Mechi sita zilizomfanya Pep kuanza kusitasita Manchester City
BINGWA mtetezi wa Ligi Kuu ya Kandanda Uingereza (Epl) Manchester City wamejikuta katika hali ambayo hawajazoea miaka ya hivi karibuni.
Mechi ya Jumanne ya Kipute cha Klabu Bingwa Ulaya (Ucl) dhidi ya Feyenoord ya Uholanzi, iliendelea kuharibu historia nzuri ya The Citizens.
Manchester City walikuwa kifua mbele 3 – 0 ndani ya dakika 53 ya mechi hiyo. Na kipenga cha mwisho kilipopulizwa, mechi iliisha sare ya 3 – 3.
Mshambulizi wa City Erling Haaland alifunga mabao mawili dakika ya 44 na 53 ya mechi hiyo naye İlkay Gündoğan akafunga kunako dakika ya 50.
Ilichukua robo saa kwa Feyernoord kusawazisha kupitia mabao ya Anis Hadj Moussa (75’) Santiago Gimenez (82’) na David Hancko (89’).
Matokeo ya mechi hii imewapa City rekodi mbaya zaidi katika mkanyagano wa mechi za klabu bingwa ulaya.
Ni timu ya hivi punde zaidi kuwahi kuacha ushindi wa mabao matatu nunge uwaponyoke katika historia ya Ligi ya Mabingwa.
Hakuna timu iliyowahi kuongoza 3-0, zikiwa zimesalia chini ya dakika 20, na kushindwa kuibuka mshindi katika Ucl.
Masaibu ya Pep yanaendelea
Utepetevu wa Man City chini ya Kocha Pep Guardiola umekithiri katika mechi sita zilizopita.
Matokeo haya ambayo yanaonekana kuwa duni kwa mabingwa wa Uingereza, yanajiri baada City kunyanyaswa kwa mabao 4 – 0 walipokabana koo na Tottenham Hotspur katika mechi ya Epl.
Kutokuwepo kwa kiungo Mhispania, Rodri, katika kikosi cha Pep kumewaletea madhara makubwa.
Tangu Februari 2023, Manchester City imepoteza mechi moja pekee kati ya 78 ambazo Rodri ameshiriki, Pep akishinda robo tatu za mechi hizo.
Ila katika mechi 28 ambazo Rodri amekuwa mkekani, asilimia ya ushindi wa City imeshuka hadi 57 huku wakipigwa mara tisa.
Kabla ya kumenyana na Spurs, City ilikuwa tayari imeburuzwa na Brighton & Hove Albion FC 2 – 1 ugani Amex mnamo Novemba 9, 2024.
Vijana wa Pep walianza mechi hiyo vizuri kwa umiliki mkubwa wa mpira kabla ya Haaland kufungua ukurasa wa magoli dakika ya 23.
Brighton walirejea kipindi cha pili kwa nia ya kushambulia zaidi ambapo nguvu mpya Joao Pedro alisawazisha dakika ya 78.
Bao la kipindi cha lala salama la Matt O’Riley liligongomelea msumari wa mwisho katika jeneza la City.
Siku nne kabla ya Brighton kutonesha kidonda cha Pep, vijana wa Ruben Amorim (sasa Kocha Mkuu wa Manchester United) walilima City 4 – 0 katika mchwano wa Ucl walipokutana na Sporting Lisbon ya Ureno.
Kabla ya kushuka dimbani kumenyana na Sporting, Manchester City ilikuwa imepoteza mechi mbili mfululizo kwa mabao 2 – 1 dhidi ya Spurs (Kombe la Carabao) na Bournemouth (Epl).