MBURU: Lazima maafisa wa serikali watii sheria za trafiki
Na PETER MBURU
WIKI hii ilianza kwa mambo mengi hasa siasa kama kawaida ya Kenya, lakini kuna kisa ambacho kilivutia Wakenya wengi.
Mwanaharakati Boniface Mwangi alipokuwa katika barabara moja jijini Nairobi alikutana na msafara wa magari matatu yanayoaminika kuwa ya afisa mashuhuri serikalini, yakiwa yanaendeshwa katika upande mbaya wa barabara.
Ijapokuwa magari mengine katika barabara hiyo yalikuwa yakiondokea yale ya ‘mkubwa’ kuyapa nafasi, Bw Mwangi alidinda na kuwazomea kwa kuvunja sheria.
“Kwanini mnaendeshea magari katika upande mbaya wa barabara? Siwaondokei, fuateni sheria,” mwanaharakati huyo akawaambia, wakati mwanamume aliyetoka katika gari moja la msafara huyo akijaribu kumshurutisha awape nafasi.
Mwanaharakati huyo alikuwa jasiri na akakataa hadi wakaamua kujiendea zao.
Watu mashuhuri, hasa wanasiasa na maafisa wa serikali wamekuwa na hulka ya kuvunja sheria barabarani wanapojaribu kukwepa misongamano, wakitumia taa ama sauti kama zinazotumiwa na ambulensi na magari ya polisi, ili wasafiri haraka.
Hata hivyo, huwa wanafanya hivi kinyume na sheria, kwani kuna magari mahususi ambayo yanaruhusiwa kuendeshea upande mbaya wa barabara.
Kinaya ni kuwa wengi wa wanaofanya tabia hii ni viongozi ambao wana jukumu la kufanya mabadiliko ili kumaliza misongamano ya magari, lakini hawajafanya hivyo.
Hivyo, hatua ya Bw Mwangi kuzuia magari hayo ilikuwa ishara nzuri kwa maafisa wa serikali ambao wamekuwa na tabia hiyo, kuwa pia wao ni binadamu kama wengine na waache kujiona wa maana.
Vilevile, ni kinaya kikubwa kuwa maafisa wanaofaa kutoa mfano bora kwa wananchi kuhusu kutii sheria za trafiki ili kuzuia ajali barabarani ndio kipau mbele kuzivunja.
Ni majuzi tu ambapo mtoto wa shule ya msingi aliuawa na magari ya msafara wa Naibu Rais William Ruto, baada ya kugongwa.
Fauka ya hayo, magari ya maafisa wakuu serikalini na viongozi yanajulikana kwa kuwahangaisha watumizi wa barabara, hasa wanapokosa kupewa nafasi waendeshe kwa kasi kukiwa na misongamano.
Ni aibu kubwa wakati mtu amepewa kazi kusuluhisha changamoto fulani, kisha anaposhindwa anatafuta njia ya mkato kujisaidia yeye, na kuacha waliomwajiri wakiteseka. Hali inayoshuhudiwa katika barabara zetu si tofauti.
Maafisa wa serikali wafuate sheria za trafiki kama watu wengine, ama waboreshe barabara na kurahisishia watu wote kwani hakuna asiyetaka kutumia muda mfupi barabarani.