Akili MaliMakala

Mfumo huu unavyoweza kubadilisha kilimo mijini

Na SAMMY WAWERU September 12th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

KILA Derrick Mugodo anapotazama ardhi ya mijini isiyotumika, huona fursa — nafasi inayoweza kutumika kuzalisha chakula na kukidhi mahitaji ya idadi ya watu inayozidi kuongezeka kila uchao.

Mjasiriamali huyu wa kilimo mwenye umri wa miaka 28, anaamini Kenya haipaswi kuendelea kuwa mateka na kutegemea chakula cha kuagizwa kutoka nje, hasa ikizingatiwa kuwa ni nchi yenye ardhi kubwa isiyotumika ipasavyo.

Kwa Mugodo, ubunifu wa kiteknolojia ndio ufunguo kukabiliana na uhaba wa chakula na njaa.

Akiwa mwanzilishi na Mkurugenzi wa AgriPlant Kenya, kampuni inayoshirikisha vijana, amebuni mfumo wa kilimo cha mashamba ya kusimama – vertical hydroponic system wa  kiotomatiki, unaolenga wakazi wa mijini kuendeleza kilimo.

Derrick Mugodo mwanzilishi na Mkurugenzi wa AgriPlant Kenya, kampuni inayohamasisha kilimo cha kisasa na endelevu mijini. Picha|Sammy Waweru

“Maeneo ya mijini kama vile veranda, sehemu za maegesho ya magari, na mabustani yanaweza kubadilishwa kuwa mashamba yenye tija kupitia teknolojia,” anasema.

Mugodo, ambaye amehitimu Shahada ya Sayansi Masuala ya Utengenezaji, Uhandisi na Teknolojia kutoka Chuo Kikuu cha Egerton, alianza kutathmini wazo hilo baada ya kugundua pengo kwenye sekta ya kilimo akiwa chuoni.

Baada ya kufanya kazi katika kampuni za kuuza maua na mboga nje ya nchi, aligura ajira hiyo mapema 2023 kufuata azma ya ndoto yake — uamuzi anaokiri haukuwa rahisi.

Teknolojia ya vertical gardens na hydroponic ambayo Derrick Mugodo ameboresha kuendeleza kilimo. Picha|Sammy Waweru

Akiwa na akiba kidogo, alianza katika veranda ya nyumba yake, akitumia mtaji wa Sh1,000 kutengeneza mfumo rahisi kwa kutumia vipande vya mitungi iliyogawanywa.

“Mfumo niliounda, utendakazi wake ulitekelezwa kwa mikono (manual system),” anasema.

Kulingana na Mugodo, majirani walivutiwa, na akaanza kutengeneza mifumo sawa na hiyo kwa watu wengine.

Miaka miwili baadaye, ubunifu wake umeimarishwa kupitia utafiti wa kina.

Mfumo wa sasa anautengeneza kwa mabomba ya PVC (paipu) na fremu za chuma, akitundika tangi la kuhifadhi maji na pampu ya umeme au sola.

Mseto wa mboga unaokuzwa kwenye paipu za PVC. Picha|Sammy Waweru

“Mfumo huu unatathmini kiwango cha joto, unyevunyevu, virutubisho na kiwango cha asidi na alikali (pH), na kutuma taarifa kwa mkulima kupitia simu,” anafafanua.

Vipandio badala ya udongo, ni malighafi asilia kama Peat Moss, coco peat na pumice.

Ameboresha mfumo huo kiasi kwamba umeunganishwa na simu kupitia apu au teknolojia ya jumbe fupi, ndiyo SMS.

“Mkulima hata akiwa mbali anaweza kujua mimea yake inavyoendelea, ikihitaji maji anabofya simu tu kuyafungulia na pia kudhibiti kiwango cha joto, ikiwa ni pamoja na kujua virutubisho vinavyohitajika.”

Derrick Mugodo ameboresha teknolojia ya kisasa kulima (vertical gardening/hydroponic) kiasi kuwa ameweka swichi ya kusaidia kupampu maji. Picha|Sammy Waweru

Richard Omondi, mtaalamu wa masuala ya kilimo, anasema mfumo wa vertical hydroponic system hupunguza matumizi ya ardhi na maji kwa karibu asilimia 90, huku ukiruhusu uzalishaji wa mwaka mzima bila kujali hali ya hewa.

“Kwa wanaoishi mijini, ni mfumo faafu kukuza chakula hasa mboga, voungo vya mapishi na matunda. Hupunguza gharama haswa mfumuko unaochochewa na gharama za usafirishaji bidhaa za kula,” Omondi anasema.

Mugodo ana karakana ya kuunda mifumo hiyo ya kisasa Jijini Nairobi, na huunda saizi tofautitofauti.

Derrick Mugodo ameunganisha shamba la ghorofa na tangi la kuisambazia maji. Picha|Sammy Waweru

“Ndogo zaidi inasitiri mimea 50, na tunauza Sh5,000, ile kubwa ikiwa na bei yake kwa mujibu wa maelekezo ya mteja,” akaambia Akilimali kwenye mahojiano ya kipekee.

Kando na kuhudumia wakulima, pia anashirikiana na shule katika kaunti kadhaa nchini, zikiwemo; Nairobi, Nakuru, Kiambu, Nyandarua, na Kakamega, ambapo amesaidia pakubwa kufanikisha Mpango wa Kuungana Kufanya Kusaidia Kenya (4 K Club).

Changamoto yake kuu, hasa alipoanza ilikuwa ukosefu wa fedha kuboresha huduma zake.

Alianza akiwa pekee, na sasa amebuni nafasi za ajira za kudumu kwa wafanyakazi watatu na oda zinapokuwa kibao huajiri vibarua wengine 15.

Derrick Mugodo akielezea kuhusu kilimo cha hydroponic. Picha|Sammy Waweru