• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 10:08 PM
MBWEMBWE: Ukwasi wa Sergio utagharimia karo vyuoni Kenya kwa miezi 6

MBWEMBWE: Ukwasi wa Sergio utagharimia karo vyuoni Kenya kwa miezi 6

Na CHRIS ADUNGO

SERGIO Ramos Garcia, 34, ni difenda matata raia wa Uhispania ambaye kwa sasa ni tegemeo kubwa katika safu ya ulinzi kambini mwa miamba wa soka ya bara Ulaya na Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga), Real Madrid.

Ramos kwa sasa ndiye nahodha wa timu ya taifa ya Uhispania na Real ambao ni mabingwa mara 13 wa Klabu Bingwa Ulaya (UEFA).

Yeye ni miongoni mwa walinzi ambao wanachukuliwa kuwa bora na wakamilifu zaidi katika ulimwengu wa soka ya sasa kwani pia ana uwezo wa kutitiga nyavu za wapinzani kwa kichwa na kupitia penalti.

Utajiri

Soka anayoipiga Ramos nchini Uhispania imechangia pakubwa utajiri wake ambao unamweka katika nafasi ya 26 katika orodha ya wanasoka 100 tajiri zaidi ulimwenguni. Thamani ya mali yake inakadiriwa kufikia Sh6.8 bilioni, pesa zinazotosha kulipia wanafunzi wote wa vyuo vikuu karo yao kwa angalau miezi sita baada ya serikali kutengea Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HELB) Sh12 bilioni mwaka huu.

Kiini kikubwa cha utajiri wa Ramos ni mshahara wa Sh24m aliokuwa akipokezwa kwa wiki na Sevilla kabla ya Real kuzinyakua huduma zake kwa ahadi ya Sh29 milioni kila juma kutokana na huduma anazozitoa kwa sasa uwanjani Santiago Bernabeu.

Malipo hayo ni kiasi cha pesa zinazomweka Ramos katika kikoa kimoja na Luka Modric, Karim Benzema, Marcelo, Isco, Luka Jovic na Toni Kroos; kundi la pili la nyota wanaodumishwa kwa gharama kubwa zaidi na Real baada ya kiungo wa zamani wa Chelsea, Eden Hazard.

Mbali na mshahara huo mkubwa, Ramos hujirinia pia fedha za ziada kutokana na marupurupu na bonasi za kushinda mechi akivalia jezi za wafalme hao wa jiji la Madrid na timu ya taifa ya Uhispania iliyomwaminia unahodha mnamo 2016.

Kwa pamoja na Modric, Diego Godin na Danielle De Rossi, Ramos pia ni balozi wa kutangaza bidhaa za kampuni za Electronic Arts (EA Sports) ambayo humkabidhi takriban Sh35 milioni kila mwezi.

Aidha, anashirikiana na Steven Gerrard, Michael Ballack na David Beckham kuwa mabalozi wa mauzo ya kampuni ya Adidas ambayo humpokeza kitita cha Sh220 milioni kwa mwaka.

Magari

Ramos anamiliki magari ya kifahari ambayo ni pamoja na Audi R8, Bentley Continental GT, Ferrari 458 Spider, Range RoverEvoque na Mercedes CL63. Thamani ya magari haya inakisiwa kufikia kima cha Sh195 milioni. Mke wake, Pilar Rubio huendesha magari aina ya Cayenne GTS na Audi S9 ambayo kwa pamoja yalimgharimu Sh68 milioni.

Majengo

Ramos alijinunulia kasri la Sh720 milioni jijini Madrid mwishoni mwa 2015. Ana majengo mengine mawili ya kifahari viungani mwa mji wa Camas, Uhispania. Moja kati ya majengo hayo ni lile la Sh475milioni alilowajengea wazazi wake mnamo Aprili 2014.

Familia

Ramos alizaliwa mnamo Machi 30, 1986 katika mji wa Camas, Seville. Mnamo Juni 15, 2019, alifunga pingu za maisha na kichuna mzawa wa Uhispania, Pilar Rubio, 42, baada ya kuchumbiana tangu Septemba 2012. Harusi yao ilihudhuriwa na wachezaji wengi katika kikosi cha Real. Kwa pamoja na mkewe, Ramos amejaliwa watoto wanne wa kiume – Sergio aliyezaliwa mnamo Mei 6, 2014; Marco ambaye alizaliwa Novemba 27, 2015; Alejandro aliyezaliwa Machi 25, 2018; na Maximo Adriano aliyezaliwa Julai 26, 2020.

Ramos amewahi pia kutoka kimapenzi na kichuna Abby Elinsky na mwanamitindo Elisabeth Reyes, 33 aliyeibuka mshindi wa Miss Spain mnamo 2006.

You can share this post!

DIMBA: Haaland ni silaha hatari katika ufungaji mabao

Ujasiri mpya wa Ruto