiwa na anayeingia sharti aloweshe makanyagio ya viatu kuua viini,” anafafanua.
Maji yanayotumika kunyunyizia mimea hiyo changa, Damaris anasisitiza sharti yawe safi.
Ni mbinu ya kipekee kupata miche bora waliyofumbuliwa macho kupitia mradi wa Kenya Crops and Dairy Market Systems (KCDMS) uliofadhiliwa na United States Agency for International Development (USAID), uliokamilika 2023.
Mpango huo ulilenga kupiga jeki wakulima kuongeza uzalishaji wa chakula nchini.
“Tulianza kunufaika na mradi huo 2022, na miaka miwili baadaye, uzalishaji wetu wa miche umeongezeka mara dufu,” Damaris anasema.
Kwa sasa, wanahudumia zaidi ya wakulima 3, 000 Magharibi mwa Kenya, 2, 750 wakitoka Kaunti ya Bungoma.
Kiunga cha KTL Farming Ltd kikiwa kimebuni nafasi za ajira kwa vijana 27, kwa awamu moja hupandikiza miche isiyopungua 75, 000.
Inachukua karibu miezi kumi kupata mche wa Hass uliopandikizwa.