Mjadala wa kupiga marufuku shule za bweni washika moto
KUFUATIA moto wa kutatanisha unaoathiri mabweni katika shule kadhaa za bweni nchini siku za hivi karibuni, Mbunge wa Imenti Kaskazini Rahim Dawood anapendekeza shule za bweni zifutiliwe mbali haswa ikiwa machafuko ya sasa yanayosababishwa na wanafunzi yataendelea.
Akizungumza katika Shule ya Sekondari ya CCM Township mjini Meru, Bw Dawood alisema inasikitisha kuwa matukio hayo ya moto yanaweza kusababisha majeruhi na maafa pamoja na uharibifu wa mali.
Aliongeza kuwa iwapo visa vya uteketezaji wa mabweni ya shule vitaendelea, serikali haitakuwa na njia mbadala ila kuzipiga marufuku shule za mabweni.
“Inashangaza kuwa mioto hii inashuhudiwa tu katika shule za bweni na wala si shule za kutwa. Jambo lingine ni kwamba, matukio haya kwa kawaida hutokea wakati wa mitihani ambayo mara nyingi huwa katika muhula wa tatu wa mwaka wa masomo. Kufuatia hali hiyo, serikali inafaa kuzingatia kupitisha pendekezo la kukomesha shule za bweni au kutafuta kujua sababu kuu,” akasema Bw Dawood.
Mwongozo
Wakati huo huo mbunge huyo aliwashauri wanafunzi hao kuomba mwongozo na ushauri nasaha kutoka kwa walimu, wazazi, na maafisa wa elimu endapo watapata matatizo badala ya kuchoma mabweni na kusababisha hasara.
Aliwapa pole waathiriwa wa mkasa wa moto wa Endarasha Hillside Academy akieleza kuwa, ametembelea shule kadhaa za bweni na hakufurahishwa na miundomsingi ya mabweni katika taasisi hizo.
“Wizara ya Elimu inapaswa kutathmini hali ya shule za bweni ili ziwe salama kwa wanafunzi. Pia walezi wanafaa kulazimishwa kulala kwenye mabweni na wala si nje ili waingilie kati kuwaepusha wanafunzi na hatari,” akasema Bw Dawood.
Haya yanajiri baada ya mbunge mwenzake wa Dagoretti Beatrice Elachi kusema watoto wanafaa kuishi na wazazi wao katika umri mdogo badala ya kufungiwa katika shule za bweni.
“Shule za kutwa zitasaidia sana watoto walio katika hatua za kukua wawapo shule za msingi. Kuwatenganisha na wazazi katika kipindi hiki muhimu hakufai kabisa,” alisema Bi Elachi.
“Kuenda mbele, shule zote za msingi nchini hazifai kuwa za bweni na wazazi wanafaa kukaa na watoto wao. Hii ndiyo njia ya pekee ya kuwalinda watoto wetu dhidi ya majanga,” aliongeza.
Wakati uo huo, serikali inashinikizwa kuweka ukomo wa umri ambao watoto wanafaa kuhudhuria shule za bweni.
Mwenyekiti wa Baraza la Madhehebu Mbalimbali Kaunti ya Kakamega Askofu Nicholas Olumasai amewashifu wazazi kwa kutelekeza majukumu ya kuwalea watoto wao kwa kuwapeleka shule za bweni.
“Serikali inafaa kuweka sheria ambayo inaruhusu watoto wenye umri wa angalau miaka 12 kusomea shule za bweni. Hii ni kwa sababu, wakiwa na umri huu, wanaweza kujilinda,” alisema Asjofu Olumasai.