Mike Kamau: Msusi ambaye wanawake Murang'a wanamsifia
Na MWANGI MUIRURI
BAADA ya kukamilisha elimu ya kidato cha nne mwaka wa 2015 na kupata alama ya C, Mike Kamau alikosa namna ya kusonga mbele kielimu kwa kuwa wazazi wake walikosa namna ya kumfadhili.
Alianza kufanya vibarua hapa na pale vijijini katika Kaunti ya Murang’a, kwa wakati mwingine akiwajibikia hata majukumu ya shambaboi ili maisha yake yaendelee mbele akisaka mwanya wa kujijenga.
Mwaka wa 2016 Gavana wa Murang’a, Mwangi Wa Iria alitangazo kuwa alikuwa akifadhili vijana wasio na taaluma kwa kozi za muda mfupi na ndipo Bw Kamau akaona wingu la wema limempasukia likimteremshia baraka.
Bila kusita, aliingia katika taasisi ya kiufundi ya Sabasaba ambapo baadhi ya makurutu walikuwa wamejiunga nayo kuwajibikia fursa adimu na yenye thamani kubwa ya kaunti kuwahami wawe na maarifa.
Bw Kamau anasema kuwa alipiga msasa kozi ambazo zilikuwa zikitolewa na akafanya uamuzi wake.
“Udereva, ushonaji nguo na viatu, utengenezaji sabuni, useremala, ususi na urembeshaji… Niliangalia idadi ya waliokuwa wakichagua kila kozi na ndipo nikang’amua kuwa ile ya urembeshaji na ususi haikuwa na hata mwanamume mmoja. Nilifanya hesabu yangu ya haraka na ndipo nikapata kuwa ningeishia kuwa wa kipekee ningeichagua; na nikaichagua,” anasema Bw Kamau.
Baada ya miezi mitatu, alihitimu akiwa na ujuzi wa ususi na urembeshaji na Gavana Wa Iria akawatuza kila mtu pesa za mtaji kuzindua harakati za kujipa ajira.
“Nilipewa Sh20,000 na nikaingia sokoni mara moja na nikanunua bidhaa za kimsingi katika kushirikisha kozi hii yangu,” anasema akitaja mafuta, kemikali aina mbalimbali za urembo na nyuzi pamoja na sindano kama baadhi ya vifaa alivyojihami navyo kuingia sokoni kusaka kazi ama bora tuseme wateja.
Na ule uamuzi wake wa kuchagua kozi ambayo haikuwa imewavutia wanaume wengi ukampa matunda.
“Nilijipata nikiwaniwa na wateja wa kike na hapo ndipo niligundua wanawake huwasiti kuhudumiwa na wanaume. Hata nishawahi kusikia kuwa wanawake huchagua kutibiwa na madaktari wa kiume. Hata wakiwa waja wazito, naambiwa wao hupendelea ukunga wa daktari mwanamume wala sio wa kike,” anasema ingawa kwa hili, jukwaa hili halikuzamia zaidi.
Tangu ahitimu, anasema kuwa hawezi akajutia kuchagua kozi hii.
“Mungu awabariki wanawake wote ambao hunipa kazi ambapo katika mitaa mingi ya kaunti ndogo ya Kigumo, nimejishindia umaarufu kiasi kwamba ninaweza nikapigiwa simu leo, jibu langu liwe ninaweza nikapatikana baada ya siku nne,” anasema.
Anasema kuwa utiifu wa wateja wake ni kuwa huwa wanamuelewa na huwa na subira hadi apatikane.
Uzuri ni kwamba, wateja wake humwita nyumbani kwao hivyo basi kumpunguzia changamoto za kibiashara ambapo angehitajika kukodisha jumba la kibiashara.
Kuhusu hatari ya baadhi ya wateja wake kumwingiza katika mtego wa “tuongee ya ziada juu ya uteja”, anachekacheka akisema “sitaki kuudhi wateja wangu na udaku”.
Anasema kazi yake huifanya kwa utaalamu mkubwa.