Makala

Mfumo wa kutumia gilasi za plastiki kupanda miche, je, zipo athari kimazingira?

April 24th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na SAMMY WAWERU

MICHE ni mimea michanga inayoandaliwa katika sehemu maalum kabla kuhamishiwa shambani.

Kupitia matunzo bora inapohamishwa, huzalisha mazao.

Baadhi ya mimea kama vile mboga, nyanya, matunda, na mingineyo hutegemea miche kuzalisha.

Eneo maalumu inapoandaliwa miche linafahamika kama kitalu.

Kitalu chenye uzoefu kwa wakulima ni kuandaa sehemu, ambapo mchanga huinuliwa juu kiasi, taratibu za upanzi zikafuatwa kisha ikaezekwa au kufunika kwa nyasi zilizokauka ama neti ili kuzuia uharibifu.

Steven Mwanzia, mkulima wa matunda, akionyesha mfumo wa kutumia glasi za plastiki kupanda miche. Picha/ Sammy Waweru

Pia, trei maalumu zenye mashimo hutumika kama kitalu.

Aina nyingine ya kitalu na iliyo rahisi ni kutumia gilasi za plastiki, hususan zinazotumika kunywa kahawa au maji.

Samuel Kinyua, mkulima wa nyanya eneo la Juja, kaunti ya Kiambu, anasema gilasi hizo ni bora zaidi katika utunzaji wa miche.

Zinapotumika, hutupwa na ni hatari kwani zinaweza kuharibu mchanga.

“Wakulima waliopevuka huzikusanya. Hazipaswi kutupwa wala kuchomwa. Wanazitumia kupanda miche,” anaeleza, akidokeza kwamba huzitumia kupanda miche ya nyanya eneo la Juja.

Kulingana na mkulima huyu, aina hii ya kitalu inafanikisha ukuaji wa miche karibu asilimia 95.

Steven Mwanzia, ni mkulima mwingine anayetumia mfumo huu wa kitalu. Chini ya kampuni ya kilimo ya SunBerry Berry Enterprise, hutumia glesi za plastiki kupanda miche ya mitunda inayozaa zabibubata.

“Ni rahisi kupanda na kutunza, kwa sababu glesi moja inatiwa mbegu moja ama mbili,” anasema Bw Mwanzia.

Upanzi

Upanzi wa miche kwa kutumia mfumo huu hauna ugumu wowote. Kulingana na Bw Samuel Kinyua ni kwamba gilasi zile huoshwa vizuri, udongo uliochanganywa sawasawa na mbolea unatiwa mle.

Mbolea inaweza kuwa ile hai, yaani ya mifugo au ya kisasa, fatalaiza. Hata hivyo, ni muhimu kuzingatia kilimo hai hivyo basi ya mifugo ni bora.

Mbegu hupandwa kwenye gilasi, kisha zinatunzwa katika mahali moja, kwa kuzinyunyizia maji.

“Ili kuzuia uharibifu wa ndege, wanyama na hata wadudu, mkulima aziundie hema maalumu kwa kutumia chandaria, kama vile cha mbu,” anasema Bw Steven Mwanzia.

Mbegu huchipuka kati ya siku tano hadi saba.

Miche ya mimea mingi huwa tayari kwa upanzi baada ya siku 30, yaani mwezi mmoja.

Mwanzia anaeleza kwamba humwagiliwa maji ili ing’olewe glasini.

La kutia moyo kwa kutumia mfumo huo ni kuwa hung’olewa na udongo wake na kupandwa nao, suala linaloiwezesha kunawirisha mimea.

Miche inapohamishiwa shambani bila udongo hujikokota kuanza kumea.

Uhamishiaji wa miche shambani unapaswa kufanywa majira ya jioni au asubuhi na mapema, ili kuzuia kukauka.

“Wakati huo miale ya jua si kali. Miche ni mimea midogo inayohitaji matunzo ya hali ya juu,” anahimiza Bw James Murage, mtaalamu wa kilimo Safari Seeds.

Kung’oa

Pia, mdau huyu anashauri haja ya kumwagilia miche maji ili iwe rahisi kuing’oa.

Kulingana na Bw Mwanzia, utumizi wa gilasi za plastiki katika shughuli za kilimo ni mbinu mojawapo kuzuia utupaji kiholela wa bidhaa za aina hiyo zilizotumika.

Anaendelea kueleza kwamba halmashauri ya kitaifa ya mazingira nchini (Nema), imempa idhini kukuzia miche kwenye vifaa hivyo ambavyo baada ya kutumika wengi huvitupa kama taka au kuchoma na kuishia kuharibu mazingira.

Taasisi ya kitaifa ya utafiti wa kilimo na ufugaji nchini (Karlo), ambayo SunBerry Berry Enterprise inashirikiana nayo kuibuka na mbegu bora za matunda bukini imeidhinisha utunzaji wa miche katika glesi hizo.

“Tumekuwa tukishirikiana na Karlo chini ya Dkt Lusike Wasilwa, ambaye ni mkurugenzi wa mimea makao yake makuu, katika shughuli za kutafiti mbegu bora na kukuza miche,” Mwanzia anafichua.

Karlo ndiyo taasisi iliyotwikwa jukumu na serikali kutafiti shughuli za kilimo na ufugaji nchini.