Akili MaliMakala

Mikakati ya KMC kuhakikisha Wakenya wanapata nyama bora na salama  

Na SAMMY WAWERU August 5th, 2025 Kusoma ni dakika: 3

KIWANDA cha Kutayarisha Nyama Nchini (KMC) kinapanga kufungua maduka ya kuuza nyama maeneo tofauti Kenya, hii ikiwa ni mojawapo ya mikakati yake kuhakikisha wananchi wanapata nyama salama, bora na kwa bei nafuu.  

KMC inasimamiwa na Wizara ya Ulinzi, na tayari ina maduka (buchari) yanayofanya kazi katika kaunti za Nairobi na Machakos.

Kulingana na Kamishna Mkuu wa taasisi hiyo ya kiserikali, Meja Jenerali Jattani Gula, mpango huo unalenga kuhudumia Wakenya kwa hadhi ya juu.

Alisema KMC inajikakamua kuhakikisha huduma zake zinaakithi vigezo vya Sheria ya Usalama wa Chakula na Lishe ya 2023 inayosubiri kupitishwa na bunge.

Mswad huo, uko kwenye awamu ya mwisho kuidhinishwa na utasaidia kutoa mwelekeo jinsi bidhaa za chakula nchini zinapaswa kushughulikiwa.

Kwenye mahojiano ya kipekee na Akilimali, Meja Jenerali Gula alifichua kuwa buchari zaidi na ambazo ni za kisasa zitafunguliwa Nairobi, Kajiado, Kiambu, na Mombasa kabla ya kupanua huduma katika maeneo mengine nchini.

“Tayari tuna maduka yanayofanya kazi Athi River na Muthurwa, Nairobi,” alisema.

KMC ina kiwanda cha kuchinja mifugo katika makao yake makuu Athi River, Kaunti ya Machakos, kilichokumbatia mifumo na teknolojia ya kisasa ikiwemo kuhifadhi nyama (cold chain system).

Awali, taasisi hiyo ilikuwa ikifanya mauzo yake kupitia mawakala na mabroka, lakini sasa inalenga kuanzisha maduka ya moja kwa moja kuuza nyama na bidhaa za nyama.

Miaka minne baada ya Rais mstaafu Uhuru Kenyatta kuhamisha usimamizi wa KMC kwa Idara ya Ulinzi, Jeshi la Ulinzi la Kenya (KDF) limesifiwa kufufua taasisi hiyo.

Bw Gula anasema kutokana na mafanikio yaliyoshuhudiwa, buchari zaidi zitafunguliwa Kitengela na Rongai (Kajiado), Thika (Kiambu), Mtwapa, Changamwe (Mombasa) na Likoni (Kilifi).

Kenya Meat Commission (KMC), kufikia mwishoni mwa mwaka huu, 2025 itaanza kuuza nyama na bidhaa za nyama Gulf. Picha|SAMMY WAWERU

“Baadhi ya maduka yetu hufanya mauzo ya hadi Sh1 milioni kwa siku – kila buchari, hasa Ijumaa na wikendi,” alibainisha.

Mauzo hayo ya juu ndiyo yamechochea kiwanda hicho kufungua buchari zaidi.

Kiwanda cha KMC huzalisha nyama bora na bidhaa kama vile sausagessmokiesmutura, na nyinginezo.

Hata hivyo, maduka hayo yanapangishwa, na gharama ya kodi haitazidi Sh100,000 kwa mwezi, Meja Jenerali Gula alidokeza.

KMC huzingatia viwango vya kimataifa katika usindikaji wa nyama, huku ikinunua mifugo kutoka maeneo kame na nusu-kame (ASAL).

Taasisi hiyo pia inapanga kufungua vituo vya kuchinja mifugo kaunti mbalimbali.

Gula alielezea kuwa wafugaji wanakumbwa na changamoto ya gharama kubwa ya kusafirisha mifugo hadi Athi River, hivyo ufunguzi wa vituo maeneo wanayotoka utasaidia kupunguza hasara.

KMC inashirikiana na serikali za kaunti kujenga vituo vya kuchinja mifugo ili kupunguza gharama hizo.

Kaunti ya Mombasa tayari ina kichinjio cha kisasa eneo la Kibarani, huku baadhi ya kaunti kutoka Kaskazini Mashariki, Nyanza, Bonde la Ufa na Magharibi Gula akisema wanaendeleza mipango kushirikiana kuanzisha vituo vya kuchinja.

“Mifugo itakuwa ikichinjwa katika kaunti, na kwa kutumia matrela yetu yenye jokofu kuhifadhi, nyama zitasafirishwa hadi kiwandani kwetu kwa minajili ya usindikaji zaidi,” alisema afisa huyo.

Tangu KDF ichukue usimamizi 2021, uzalishaji umeimarika, huku KMC ikichangia kati ya Sh2.1 bilioni hadi Sh2.8 bilioni kwa pato la taifa (GDP) kila mwaka.

Awali, taasisi hiyo ilikuwa ikipata Sh256 milioni pekee kwa mwaka.

Kwa sasa, KMC inachinja wastani wa mifugo 300 kwa siku, ikilinganishwa na 50 miaka ya zamani.

Kiwanda hicho, Meja Jenerali Gula anasema kina uwezo wa kuchinja ng’ombe 1,000, na mbuzi na kondoo 1,500 kwa siku.

Kwenye Makala ya Nne ya Kenya Meat Expo and Conference yatakayofanyika KICC Nairobi kuanzia Agosti 6 hadi 8, 2025, KMC itakuwa miongoni mwa washirika watakaohudhuria kuonyesha mchango wao kwenye sekta ndogo ya nyama.

Maonyesho hayo yanayofanyika kila mwaka, 2025 kaulimbiu ikiwa ‘Driving Sustainable Growth Across the Meat Value Chain’, huandaliwa na Nation Media Group (NMG) PLC.

Afisa Mkuu Mtendaji wa Shirika la Habari la NMG, ambaye pia ndiye Mkurugenzi Mkuu, Bw Geoffrey Odundo, anasema kampuni hiyo itaendelea kuunga mkono sekta ya nyama kwa kutoa taarifa za kina na kuangazia changamoto zinazokumba mtandao mzima.