Mbona mapasta huwabaka waumini?
NA WANGU KANURI
BAADHI ya wazazi wamejipata wakijutia mwenendo wa kukosa kuwasikiza watoto wao, hata katika masuala yanayotishia usalama wa wanao.
Mapuuza hayo yamesababisha visa kadhaa vya kukera kushuhudiwa huku watoto wakikandamizwa haswa kihisia na kudhulumiwa kimapenzi. Aghalabu, wazazi wengi huamini kuwa njia yao ni bora kiasi cha kwamba wanapuuza ushauri kutoka kwa watoto wao.
Kisa cha hivi karibuni kilichotia saini ukweli huu kilitokea katika Kaunti ya Migori, ambapo pasta mmoja alitiwa mbaroni kwa kumdhulumu kimapenzi msichana mwenye umri wa miaka 14.
Bi Centrine Wekesa, ambaye ni mama wa watoto watatu aliambia Taifa Leo Dijitali kuwa kama mzazi hawezi kubali jambo ambalo mtoto amelikataa kabla hajamweleza mbona amelikataa.
“Isitoshe, mara kwa mara sisi kama wazazi huona kama mtoto anataka tu kukiuka amri uliompa kwa hivyo ujapokuwa na mazoea ya kumsikiza akikataa jambo lolote lile basi utakuwa unalea mtoto mkaidi. Ijulikane kuwa si eti tunakataa kuwasikiza watoto wetu wakikataa kufanya tuliloagiza bali watoto hawa hawatupi sababu za kutosha za kukataa tunachotaka,” Bi Wekesa akaungama.
Msichana huyo hapo awali alikuwa amekataa kuandamana na pasta huyo wa Migori hadi kanisani lakini wazazi wake wakamlazimisha.
Msichana huyo aliishia kubakwa katika jumba moja mle kanisani na alipomuuliza pasta ni nini kiliendela, mchungaji huyo alisema kuwa alikuwa anamtoa vitu ambavyo vilikuwa vinamuumiza tumboni.
Tendo hilo lilijulikana wakati ambapo msichana huyo aliwaandikia wazazi wake barua ya kujitia kitanzi huku akiwalaumu kwa kubakwa kwake.
“Pahala kama kanisa ni pahala patakatifu na mimi kama mzazi nijapomweleza mtoto wangu aende mahali kama hapo kisha akatae, hiyo ni ukaidi kwa kuwa nikipiga darubini siku zake za usoni hatakuwa mtoto mwenye maadili ya Kikristu na singemtakia hayo. Isitoshe, wengi wa wazazi huwalea wana wao sawa sawa na kile walichokiona wazazi wao wakifanya.
“Hamna jambo geni lipo kwenye uzazi na kama mzazi yote niyafanyayo kwa mtoto wangu huwa ili awe bora, mtu wa maana nchini na katika jamii ajapokua. Isitoshe, kukubali kile mtoto anakataa pasi sababu murua ni kumfunza mtoto huyo kuwa kile atakachokataa ni sawa hamna ubishi na huko si kumlea mtoto vyema,” Matthew Korir ambaye ni mmiliki wa duka mtaani Daystar, Athi River alieleza Taifa Leo Dijitali.
Lakini je, mbona wachungaji siku hizi wanawadhulumu wasichana wapevu? Swali hili linazonga akili za wengi huku mchungaji Fredrick Ogore wa kanisa la Hearts Ablaze Kitengela anasema kuwa mchungaji yeyote anayemdhulumu mshirika wake kimapenzi ni mchungaji ambaye hana yeyote anayemwelekeza.
“Aghalabu kukosa mchungaji mwingine anayemwelekeza na kumweleza anayokumbana nayo humfanya afanye lolote bila kuwazia. Isitoshe, mchungaji ambaye hakufunzwa kuhusu maadili licha ya kufunzwa kuhusu uhubiri hukosa msimamo imara katika huduma na kuondokea kuwabaka washirika wake,” anasema.
Anaongeza kuwa wengine huwa wamedorora kitabia huku kila mshirika haswa wa jinsia ya kike akiwa kama windo kwake. Pia washirika wengine huvalia mavazi yanayosisimua ari ya uasherati ndani ya mchungaji ambaye hana maadili ndiposa akaondokea kuwabaka.
“Mwishowe, mchungaji anayembaka mshirika wake anaweza kuwa amenyimwa ngono na mke wake. Hii humfanya kutosheleza kiu hiki na wengine bila hiari yao,” anaeleza.