Mbinu ya kisasa kudumisha muda wa asali
KENYA huagiza kwa kiasi kikubwa asali kutoka nchi jirani kama vile Tanzania, South Sudan, na Ethiopia.
Uagizaji huu unaendelea licha ya Kenya kuwa na maeneo mengi yenye uwezo kufuga nyuki.
Asali, ikiwa mojawapo ya bidhaa zinazotokana na ufugaji nyuki zenye ushindani mkuu sokoni, Waiyaki Way Beekeepers, kampuni ya kufuga nyuki, huongeza thamani asali yake ili kudumu mrefu.

Awali, kulingana na Erick Kamau ambaye ni Afisa Mkuu Mtendaji, walikuwa wakitumia mbinu za kitambo kusindika asali, hatua zilizochangia upotevu mkubwa.
Huchoma asali kwa njia isiyo ya moja kwa moja, ili kuitenganisha na nta, nyuki wanaosalia na uchafu mwingine.
Aidha, wamekumbatia matumizi ya teknolojia ya kisasa kuchoma asali (pasteurizer), na pia wana kifaa cha kukama asali na kuchuja (honey press).

“Ni teknolojia zinazopunguza upotevu wa asali na kuokoa muda,” Kamau anasema.
Asali huchomwa kwa njia isiyo ya moja kwa moja kwa kutumia maji kwenye pasteurizer, kwa kiwango cha nyuzijoto kati ya 45 hadi 50 (°C).
Baada ya kurina asali, huhifadhiwa kwenye mitungi kabla ya kuchomwa na kuwekwa kwenye matangi ya baridi.

“Kwenye matangi baridi, hukaa siku tatu au nne ili asali itengane na nyuki, nta na uchafu mwingineo,” Philip Muchemi, Mkurugenzi Mkuu Waiyaki Way Beekeepers anaelezea.
Uchafu unaojitokeza hutolewa kwa mikono, kisha asali inapakiwa tayari kuingia sokoni.
Kamau anasema muhimu ni kukagua mizinga mara kwa mara, akisisitiza kwamba asali iliyo tayari kurinwa mazega (combs) lazima yawe yamefunika bidhaa hiyo kwa zaidi ya asilimia 80.
