Jamvi La SiasaMakala

Michakato ya kutimua magavana, manaibu gavana yarahisishwa

Na CHARLES WASONGA March 21st, 2025 Kusoma ni dakika: 1

MCHAKATO wa kuwaondoa afisini magavana na manaibu gavana sasa utarahishwa kufuatia kuzinduliwa kwa mwongozo unaofafanua taratibu na kanuni zinazopasa kuzingatiwa kuendesha zoezi hilo.

Mwongozo huo ambao umechapishwa na Seneti unalenga kuhakikisha kuwa madiwani wanazingatia Katiba ya Kenya na Sheria ya Serikali za Kaunti wanaposhughulikia hoja ya kumtimua wakuu hao wa kaunti wanapotenda mazito.

Aidha, chapisho hilo linalenga kuhakikisha kuwa adhabu hiyo inatumika kama chombo cha kuimarisha uwajibikaji kinatumika kisheria na kwa njia ya haki.

Akiongoza hafla ya uzinduzi wa mwongozo huo Alhamisi, Machi 20, 2025, Spika wa Seneti Amason Kingi alisema utawarahishia kazi madiwani na maseneta wanaohusika katika mchakato wa kuondolewa afisini kwa magavana na manaibu wao.

“Kwa kutoa taratibu, kanuni, mahitaji ya kisheria na ya kikatiba ambayo yanapasa kufuatwa, chapisho hili linawarahishia kazi madiwani ambao ndio huandaa hoja za kuwatimu magavana na maseneta walio na usemi wa mwisho katika kuthibitisha mashtaka yaliyoko kwenye hoja hizo,” akaeleza.

“Kwa njia hiyo, mwongozo huu unahakikisha kuwa hoja kama hiyo inatumika kuendeleza ajenda ya kuimarisha uwajibikaji na uongozi bora wala haitumiki kufanikisha malengo ya kisiasa,” Bw Kingi akaongeza alipoongoza uzinduzi huo katika mkahawa mmoja jijini Nairobi.

Magavana wamekuwa wakidai kuwa nyingi za hoja zinadhamini dhidi ya wenzao huchochewa na mahasidi wao kisiasa.

Uzinduzi wa chapisho hilo umefanyika siku chache baada ya Mahakama Kuu kutoa uamuzi uliodumisha kutimuliwa afisini kwa aliyekuwa Gavana wa Meru Kawira Mwangaza.

Jumatatu wiki hii aliyekuwa naibu wake, Isaac Mutuma aliapishwa kuwa Gavana mpya wa Meru.

Ndani ya miaka 10 iliyopita, Seneti imekabiliwa na hoja 15 za kutimua magavana na manaibu gavana.

Kando na Bi Mwangaza, magavana wengine ambao wamewahi kuondolewa afisini kwa njia hiyo ni Mike Sonko (Nairobi) na Ferdinand Watitu (Kiambu).

Mnamo Mei 24 mwaka jana Seneti pia ilipitisha hoja ya kutimua aliyekuwa Naibu Gavana wa Kisii, Robert Monda.