Makala

AKILIMALI: Mhadhiri anayekuza miwa jijini na kuunda hela akiuza sharubati

February 21st, 2019 Kusoma ni dakika: 3

Na PETER CHANGTOEK

SIKU moja alipokuwa akiendesha gari katika barabara kuu ya Thika, Daktari Kennedy Ongaro alilisimamisha gari lake katika kituo cha kuuzia mafuta ili kuongeza mafuta kwa gari lake.

Karibu na kituo hicho cha kuuzia mafuta, palikuwapo na wanawake waliokuwa wakiuza miwa. Pasi na kusita, aliwaomba wampe vipande vya miwa vya kupanda. Walimkabidhi na alivileta vipande hivyo saba, na kuvipanda katika bustani yake iliyoko nje ya nyumba yake, mtaani Ngara, Nairobi.

Dkt Ongaro, mwenye umri wa miaka 51, ambaye pia ni mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Daystar, anasema kwamba alikabidhiwa vipande hivyo vya miwa mnamo mwaka 2013 na mazao yamekuwa yakimridhisha mno.

Mimea yake iliongezekaongezeka, na akashurutika kuvitengeneza vipande vya shamba nje ya nyumba yake ili kuikuza mimea mingine mingi.

Akitutembeza

“Niligundua kwamba miwa ambayo sisi tulikuwa tukiikuza kule nyumbani Kisii, ilikuwa tofauti kabisa na aina iliyokuwa ikikuzwa katika maeneo hayo ya Ol Donyo Sabuk. Niliileta na kuipanda hapa,” asema, huku akitutembeza katika vipande vyake vya shamba.

Mkulima huyo anadokeza kwamba miwa haihitaji mtaji mwingi kuikuza. Anaongeza kuwa alizitumia Sh3,000, pesa taslimu, kuliandaa shamba.

“Mimi hupenda kufanya kazi mwenyewe kwenye shamba siku za wikiendi badala ya kuenda kufanya mazoezi,” asema Ongaro, ambaye ni baba wa watoto watatu.

Anasema aina ya miwa ambayo anaikuza huyazalisha mazao mengi sana. Aidha, anaongeza kuwa miwa hiyo huwa ni mirefu na minene.

Pia, Ongaro anasema kwamba miwa hiyo hukua hadi futi 21 kwa urefu. Fauka ya hayo, muwa mmoja ukipandwa, unaweza kuzaa miwa 21 unapokomaa. Hali kadhalika, aina iyo hiyo huwa na maji mengi yenye sukari.

Dkt Kennedy Ongaro hutayarisha sharubati ya miwa akitumia mashine maalum Ngara, Nairobi. Picha/ Peter Changtoek

Kwa mujibu wa mkulima huyo, aina hiyo ya miwa hukua upesi mno, na hukomaa kabla ya kipindi cha mwaka mmoja.

Mkulima huyo hutegemea mvua ili kuikuza miwa hiyo. Anadokeza kwamba yeye huipanda miwa siku chache kabla mvua haijaanza kunyesha, hususan anapoona dalili za mvua.

Kwa zaidi ya miaka mitano ambapo amekuwa akiendesha shughuli hiyo ya ukuzaji wa miwa, Ongaro anasema kuwa mimea yake haijawahi kuathiriwa na maradhi wala kuvamiwa na wadudu waharibifu.

Yeye huikuza mimea hiyo pasi na kuzitumia mbolea ya madukani. Pia, anafichua kuwa hazitumii kemikali zozote, maadamu kemikali zitawaathiri wateja wake.

Hata hivyo, mkulima huyo huwa haiuzi miwa anayoizalisha, bali huitumia kuitengeneza sharubati.

Hapo awali, yeye alikuwa akiitengeneza na kuiuza sharubati/juisi ya matunda, lakini kwa sababu wakati mwingine matunda huwa hayapatikani, akaamua kuiacha shughuli hiyo, na kujitosa katika shughuli ya kuitengeneza sharubati ya miwa.

Alizinunua mashine tatu za kutengeneza sharubati ya miwa, kutoka nchini Vietnam kwa kima cha Sh1.5 milioni, ambapo mashine moja ilimgharimu Sh500,000.

Hata hivyo, alizinunua mashine zizo hizo akiwa na madhumuni ya kuitumia moja kutengeneza sharubati, nyingine kuwafunza wakulima katika kaunti ya Kisii, na ya tatu kuwafunza watu katika mtaa wa Ngara, anakoishi na kuikuza miwa.

Ongaro ana duka la kuitengeneza sharubati ya miwa katika eneo la Kamakis, karibu na Ruiru na mkewe ndiye anayeisimamia biashara hiyo.
Kwa mujibu wa mkulima huyo, muwa mmoja hutumiwa kutengeneza lita moja au mbili za sharubati, japo hutegemea unene na urefu wa mua.

Kabla ya kuitengeneza sharubati, miwa huvunwa kutoka shambani. Baada ya kuivuna, hukatwakatwa kuwa vipande, kisha maganda hutolewa kwa kutumia kifaa fulani.

Baada ya kuyaondoa maganda hayo, miwa huoshwa na kuwekwa kwenye mashine ili kuminywa pamoja na matunda ya malimau, mmea aina ya mshubiri pamoja na tangawizi ili sharubati hiyo iwe na ladha aula na kuongezea virutubisho muhimu.

Malimau na tangawizi

Mkulima huyo anasema kwamba yeye huyanunua malimau na tangawizi kutoka kwa soko la Wakulima au Marikiti, jijini Nairobi.

Anaongeza kuwa yupo mtu ambaye ameweka mkataba naye ili awe akimletea mmea wa mshubiri.

Wao hutengeneza sharubati lita 25 kwa siku nzuri, na lita moja ya juisi hiyo huuzwa kwa bei ya Sh400, katika eneo la Kamakis. Hata hivyo, huiuza juisi hiyo lita moja kwa Sh200 nyumbani. Juisi glasi moja kubwa huuzwa kwa Sh200.

Sharubati anayoitengeneza huwa haiongezewi maji hata chembe.

“Baadhi ya watu huongezea maji kwa juisi, na haifai, ndiposa ni muhimu kuitengeneza wakati mteja anapotazama,” asema mhadhiri huyo wa Chuo Kikuu cha Daystar.

Anadokeza kwamba biashara hiyo imenoga mno kwake, na hajawahi kujuta asilani, kujitosa katika shughuli hiyo.

Dkt Ongaro anafichua kuwa kuna shamba ekari 40, alilolinunua miaka mitano iliyopita, katika kaunti ya Kajiado, na ananuia kulitumia kuwa kituo cha kutolea mafunzo kuhusu ukuzaji wa miwa na mizabibu.

Pindi tu kituo hicho kitakapokamilika kujengwa, wakulima, hususan vijana, watapata fursa ya kupokea mafunzo ya bwerere, kuhusu jinsi ya kuikuza miwa na mizabibu, na jinsi ya kuiboresha thamani ya mazao yatokanayo na mimea hiyo.

Anaongeza kusema kuwa anaendelea kufanya mazungumzo na kampuni inayozitengeneza mashine za kutengeneza sharubati ya miwa, iliyoko nchini Vietnam, ili awe akizinunua mashine hizo kutoka kule, na kuwauzia vijana.

“Watalazimika kulipa nusu ya fedha halafu walipe zilizosalia kwa muda wa miaka miwili au mitatu,” afichua.

Kwa mujibu wa wataalamu wa afya, sharubati ya miwa ina vitamini kama vile Vitamini A, C, B1, B2, B3, B5 na B6.