MKASA: Stovu yasababishia familia majeraha
Na GEOFFREY ANENE
MAMA mmoja kutoka mtaani Kariobangi South Civil Servants anataka kampuni ya kuunda majiko ya KOKO Networks iondoe bidhaa zake hizo sokoni baada ya kuchomwa vibaya stovu hiyo ya meko mawili ilipojiwasha yenyewe.
Grace Mbwika anauguza majeraha hayo ambayo Daktari Jackson Onduso kutoka hospitali ya Apollo Medicare ametaja kuwa mabaya sana. Stovu hiyo, ambayo inatumia mafuta ya Ethanoli, iliwaka moto bila ya mtu kuwa ndani ya nyumba na kuanza kuteketeza vitu.
Anasema kampuni hiyo ilikubali kuwa stovu hiyo ina kasoro baada ya kuikagua wenyewe nyumbani kwake. Mtoto wake wa kiume Prince Jeremy pia aliumizwa miguu yake katika ajali hiyo ya moto mnamo Aprili 22 mchana.
Aliponunua jiko hilo kwa Sh3,500, Mbwika alikuwa mwenye furaha sana. Alikuwa ametimiza ombi la watoto wake Jeremy na Ann Titus, ambao walitamani sana kuwa na kifaa hicho nyumbani mwao baada ya kukiona kwa rafiki yao mtaani Buru Buru.
Miezi miwili baadaye, furaha hiyo iligeuka kuwa karaha.
“Tulikuwa nje ya nyumba tukiambua maganda ya mbaazi tulizokuwa tumenunua sokoni wakati mtoto wangu wa kiume alipopiga kelele kusema kuna moto,” alitanguliza.
Mwanzoni, Mama Jere anavyofahamika Mbwika kwa jina la utani na wakazi wa mtaa wa Kariobangi South, alidhani mtoto wake alikuwa akifanya mzaha.
Hata hivyo, aliamua kuingia kwenye nyumba kuthibitisha. Kwa mshangao, jikoni ilikuwa imeshika moto uliokuwa unasambaa kutoka stovu hiyo.
“Nilianza kutupa vitu, ambavyo havikuwa vimeshika moto, nje ya nyumba ili kuuzuia kuenea zaidi. Hata hivyo, mafuta hayo ya Ethanoli yalinirukia kwenye mkono wangu wa kulia na moto kuanza kunichoma. Ilinilazimu nikimbilie usalama nje ya nyumba. Nilitoa tishati niliyokuwa nayo kwa sababu ilikuwa imeshika moto na kujibingirisha kwenye nyasi mbichi ili kujiokoa. Mtoto wangu wa kiume pia alichomwa miguu. Hata hivyo, sikumbuki kilichofuata kwa sababu nilikuwa na uchungu mwingi, ingawa niliambiwa baadaye kuwa watu walikuja hapa na kusaidia katika kuzima moto kwa kutumia maji nilipokimbizwa hospitali kupokea matibabu,” alisema mama huyo.
“Nilihisi uchungu sana, lakini nashukuru kuwa daktari alifaulu kunipatia dawa za kuupunguza pamoja na kunitibu. Bado naendelea kupokea matibabu,” alisema Mbwika, ambaye ni mfanyabiashara katika soko la City Market katikati mwa jiji la Nairobi.
Baadaye, Mama Jere anasema, alipigia simu watu kutoka kampuni ya KOKO kuwafahamisha kuhusu ajali hiyo.
“Walikuja hapa na kufanya uchunguzi wao. Walikagua stovu hiyo na kupata kuwa inavuja na kukiri kuwa stovu zao zina hitilafu. Walipiga picha kadha na kuondoka. Waliahidi watanipigia simu, lakini hawajafanya hivyo. Walitaka kuenda na jiko lao, lakini nikawakataza. Nimeliweka nyuma ya nyumba yangu na kulifunika. Bado halijaacha kuvuja,” alisema.
Ajali hiyo ni pigo kubwa kwa familia ya Mama Jere. “Kwa sasa, sijui ni aina gani ya kafyu ambayo nimejipata ndani kwa sababu siwezi kuenda kazini. Nahitajika kulipa kodi ya nyumba, bili nyinginezo, watoto wangu wanahitaji kula na pia mahitaji mengine. Wananihitaji. Mimi ndiye baba yao na pia mama. Tangu waende, watu kutoka KOKO walisalia kimya,” alisema na kudai kuwa hicho hakikuwa kisa cha kwanza katika eneo hilo.
