Mkulima alivyovamiwa na nyani Murang’a
NA MWANGI MUIRURI
MKULIMA wa kiume katika Kaunti ya Murang’a anauguza majeraha baada ya kuvamiwa na genge la tumbili alipokuwa akihepa na mtoto wa wanyama hao.
Kwa mujibu wa mdokezi, mkulima huyo alikuwa amechoka kuharibiwa mimea yake na tumbili hao na ndipo aliweka mitego kuwanasa.
“Baada ya siku kadha, mtego mmoja ulinasa mtoto wa tumbili. Mkulima huyo alifika na akampata mtoto huyo akitoa sauti za dharura akijaribu kujinasua huku nao tumbili wengine wakirukaruka na kupiga makelele kwa hamaki karibu na mtego huo,” akasema mdokezi wetu.
Mkulima kwa furaha yake ya kisasi alimtwaa mtoto huyo wa nyani kutoka kwa mtego na akaanza safari ya kwenda naye nyumbani kwake.
“Alipewa ushauri mtaani kwamba akifanikiwa kumnasa tumbili mmoja, amchinje na amkatekate vipande vipande vya kuweka katika maeneo tofauti ya shamba lake wanyama hao wataogopa,” akasimulia mdaku wetu.
Akiwa amebeba mtoto wa tumbili aliyekuwa akilia kwa taharuki kuu, mkulima hakujua ni nani aliyewapa tumbili hao ujasiri wa kumvamia.
“Mimi nilijisikia tu nikiwa katikati mwa tumbili kama 10. Nilijaribu kupiga kelele nikiwatisha lakini wengine waliruka kwa mgongo, mabega na kwa kichwa…Wengine walinishika miguu na kabla nijue jinsi ya kujinusuru, nilikuwa nimeangushwa chini,” akakariri mkulima huyo akiwa hospitalini.
Alisema kwamba alihisi uchungu sana, kukwaruzwa na kuchapwa na nyani hao na kwamba angekufa iwapo majirani wake hawangemwokoa.
“Tulikimbia shambani mwake kumnusuru tukiwa na na mapanga. Tumbili hao walimchukua mtoto wao na wakaruka kwenye miti huku sisi tukibakia kumnusuru mwenzetu. Hali yake si mbaya lakini alikipata cha mtema kuni. Amejaa majeraha mwilini na angeuawa iwapo hatungefika kumwokoa,” akasema jirani.