MBURU: Tusaidie kwa nia ya kufaa wengine, sio kujipatia sifa
Na PETER MBURU
Unapoamua kusaidia wenzako wakati kama huu wa kusherehekea na kukumbukana kwa wasiojaliwa, ni vyema uweke nia yako wazi kwa watu na ndani ya nafsi yako.
Msimu huu wa Krismasi, watu wengi wanamiminika katika vituo wanapoishi watoto mayatima, wagonjwa na hata watu wengine wasio na uwezo wa kifedha kufurahia pamoja nao.
Kwa kila hali, hili ni jambo la kufurahiwa na kuigwa na wote katika jamii kwani kutoa ni moyo na ni baraka kwa anayesaidia. Hii ni kwa kuwa haina maana kula ukasaza wakati jirani yako analala njaa, kwa kukosa.
Vilevile, ni vyema kukuza kizazi cha watoto wanaothamini utu na kutoa na kuwafunza maadili mema ya kijamii na kuwa Mungu hubariki zaidi yule anayetoa.
Hata hivyo, kama jamii sharti tutofautishe kutoa kwa nia ya kusaidia na kwa watu wengine walio na malengo ya kibinafsi.
Ni vyema kulaani tabia fulani ambazo zinaibuka miongoni mwa watu, ambapo wengi wanatumia fursa hizi kujigamba na kujitafutia sifa za kibinafsi wanapowasaidia wengine, badala ya kufuata lengo la kimsingi la kusaidia.
Ikiwa mtu ameamua kusaidia mwingine asiyejiweza, jambo bora zaidi ni lengo la kusaidia kusalia kuwa hivyo tu. Endapo wewe utaenda kumsaidia yatima, mjane, mzee ama mgonjwa kisha kutumia muda mrefu kujigamba mitandaoni na kwenye mikutano namna ulivyomfaa, basi lengo lako la kusaidia halitakuwa la kweli.
Miaka ya hivi karibuni tabia imeibuka katika jamii ambapo wafanyabiashara, mashirika ama wanasiasa wanajitokeza kusaidia vikundi mbalimbali vya watu walio na mahitaji ya aina aina, lakini baadaye ukitazama namna wanavyoimba walivyosaidia utasalia kushangaa ikiwa lengo lilikuwa kusaidia ama kujionyesha walisaidia.
Hali hiyo haijakuwa tofauti msimu huu wa Krismasi kwani watu wengi wamejaa kwenye mitandao ya kijamii kama Facebook, Twitter, Whatsapp na Instagram wakichapisha picha za namna wamepeana misaada kwa masikini, wagonjwa ama watu wengine.
Wengine hata wanaendelea kutoa nambari za simu na kuwataka wasamaria wema kuchanga pesa kwa ajili ya kuwasaidia kuendeleza kazi hiyo.
Haipingiki kuwa hakuna shida ya kusema unaposaidia mtu. Lakini inatia hofu wakati licha ya msaada wako ambao wakati mwingine hata utamfaa msaidiwa wako kwa wakati huo uliopo hapo tu, wewe unajigamba mbele ya watu kiwango hata unaweza kumfanya mtu mwingine aliyekuwa na nia ya kumsaidia mtu huyo zaidi kudhani tayari alisaidika na hana tatizo tena.
Ni vyema Wakenya tuanze kuwa wakweli kwa nafsi zetu na hata mbele ya Mungu na kuwacha kutumia nafasi kuwa tuna kidogo kuwakejeli kivitendo wasio nacho.
Ukiamua kusaidia, saidia bila kujali ikiwa kuna mtu anayekuona au la. Ikiwa lengo lako ni kuonekana kuwa unasaidia ndipo usifiwe, lengo lako ni la kibinafsi na halifaidi jamii.
Lakini ikiwa una nafasi ya kutafuta misaada zaidi kwa kuonyesha watu wenye matatizo, itakuwa vyema kufanya hivyo.
Mwisho, wazazi wakuze ndani ya watoto wao maadili ya utu na moyo wa kusaidia.