Mkulima aibuka na mitufaha inayochukua muda mfupi kuzaa matufaha
Na SAMMY WAWERU
BW Peter Wambugu ni mkulima wa matofaha Laikipia na ni shughuli aliyoanza mwaka 1985.
Awali, alikuwa akipanda kahawa, matunda ya kuongeza damu mwilini na karakara, na anasema hayakuwa na faida kamwe.
Aliasi kukuza mimea hiyo, akavalia njuga kilimo cha matufaha.
Ni matunda ambayo yamemzolea sifa chungu ulimwenguni kutokana na tafiti zake.
Anasema upandikizaji umemwezesha kupata matufaha ambayo yakipandwa leo, miezi tisa baadaye mkulima ataanza kupata mazao.
Matufaha ya kawaida nchini na mataifa mengine huvunwa baada ya miaka miwili.
Ya mkulima huyu ni aina ya matofaha yanayofanya vyema maeneo ya kiangazi, hasa yanayopokea mvua kiduchu.
Isitoshe, anasema hayabagui mchanga.
Matufaha yanaaminika kustawi maeneo ya baridi kwa minajili ya kushinikiza majani yapukutike, ili uchanaji wa maua uanze, hatua muhimu kuruhusu uundaji wa matunda.
Bw Wambugu anasema haya mapya pia yanakua vyema eneo lolote, bora tu mchanga usiwe utuamishao maji.
Matufaha yake ni ya kupandikiza na uvumbuzi wake umeidhinishwa na taasisi ya kitaifa ya utafiti wa kilimo na ufugaji nchini (Karlo) na ya ubora wa mimea (Kephis).
“Karlo ndiyo iliyapa jina la Wambugu Apples, baada ya kuyapiga msasa na kubainika utafiti tuliofanya uliafikia ubora unaohitajika,” anasema meneja wa mauzo na matangazo Catherine Nyokabi Wambugu, ambaye pia ni binti ya mtafiti huyu.
Mara ya kwanza baada ya upanzi, Wambugu Apples huzalisha karibu matunda 20, idadi hii ikiongezeka kila msimu. Kulingana na utafiti wa mkulima huyu ni kwamba, mavuno ya kwanza, mengi ya mitofaha inazalisha ikiwa na urefu wa futi mbili.
“Kiwango cha mavuno huongezeka kila msimu, cha muhimu ni kuyatunza kwa maji na mboleahai (ya mifugo),” adokeza Bw Wambugu, akiongeza kuwa yana misimu tatu kwa mwaka.
Soko lake kuu la miche limekuwa mataifa ya kigeni, Barani Afrika; Nigeria, Zimbabwe, Botswana, Ghana na Cameroon. Marekani na Israili pia ni baadhi ya wanaotambua umuhimu wa Wambugu Apples.
Agnes Omingo ambaye ni mkulima Ongata Rongai, Kajiado ni mmoja wa wateja wa Wambugu Apples. Kajiado hukumbwa na kiangazi, na amepanda mitufaha 100 kwenye robo ekari.
“Nilianza ukulima wa matunda haya Julai 2017. Mavuno ya kwanza yalikuwa Aprili 2018, hayakuwa mengi. Ninaendelea na ya pili na kufikia sasa nimevuna kilo 500, yanaendelea kuchana maua na kuzalisha,” asema Bi Agnes.
Mche mmoja wa Wambugu Apples unagharimu Sh1,000 huku tofaha akiuza Sh50 kwa bei ya kijumla na Sh100 rejareja. “Msimu wa kwanza ni tosha kurejesha gharama ya miche. Ni matufaha utakayovuna kwa muda mrefu,” anasema Wambugu.
Pongezi
Amepongezwa na baadhi ya wateja nchi za kigeni wakihoji yanazalisha hata zaidi ya matunda 1,000 kwa msimu.
Hapa nchini Mama Ngina Kenyatta, mke wa Rais mwanzilishi wa taifa hili Hayati Mzee Jomo Kenyatta na mama ya Rais wa sasa Uhuru Kenyatta ni baadhi ya viongozi tajika waliomzuru kuthibitisha Wambugu Apples.
Laikipia ni miongoni mwa kaunti zinazoshuhudia kiangazi, na ndiko mkulima huyu ameyapanda. Eneo la Ngobit, Laikipia Mashariki, ufugaji na kilimo cha mahindi ndio umeshika kasi. Katika shamba la Bw Wambugu, ekari tatu imesitiri matofaha.
Anafichua kuwa ekari moja ina mitofaha 500. Wakati wa mahojiano, tulipata baadhi ikichana maua na mingine ikizalisha.
“Watu hudhani dhahabu ni ile ya kuchimbwa pekee, la hasha. Wambugu Apples ni dhahabu aliyonitunuku Mwenyezi Mungu. Matunda haya ni dhahabu jangwani,” aelezea, akihimiza serikali ipigie upatu kilimo cha matunda haya ili kuangazia upungufu wake.