Makala

‘Mitume’ 9 waaminifu kwa Ruto ambao ndio kusema serikalini

Na BENSON MATHEKA May 15th, 2025 Kusoma ni dakika: 3

RAIS William Ruto amezungukwa na kundi la viongozi ambao wamesimama naye katika nyakati muhimu za maisha yake ya kisiasa na hawawezi kuguswa katika serikali yake.

Baadhi waliamini ndoto yake hata alipokuwa akipigwa vita vikali na wapinzani na hata baadhi ya wanasiasa kutoka chama chake cha zamani cha Jubilee.

Ni viongozi hawa ambao sio tu walikita imani yao kwake, bali pia walijitoa kwa hali na mali ikiwemo kupokonywa nyadhifa kuu chini ya utawala wa Jubilee kuhakikisha anaingia Ikulu.

Hii ndiyo sababu wanashikilia nafasi ya pekee katika moyo wake.

Kimani Ichung’wah, Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Taifa, amekuwa mmoja wa wafuasi waaminifu wa Rais Ruto.

Alijitokeza wazi kumtetea Ruto wakati wa mvutano wa kisiasa ndani ya Jubilee.

Amethibitisha kuwa kiongozi wa kuaminika na mwenye msimamo thabiti, anayejua kulinda ajenda ya serikali bungeni.

Ichung’wah ni daraja kati ya Rais na wabunge wengi wa Kenya Kwanza, na hilo linampa nafasi ya kipekee katika maamuzi ya serikali.

Waziri wa Afya, Aden Duale, ni mmoja wa viongozi walioganda na Ruto hadi akapoteza wadhifa wa Kiongozi wa Wengi Bungeni wakati wa serikali ya Jubilee.

Duale ameonyesha ujasiri wa kusimama na kile anachoamini hata katika nyakati za shinikizo kubwa.

Uaminifu wake kwa Ruto, pamoja na uzoefu wake wa kisiasa, unamfanya kuwa mshirika wa karibu sana.

Ni mmoja wa mawaziri wa serikali ya Ruto ambao wamesimamia wizara tatu chini ya miaka mitatu ya utawala wa Ruto.

Alianza na Ulinzi, akahamishiwa Mazingira na sasa yuko Afya.

Kama vile Duale, Waziri wa Usalama wa Ndani Kipchumba Murkomen alipoteza wadhifa wake kama kiongozi wa wengi katika seneti wakati wa utawala wa Jubilee kwa kuunga Ruto, alikuwa miongoni mwa wanasiasa wa kwanza kumtetea Ruto alipokuwa na changamoto ndani ya serikali ya Jubilee.

Ufasaha wake wa kujieleza na ushujaa wake bungeni ulimweka mstari wa mbele katika kutetea mrengo wa Ruto.

Leo, akiwa waziri, anaendelea kusukuma mbele ajenda ya Rais ya kuinua uchumi kutoka chini kwenda juu.

Kama Duale pia, ameshikilia wizara tatu katika serikali ya Kenya Kwanza. Alianza na Uchukuzi, akahamishiwa Michezo na kwa sasa anasimamia wizara yenye nguvu zaidi ya Usalama wa Ndani.

Naibu Rais Prof Kithure Kindiki pia ameganda na Ruto tangu akiwa wakili wake katika kesi iliyomkabili ICC.

Kwa sababu ya kumuunga Ruto, alivuliwa wadhifa wa Naibu Spika wa Seneti chini ya utawala wa Jubilee. Baada ya Ruto kushinda urais, alimteua waziri wa Usalama wa Ndani.

Alikuwa miongoni mwa washauri wa karibu wa Ruto wakati wa kampeni za uchaguzi wa 2022.

Baada ya Ruto kutofautiana na aliyekuwa mgombea mwenza wake Rigathi Gachagua na kumtimua kama naibu rais alimzawadi Kindiki wadhifa huo.

Waziri wa Ardhi Alice Wahome alianza kwa kuteuliwa na Ruto kuwa Waziri wa Maji.

Ni mmoja wa wanawake wachache waliothubutu kusimama na Ruto katika wakati mgumu wa kisiasa.

Msimamo wake usioyumba, hasa alipokuwa mbunge wa Kandara, ulimweka katika kundi la wanasiasa waliomsaidia Ruto kujijenga kisiasa na kuimarisha umaarufu wake miongoni mwa wanawake na Mlima Kenya kwa jumula.

Davies Chirchir, Waziri wa Uchukuzi, ni mtaalamu ambaye alichangia sana katika mikakati ya uchaguzi wa Ruto.

Uwezo wake katika teknolojia na usimamizi wa uchaguzi ulimpa heshima kama “mtaalamu wa kimkakati” wa kikosi cha Ruto.

Uaminifu wake kwa Ruto na utendaji wake uliomakinika zinamfanya kuwa na nafasi muhimu katika moyo na utawala wa Ruto ambaye alimteua kwanza kusimamia wizara ya Kawi na Petroli kabla ya kumhamishia uchukuzi.

Ukuraba wa Dennis Itumbi na Rais Ruto ulianza wakati wa kesi yake katika ICC na katika utawala wa Jubilee.

Itumbi alipoteza kazi yake kama mkurugenzi wa mawasiliano ya dijitali Ikulu lakini akaganda na Ruto hadi wakati wa kampeni.

Anatekeleza jukumu muhimu katika mawasiliano ya Kenya Kwanza.

“Viongozi hawa si tu washirika wa kisiasa wa Rais William Ruto, bali ni watu waliopata imani yake. Walihatarisha taaluma zao za kisiasa kumuunga mkono, na sasa, anawategemea kutekeleza ajenda ya serikali yake. Nafasi yao moyoni mwake si kwa sababu ya nyadhifa za kisiasa tu, bali ni matokeo ya safari ya pamoja ya kujitolea na uaminifu usioyumba,” anasema mchambuzi wa siasa Dkt Isaac Gichuki.

Felix Kiptarus Koskei, Mkuu wa Wafanyakazi na Mkuu wa Utumishi wa Umma, ni mmoja wa wandani wa karibu na wanaoaminika zaidi wa Rais William Ruto.

Uhusiano wao, uliotokana na historia ya pamoja ya kitaaluma na kujitolea kwao kwa huduma kwa umma, umegeuka kuwa ushirikiano wa kisiasa wa nguvu.

Mnamo Oktoba 2022, Rais Ruto alimteua Koskei kuwa Mkuu wa Wafanyakazi na Mkuu wa Utumishi wa Umma, akichukua nafasi ya Joseph Kinyua.

Nafasi hii ilimweka Koskei katikati ya utendaji wa serikali, akisimamia uratibu wa shughuli za serikali na kuwa kiungo muhimu kati ya Rais na utumishi wa umma, kuhakikisha kuwa shughuli zinaendana na ajenda ya Rais.

Farouk Kibet ni mmoja wa watu wenye ushawishi mkubwa zaidi na wanaoaminiwa na Rais Ruto.

Katika serikali ya Kenya Kwanza, Kibet ana ushawishi mkubwa. Anajulikana kwa maadili yake ya nidhamu, uaminifu, na mpangilio, sifa ambazo zimemfanya kuwa mtu muhimu katika serikali ya Kenya Kwanza.

Uaminifu wa dhati wa Farouk Kibet, uwezo wake wa kupanga mambo, na ushiriki wake mkubwa katika masuala ya kisiasa na ya kijamii vinadhihirisha nafasi yake ya kipekee katika safari ya kisiasa ya Rais Ruto.