“Ajali mbili zinazotokana na stovu hiyo ziliripotiwa wiki chache zilizopita; moja katika mtaa wa Dandora na nyingine papa hapa Civil Servants. Kwa bahati mbaya, wao waliamua kukimya tu. Mimi nimeamua sitanyamaza. Nitapaza sauti yangu kwa sababu hata sijaona muhuri wa Shirika la Kukadiria Ubora wa Bidhaa (KEBS) katika jiko lao. Sijui hata kwa nini majiko haya yanapatikana sokoni bila idhini ya KEBS,” aliuliza Mama Jere.
Kwenye tovuti yake, kampuni ya KOKO inasema kuwa ni kampuni ya kimataifa ya teknolojia isiyo na kifani.
“Sisi tunaongoza duniani kwa kutumia mafuta safi ya Ethanoli na pia bidhaa za kupika,” inaongeza.
KOKO inasema kuwa stovu zake zimeundwa spesheli kwa soko la Kenya na nizakutemegewa”.
Hata hivyo, wateja kadha wametilia shaka usalama wa stovu hizo. Huenda stovu hizo si ‘salama kabisa’ jinsi kampuni hiyo inadai.
Mtumiaji mmoja wa mtandao wa Facebook kwa jina Issa Kiama aliuliza kampuni hiyo kwanini kizibo cha kufunika mafuta cha stovu hiyo kinafunguka chenyewe. Richie Odero pia alitaka kujua kwanini chombo hicho hakijifungi.
Badala ya kuchapisha majibu kwenye ukurasa huo wake wa Facebook, kampuni hiyo iliitisha nambari zao za simu ili kuzungumza nao binafsi. Wateja wengine pia wamekuwa wakilalamika kuwa majiko hayo yanatumia mafuta mengi sana na pia bei ya Ethanoli si rahisi.
Tatizo kubwa kwa Mama Jere sasa ni kuwa maisha yake yamefanywa kuwa magumu zaidi. Hawezi kuinua mkono wake wa kulia anaotumia sana. Anasema akijaribu kuuinua anahisi kama kwamba anainua ndovu.
Daktari wake anasema Mama Jere anapiga hatua nzuri katika matibabu hayo. Mama Jere mwenyewe anasema anatarajia kurejea kazini mwezi Juni.
Yeye hulipa kodi ya nyumba ya Sh9,000. Ukiongeza vitu kama bili za stima, maji, ada ya usalama na matumizi mengineyo, anasema yeye hutumia Sh20,000 kila mwezi. Akiwa anategemewa kwa kila kitu, mambo yamefanywa kuwa hata magumu zaidi wakati huu wa janga la virusi hatari vya corona.
Kampuni ya KOKO Networks ilizinduliwa jijini Nairobi mwezi Mei 2019. Inapatikana jijini Nairobi na viungani mwake. Inasema imefungua stoo zaidi za 700. “Tunafanya mipango ya kuanza kuhudumia wateja nje ya Nairobi,” kampuni hiyo ilitangaza kwenye ukurasa wake wa Facebook ilipoulizwa na mteja mmoja kwa jina Eunice Kairuthi kutoka kaunti ya Meru.
Wakati huu, stovu ya KOKO ya meko mawili inanuliwa kwa Sh4,500. Huwa ina mtungi mmoja wa mafuta lita 2.3, ambao hujazwa ukiisha.
Hapo Jumanne, Mama Jere aliambia tovuti ya Taifa Leo kutoka mtaani mwake kuwa maafisa wa kampuni hiyo walifika kwake adhuhuri baada ya kupokea maswali kutoka Taifa Leo. Walitaka akubali kubadilishiwa stovu yake. “Nilikataa,” alisema mama huyo kabla ya kuongeza kuwa aliuliza maafisa hao kuhusu fidia, lakini wakasema lazima wazungumze na afisi ili kupata mwelekeo zaidi.
Baadaye jioni, KOKO ilitoa taarifa kusema kuwa usalama wa wateja wake ni kitu inachukulia kwa uzito. “KOKO haitawahi kuchukulia usalama kimzaha na itaendelea kutua huduma ambazo wateja wanamudu kununua na kutoa njia mbadala ya kupikia,” Afisa Mkuu Mtendaji Greg Murray alisema katika taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari akisisitiza kuwa bidhaa zao zimeidhinishwa na KEBS.
Hatujafaulu kupata maoni kutoka kwa KEBS kuhusu suala hili baada ya simu zetu kukatwa tukijaribu kuwafikia.